Pages

Monday, March 2, 2020

BILIONI 50 KUJENGA KIWANJA CHA NDEGE CHA MTWARA



Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (katikati), akielekeza jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mtwara, Mhandisi, Dotto Chacha (Wa Kwanza Kulia), alipofika kukagua hatua za ujenzi zilizofikiwa katika mradi wa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mtwara, Mhandisi, Dotto Chacha, akimuonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi,
Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga (kulia), hatua ya ujenzi iliyofikiwa ya upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Mtwara.
Muonekano wa upanuzi wa kiwanja cha Ndege cha Mtwara ukiwa katika hatua za awali. Mradi huo umefika asilimia 31 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2020.
PICHA NA WUUM
**************************
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amesema kuwa ameridhishwa na mradi wa
upanuzi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Mtwara ambao unajengwa na mkandarasi M/S Beijing
Construction Engineering Group Company Ltd na kugharimu shilingi Bilioni
50.3.

Akizungungumza wakati akikagua kiwanja hicho ambacho utekelezaji wake umefika asilimia 31, Mwakalinga, amesema kuwa kukamilika kwake kutafungua fursa nyingi za uwekezaji katika mkoa huo na kutasaidia kurahisisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mwakalinga amebainisha kuwa mkandarasi anaendelea kutekeleza kazi zake vizuri kwani kazi nyingi za awali ambazo zinahusisha upanuzi wa uwanja huo zimefanyika kwa asilimia kubwa.

“Hadi sasa kazi inaendelea vizuri, ukiangalia kazi nyingi za awali zimeshafanyika, kinachotakiwa kwa sasa ni kwa mkandarasi kuendelea na hatua zinazofuata ili kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba”, amesema Mwakalinga.

Ametaja kazi hizo kuwa ni kuchimba eneo kwa ajili ya kuacha nafasi ya kuweka tabaka mbalimbali za barabara ya kurukia na kutua ndege pamoja na kuweka lami nyepesi juu ya tabaka lililochanganywa na saruji katika barabara hiyo ambayo imefika asilimia 46.

Aidha, ameongeza kuwa kiwanja hicho ambacho kilijengwa kwa mara ya kwanza na kuanza kutoa huduma katika miaka ya 1952/53 hakikidhi mahitaji ya ukuaji wa uchumi, hivyo Serikali imeamua kupandisha daraja kiwanja hicho ili kuweza kuhudumia ndege kubwa za ndani na nje ya Nchi.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mtwara, Mhandisi, Dotto Chacha, amesema kuwa upanuzi wa kiwanja hicho unahusisha ujenzi wa barabara ya magari ya
kuingia na kutoka kiwanjani pamoja na maegesho ya magari.

“Tunatarajia ujenzi huu utakidhi viwango vya kimataifa kwa kuongeza daraja kutoka code 3C ya sasa kwenda code 4E na itahusisha ujengaji wa uzio wa usalama kuzunguka kiwanja, uwekaji wa mfumo wa umeme wa akiba, vifaa vya zimamoto pamoja na taa na alama za kuongozea ndege”,
amefafanua Chacha.

Katika hatua nyingine, Mwakalinga, amekagua barabara ya Mtwara- Nanyamba- Tandahimba-Newala-Masasi sehemu ya Mtwara- Mnivata (Km 50) ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.67 Mwakalinga amebainisha kuwa asilimia hiyo inahusisha ujenzi wa makalvati madogo 41 kati ya 43 pamoja na ujenzi wa makalvati makubwa
manne kati ya sita yamekamilika kwa asilimia mia.

Awali wakati akielekea mkoani Mtwara, Mwakalinga alikagua mizani wa sisi kwa sisi uliopo mkoani Ruvuma na kuwataka watumishi wa mizani hiyo kuwa mfano wa kuigwa na watumishi wengine kwa kuepuka vitendo vya
rushwa na kufanya kazi kwa uadilifu.

No comments:

Post a Comment