*********************************
WADAU wa mikutano ya mashauriano
kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji wameendelea kupatiwa
elimu kuhusiana na majukumu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), fursa
ya wajasiriamali kupatiwa bure alama ya ubora pamoja na kuzipatia
ufumbuzi wa changamoto zinawakabili.
Mikutano hiyo ya mashauriano kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa
inayojumuisha Mara, Simiyu, Shinyanga na Mwanza ilianza Jumatatu,
Februari 24, mwaka huu na kuhudhuriwa na mawaziri na manaibu waziri
zaidi ya nane ikiwa ni mwendelezo wa mikutano iliyotangulia inayolenga kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wafanyabiasha na wawekezaji.
Mkutano wa majumuisho ya mikutano
hiyo ya Kanda ya Ziwa ulifanyika jana jijini Mwanza. Katika mikutano
hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, alitoa elimu kwa wadau
hao kuhusu fursa wanazopata wafanyabiashara na wazalishaji ambao bidhaa
zao zimekidhi viwango vya ubora, kuhamasisha wajasiriamali kuthibitisha
ubora wa bidhaa zao bure pamoja na kuzipatia majibu changamoto
wanazokumbana nazo wadau mbalimbali.
Dkt. Ngenya alitaja fursa zinazotolewa na shirika hilo kwa
wajasiriamali kuwa ni pamoja kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha
bila malipo kwa miaka mitatu lengo likiwa ni kuwawezesha kupanua soko la
bidhaa zao na kuwaondolea vikwazo vya kibiashara.
Alisema Serikali imeanzisha utaratibu huo ili kuwasaidia
wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora na kupanua wigo wa masoko hayo.
wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora na kupanua wigo wa masoko hayo.
Alitoa wito kwa wajasiriamali na
wananchi kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo hasa katika kipindi hiki
ambacho Serikali inasisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda.
“TBS kama taasisi wezeshi inatoa
huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa bure kwa wajasiriamali wadogo na
wakati, lengo likiwa ni kuendeleza viwanda vya Tanzania, hivyo ni vyema
wakathibitisha ubora wa bidhaa zao ili wasipate vikwazo vyovyote katika
kupata soko ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt. Ngenya.
Alisema kuwa endapo wajasiriamali hao watathibitisha bidhaa zao itawasaidia kuzalisha bidhaa endelevu ambazo zitakuwa na soko kila mahali ikiwemo masoko ya kikanda.
Dkt. Ngenya, alifafanua kuwa lengo la TBS ni kuwawezesha
wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija kwa taifa, bila kuathiri
taratibu na sheria za nchi.
Kutokana na umuhimu huo, alisema
ndiyo maana shirika hilo limeshiriki mikutano hiyo kama taasisi wezeshi
kuzipatia majibu changamoto zinazowakabili wadau, kuwaelimisha kuhusu
majukumu ya shirika, maboresho kwenye masuala ya viwango na jinsi
shirika lilivyoondoa baadhi ya tozo ili kurahisisha ufanyaji biashara.
Alisema Shirika litaendelea kutoa
elimu ya viwango kwa Watanzania wote lengo kuu likiwa ni kuwa na uelewa
wa pamoja wa masuala ya viwango na ubora wa bidhaa zinazozalishwa ndani
ya nchi na zile zinaingizwa kutoka nje nchi.
No comments:
Post a Comment