Mkurugenzi wa mgodi wa kampuni ya
California Camp, Deo Minja akiongoza njia wakati Paroko wa Parokia ya
Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu, Padri Vincent Ole Tendeu (kulia)
akinyunyiza maji ya baraka kwenye eneo la mgodi.
************************************
WACHIMBAJI wa madini
ya Tanzanite wa kampuni ya California Camp eneo la Kitalu B (Opec) Mji
mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamefanya misa ya
kumshukuru Mungu kwenye mgodi huo kwa kumaliza mwaka salama bila kupata
ajali wala misukosuko katika shughuli zao.
Mkurugenzi wa mgodi
huo wa California camp, Deogratius Minja alisema wamefanya misa hiyo ya
shukrani katika mgodi huo ili kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka salama
na kufanya kazi zao bila matatizo.
Minja alisema kazi za
uchimbaji madini ya Tanzanite ni ngumu na wanamshukuru Mungu kupitia
misa hiyo ya shukrani kwa kuwaepusha na ajali kwenye mgodi wao.
“Shughuli za
uchimbaji madini ya Tanzanite ni ngumu na zinahitaji gharama kubwa
lakini tunamshukuru Mungu kwa mema yote aliyotujalia na kumaliza mwaka
2019 na kukaribisha mwaka mpya wa 2021,” alisema.
Paroko wa parokia ya
Bikira Maria Mama wa Rozali Takatifu wa Kanisa katoliki Mirerani, Padri
Vincent Ole Tendeu aliyasema hayo jana kwenye misa ya shukrani katika
mgodi wa madini ya Tanzanite Africa California camp.
Padri Ole Tendeu
alisema mara nyingi watu wana tafsiri potofu kwamba wachimbaji wa madini
ya Tanzanite hawapo karibu na Mungu jambo ambalo siyo sahihi.
Alisema tukio la misa
ya shukrani katika mgodi wa kampuni ya California camp imedhihirisha
kuwa wachimbaji madini ya Tanzanite wana imani kubwa kwa Mungu na
wanamtangukiza mbele katika shughuli zao za uchimbaji madini.
“Misa hii ya shukrani
iliyofanyika kwenye mgodi wa ndugu yetu Deogratius Minja kupitia
California camp imetuonyesha imani kubwa kwa Mungu walionao wachimbaji
madini ya Tanzanite,” alisema padri Ole Tendeu.
Katekista wa kigango
cha Mtakatifu Malaika mkuu Gabriel, Martin Mbuya alisema Mungu ni mwema
kwani wamefanikiwa kuwa na eneo la kufanya ibada katika machimbo hayo.
Mbuya alisema
wanamshukuru ofisa madini mkazi wa Mirerani Daudi Ntalima kwa kuwapa
fursa ya kupata eneo la kufanya ibada katika machimbo ya madini ya
Tanzanite.
Alisema hivi sasa
hakuna ushirikina kwenye madini hayo na wachimbaji wamemtambua Mungu na
wanatarajia Tanzanite itapatikana kwa wingi kutokana na imani waliyonayo
kwa Mungu.
No comments:
Post a Comment