Pages

Thursday, December 26, 2019

JAMII YAHIMIZWA KUPANDA MITI YA ASILI KWA MANUFAA YA KIZAZI KIJACHO NA KULINDA UOTO WA ASILI-SAGO


Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WANANCHI wa Mji wa Kibaha ,mkoani Pwani wamehimizwa kupanda miti ya asili ambayo ipo hatarini kutoweka pamoja na kulinda mazingira kwa faida na manufaa ya kizazi kijacho.
Aidha wananchi wameaswa kuacha kukata miti na misitu ovyo kwani kwa kufanya hivyo kunasababisha kuondoa uoto wa asili.
Rai hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la – SAHO-linalojishughulisha na masuala ya upandaji miti na kuhimiza kutunza mazingira , Emmanuel Sago wakati wa zoezi la ugawaji wa miti kwa kaya  na taasisi za serikali kata ya Visiga ,halmashauri ya Mji wa Kibaha.
Aliitaka jamii wakati ikipanda miti ya matunda na ya kisasa pia ipande miti ya asili ikiwemo mninga,mkwaju,mkongo ambayo ina faida zake katika kukuza uchumi pamoja na kuleta hewa safi .
Sago alifafanua, kwa mwaka huu wameotesha miche ya miti ya asili ipatayo 13,000 ambayo wanaisambaza iweze kupandwa taasisi za umma ikiwemo mashuleni ,kwa wananchi kata ya Visiga miche mitatu mitatu kwa kila kaya na kisha ngazi ya halmashauri .
“Mpango kazi huu tulianza miaka mitatu sasa ,katika kata hii,tulianzia taasisi za umma ikiwemo shule mbalimbali na jamii ili kuwa na uelewa wa kujua faida za miti hii kwa manufaa ya sasa na vizazi vinavyokuja” alisisitiza Sago.
Hata hivyo, alieleza, mpango kazi na mkakati uliopo kwa mwaka 2020 ni kuotesha miti 30,000 na kuigawa katika kaya na taasisi hizo.
Nae diwani wa kata ya Visiga Kambi Legeza aliishukuru SAHO kwa kuunga mkono juhudi za serikali ,”:’na kuelezea hali ya mazingira ni mbaya ,kwakuwa miti mikubwa inakatwa ovyo kwa ajili ya mkaa ,mbao hali inayosababisha kutoweka kwa miti ya asili.
Legeza alibainisha ,jitihada iliyopo kwa halmashauri hiyo ,ni kurejesha miti hiyo na kukemea uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake,Shabani Mchora kutokea Mchangani Visiga, alisema juhudi za shirika la SAHO zitasaidia kuweka mazingira bora na kuwapa wananchi uelewa wa kutunza mazingira.

No comments:

Post a Comment