Pamoja
na kujadili masuala mbalimbali ya mahusiano ya pande mbili (bilateral
relations), viongozi hawa walizungumzia utayari wa Serikali wa nchi zote
mbili katika kupambana na mgonjwa wa COVID-19. Sambamba na utayari huo,
Katibu Mkuu alimfahamisha Balozi Wang Ke kuhusu hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupambana na kuenea kwa
ugonjwa wa virusi vya corona. Wakati huohuo, alimweleza kuhusu utayari
wa Serikali kushirikiana na wadau wengine duniani ikiwemo China katika
kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona.
Vilevile,
Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu
wa China, kwa jitihada kubwa walizozifanya kiasi cha kufanikiwa
kudhibiti kuenea zaidi kwa COVID-19 nchini humo na jitihada
wanazozifanya ikiwemo kusaidia wataalamu, vifaa tiba na vya kujikinga
kwa Mataifa mengine duniani ambapo COVID-19 inaendelea kuleta madhara.
Hadi sasa China imefanya mazungumzo na nchi 24 za Afrika ikiwemo
Tanzania yanayolenga kushauri na kubadlishana uzoefu na taarifa muhimu
zitakazo saidia kutokomeza COVID-19.
Aidha,katika
mazungumzo hayo Balozi wa China nchini Mhe. Wang Ke amebainisha
kuridhishwa kwake juu ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya
Tanzania katika kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa wa
virusi vya corona. Balozi Wang Ke aliongezea kusema pamoja na kutokuwepo
maambukizi mapya nchini China, Serikali ya nchi hiyo bado inaendelea
kuchukua tahadhari na hatua za kuzuia maambukizi mapya, na kuwa
wataendelea kutoa mchango kwa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na
COVID-19. Balozi Wang Ke amesisitiza kuwa, Serikali ya China ipotayari
kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi
ya COVID-19.
Katibu
Mkuu ameushukuru Ubalozi wa China kwa utayari wake wa kushirikiana na
Tanzania dhidi ya mapambano ya COVID-19, na kueleza kwamba Wizara
itawasiliana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili
kuandaa orodha ya mahitaji ambayo Ubalozi wa China unaweza kusaidia.
Katibu Mkuu alirejea kauli ya Serikali kwamba mapambano dhidi ya virusi
vya corona ni vita ambayo Tanzania haina budi kukabiliana navyo, kwa
ujumla wake na kwamba hatua zote ambazo Tanzania inachukua chini ya
uongozi wa Waziri Mkuu zinalenga kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo
bila kuathiri shughuli za kila siku. Alisistiza kwamba Tanzania
inaamini kwa jitihada inazochukua na kwa ushirikiano kutoka China
itafanikiwa kushinda janga hili.
Mwisho,
Balozi Wang Ke alimpongeza Katibu Mkuu kwa kuendelea kufanya mikutano
na Waheshimiwa Mabalozi licha ya changamoto iliyopo ya COVID-19 kwa
kuweka utaratibu wa kufanya kwa mikutano hiyo kwa njia ya Video akiwa
Ofisini kwake Mtumba, Dodoma wakati Mabalozi wakiwa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment