Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa
Mhandisi wa Ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Injia Kazoba
Wilson (kushoto) wakati akitoka kukagua maendelezo ya ujenzi wa
hospitali hiyo jana Musoma mkoani Mara. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya
ya Musoma Dkt Vincent Naano Anney.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia utengenezwaji
madirisha ya Alminium kwa ajili ya kuwekwa katika Hosiptali ya Rufaa ya
mkoa wa Mara alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi huo jana Musoma
mkoa wa Mara. Kushoto ni Mhandisi wa Ujenzi wa mradi wa Hospitali hiyo
Injia Kazoba Wilson.
Jengo la hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara lililopo eneo la Kwangwa Musoma likiwa katika hatua za ukamilishaji.
(PICHA NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
……………………………………………………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM, MUSOMA
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameridhishwa na
kasi ya
ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyoko
Kwangwa Musoma unaogharimu takriban Bilioni 15.082.
Dkt Mabula
aliridhishwa na kasi ya mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo alipokwenda
kukagua maendeleo ya ujezi wake jana wakati akiwa katika ziara ya siku
moja mkoani Mara.
Alisema, ujenzi
wa mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa Mara sambamba na mikoa na nchi
jirani kwa kuwa itakuwa ikitoa huduma za kitabibu kwa wananchi wa maeneo
hayo.
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alibainisha kuwa, hana mashaka na
Shirika la Nyumba la Taifa katika kutekeleza mradi huo kutokana na
Shirika hilo kufanya vizuri kwenye miradi mbalimbali inayosimamia.
‘’Kwa sasa sina
mashaka na Shirika la Nyumba la Taifa katika masuala ya ujenzi kutokana
na kufanya vizuri kwenye miradi mingi ya ujenzi inayosimamia lakini
kinachotakiwa hapa ni kukamilisha ujenzi kwa wakati’’ alisema Dkt Mabula
Ameitaja baadhi
ya miradi ya ujenzi inayofanywa na NHC na kufanya vizuri kwenye maeneo
mablimbali kuwa ni ujenzi wa ofisi kumi na saba za Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS), Hospitali ya Rufaa ya Kusini iliyopo Mtwara,
Ofisi ya wilaya ya Wang’ingombe na nyumba za wakuu wa wilaya za Hai na
Ulanga.
Kwa upande wake
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mara Goodluck Thomas
alisema Shirika lake katika kutekeleza mradi huo tayari baadhi ya kazi
zimekamilishwa ikiwemo jengo la Huduma ya Mama na Mtoto, nyongeza ya
ghorofa moja na kupaua, kupiga plaster nje na ndani, maandalizi ya
rangi, fremu za milango pamoja na kuweka marumaru.
Kwa mujibu wa
Goodluck, kazi zinazoendelea sasa ni uwekaji mifumo ya maji safi na maji
taka, kazi ya umeme, uwekaji mifumo ya gesi, ufungaji madirisha ya
alminiuam na ukamilishaji kazi nyingine ukiendelea na mradi wa ujenzi wa
hospitali hiyo umefikia asilimia 65.
Mkuu wa wilaya ya
Musoma Dkt Vincent Naano Anney alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa
wakati ujenzi wa hospitali hiyo ukiendelea kukamilishwa kuna haja kwa
mamlaka husika kuanza kuangalia mahitaji ya Wataalamu na Vifaa
vinavyohitajika kwenye vitengo mbalimbali vya hospitali hiyo na
kubainisha kuwa kazi hiyo isipofanyika mapema kuna hatari ujenzi
utakapokamilika hospitali hiyo ikakosa wataalamu wa kutosha kutokana na
ukubwa wake.
No comments:
Post a Comment