Pages

Wednesday, March 4, 2020

DAWASA YAMKABIDHI RC NDIKILO MRADI WA MAJI KISARAWE UTAKAOZIMA KILIO CHA MAJI TANGU 1907



……………………………………………………………………………………
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
Mamlala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) ,imekabidhi mradi wa maji Kisarawe kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ,mradi ambao umegharimu kiasi cha sh.bil 10.6 na unakwenda kuondoa kilio cha maji kilichodumu
tangu mwaka 1907.
Aidha mradi huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni sita huku wilaya nzima ya Kisarawe ikiwa na uwezo wa kutumia lita milioni 1.2 pekee hivyo maji yatakuwa mengi zaidi ya mahitaji.
Mhandisi, Ndikilo alisema Kisarawe ilitaabika kwa kipindi kirefu lakini sasa serikali ya awamu ya tano inajibu hiyo kwa vitendo na kutekeleza ilani ya CCM ya kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Akitembelea mradi huo baada ya kutokea kukagua tanki la Kibamba hadi Kisarawe kwenye tenki la kuhifadhia maji,alieleza inatakuwa vyema mradi huo uzinduliwe na Rais dk.John Magufuli.
“Mradi huu umekamilika kama maagizo ya Rais mwenyewe kwa Mamlaka hiyo wakati wa uzinduzi wa Chanzo cha maji Ruvu Juu na kuelekeza wapeleke maji Kisarawe ambapo mamlaka hii imeutekeleza agizo kwa muda mfupi”alieleza Ndikilo.
Akikabidhi mradi huo ,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Cyprian Luhemeja
alieleza,wameshakamilisha ujenzi wa mradi huo kwa miezi 11 na tayari wananchi wameshaanza kupata huduma ya maji.
“Mradi huu tulitumia fedha zetu za ndani takribani Bilioni 10.6 mahitaji ya wananchi hapa ni lita milion 1.2 na tenki linahifadhi maji Lita Milion 6 ,Hadi kufikia sasa maunganisho ya wateja wapya 1200 yameshafanyika na kulaza karibia km 33 za usambazaji wa maji kupeleka kwa wananchi”alifafanua Luhemeja.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo aliishukuru serikali ya awamu ya tano na Dawasa kwa kufanikisha upatikanaji wa maji ndani ya Wilaya ya Kisarawe.
Alisema,maji ni mkombozi kwa wananchi wa Kisarawe na sasa hakutakuwa na shida ya maji na eneo la viwanda Visegese umeme ukishafika na maji basi pia kutakuwa hakuna tatizo kwa wawekezaji.
Ziara hiyo iliendelea wilaya ya Mkuranga ambako, mhandisi Luhemeja alieleza wanatekeleza mradi wa maji utakaogharimu bilioni 5.6 hadi Vikindu.
Mtendaji huyo mkuu DAWASA ,alisema, mradi huo unatarajiwa kumalizika mwezi april kwa awamu ya kwanza,visima viwili vimekamilika, na awamu ya pili kwa Vikindu itamalizika mwezi June.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga alibainisha, adha ya maji ni ya muda mrefu lakini anaipongeza Dawasa kwa kutatua changamoto hiyo.

No comments:

Post a Comment