Na Lillian Shirima–Maelezo
Imetimia miezi 48 sasa sawa na
miaka minne tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli alipochukua jukumu rasmi la kuiongoza nchi Novemba 5,
2015.
Kiongozi huyu amefanikiwa
kuhakikisha watanzania wanatoka hatua moja kwenda nyingine
kimaendeleo
badala ya kubaki kama walivyo miaka nenda miaka rudi. Aina ya uongozi wa
rais Magufuli umeonesha uwezo au karama ya kuondoa taratibu zilizooleka
katika jamii na kisha kubuni, kuelekeza njia sahihi kwa vitendo ni
ushindi wa mafanikio katika uongozi wake.
Katika kipindi kifupi rais
Magufuli amekuwa gumzo ndani na nje ya nchi kutokana na uwezo alionao
kushawishi watu kufikia maendeleo yaliyotarajiwa kwa kuondoa taratibu
zisizofaa kama vile uzembe kazini, ubadhirifu wa mali ya umma, na
huduma mbovu za jamii kama vile maji safi na salama, elimu, afya.
Akihojiwa na Idara ya Habari
Maelezo mchambuzi na mtafiti wa wa masuala ya uchumi na siasa Dkt.
Bravious Kahyoza anamuelezea Rais John Pombe Magufuli kama kiongozi
mwenye uthubutu wa kuamua mambo mazito na kuyatekeleza kwa wakati kwani
ameweza kuvunja taratibu zisizofaa ambazo zilikuwa kizingiti cha
maendeleo ya nchi jambo ambalo limemjengea imani kwa wananchi .
“hakuna jinsi nyingine kubwa ya
kuhakikisha watu wanatoka hatua moja kwenda hatua nyingine kama
taratibu za maisha yao zinabaki zilivyo na tafsiri za kiuchumi duniani
zinaonesha kuwa maendeleo ya watu kiuchumi yanahusiana na utaratibu wa
maisha ya watu wenyewe, Rais wetu amevunja taratibu korofi ”. Anasema Dkt. Kahyoza.
Aidha, ameongeza kuwa
kinachomtofautisha rais Magufuli na viongozi wengine kiasi cha
kusababisha awe gumzo ndani na nje ya nchi ni muda mfupi aliotumia
kuleta mageuzi makubwa nchini. Pia namna alivyoonesha mfano wa kubana
matumizi katika kutekeleza majukumu yake kama kiongozi wa nchi.
Mwandishi David Lender katika kitabu chake cha ‘The
Wealth and Poverty of Nations: why some are so rich and some are so
poor (Utajiri na Umasikini wa Mataifa: kwanini mengine ni tajiri na
mengine masikini. Kitabu hicho kimeeleza kwamba mataifa ambayo
yameweza kuwa na sehemu kubwa ya mabadiliko kati ya miaka 1961 na 2014
ni yale yaliyobadilisha taratibu na tabia za watu zilizooeleka na
kuzielekeza kwenda kwenye mtazamo wenye tija kwa taifa lao, miongoni mwa
mataifa hayo ni ulaya na Asia katika nchi za Uingereza, Japan na Afrika
ni nchi za Namibia, Botswana, Rwanda na Ethiopia.
Anasema, mfano hai ni kama vile
uandaaji wa sherehe za kitaifa za gharama kubwa, sherehe wakati wa
uteuzi wa viongozi mbalimbali, kumbukumbu za kitaifa, sherehe za uhuru,
muungano na uzinduzi wa miradi ambapo fedha nyingi hutumika kusherehesha
wakubwa serikalini na baadhi ya jamii.
Rais Magufuli alichukua hatua ya
kubatilisha taratibu za ufanyaji wa sherehe hizo kwa kufanya kazi za
kijamii kama vile usafi, kuhudumia wagonjwa na mara kadhaa kutumia fedha
husika kwa ajili ya manufaa ya taifa ambapo sherehe za maadhimisho ya
miaka 54 ya uhuru aliagiza fedha zitumike kwenye ujenzi wa barabara ya
Mwenge hadi Morocco.
Pia, Rais Magufuli alipounda
Baraza la Kwanza la Mawaziri 2015, Baraza lilikuwa mawaziri 19 tu huku
baadhi ya wizara zikibaki bila naibu mawaziri. Rais aligiza kiasi cha
shilingi bilioni 2 zilizokuwa zitumike kwaajili ya semina elekezi kwa
viongozi wapya zipelekwe Wizara ya Elimu kutunisha fungu la elimu bure
ikiwa ni pamoja na kununua madawati ya wanafunzi.
Rais hakuishia hapo, alizuia
safari za viongozi nje ya nchi zisizokuwa za lazima na yeye mwenyewe
kupunguza safari zake nyingi nje ya nchi na kuagiza balozi kumwakilisha
katika masuala ya Kimataifa.
Aidha, uzoefu wake katika
kulitumikia taifa kwa muda mrefu, aligundua ndani ya utumishi wa umma
yapo makundi mawili ya wafanyakazi wanaolipwa mshahara kwa mazoea. Kundi
la kwanza ni watumishi ambao kwenye kumbukumbu za utumishi wanaonekana
waajiriwa wa serikali wanaolipwa stahiki zote za utumishi lakini si
watumishi ambao kwa idadi walikuwa 20,000.
Kundi la pili ni watumishi ambao
kwa mazoea wanafanya kazi lakini hawana sifa kwa nafasi walizonazo kwa
idadi walikuwa 14,000. Watumishi hao baadhi walitumia vyeti visivyo
sahihi kuajiriwa na wengine walifanya kazi za taaluma ambazo hawakuwa na
ujuzi nazo.
Kwa mamlaka aliyonayo, Rais
Magufuli alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa kuhakikisha watumishi wa aina
hiyo wanaondolewa sehemu zao za kazi. Zaidi ya watumishi 10,000
walipoteza ajira na serikali iliokoa zaidi ya shilingi Bilioni 15 za
mishahara hewa huku Wakuu wa Mikoa walioshindwa kutekeleza agizo hilo
kwa usahihi nyadhifa zao zilitenguliwa.
Pengine hali hii ndio iliyokuwa
inasababisha hasira dhidi ya serikali kwakuwa wananchi hawakuona huduma
zinatolewa kama zinavyostahili. Dkt. Kayhoza alisema kuwa nanukuu maneno
ya rais Magufuli “Naagiza wakuu wote wa mikoa hakikisheni watumishi
hewa yaani ambao hawapo wanaondolewa kwenye orodha ya utumishi na sehemu
zao za kazi’.
Pia, matokeo yake ndani ya kipindi
kifupi serikali iliweza kutangaza nafasi za kwa wenye sifa katika sekta
nyingi mathalani Tamisemi ilitangaza ajira mpya kwa walimu wa shule za
msingi na sekondari pamoja na sekta ya afya na nyingine nyingi.
Hii leo watanzania tunaona mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika utumishi wa umma.
Dkt. Kayhoza anasema, Rais
Magufuli ameonyesha dhahiri kuwa kiongozi bora asiye mlalamishi bali ni
kiongozi anayetafuta ufumbuzi wa kila changamoto anayokutana nayo.
Aidha, ni kiongozi mwenye uthubutu , maamuzi sahihi, mtekelezaji,
mfuatiliaji wa maamuzi yake mpaka yanapokamilika.
“Hii inaonesha dhahiri uwezo
alionao wa kuzisoma nyakati na kuhakikisha nyakati hizi zinaweza
kutafsiriwa si tu kwa nchi anayoiongoza lakini pia kuangalia uchumi wa
nchi unategemea masuala gani yanatokea na namna gani yanaweza kusaidia
nchi kwenda mbele”. Amesema Dkt Kahyoza.
Maamuzi mengine aliyoyafanya ni
serikali yake kuhamia Dodoma. Hadi sasa Mawaziri wote chini ya Waziri
Mkuu, Naibu Mawaziri, Makatibu na Kurugenzi zote muhimu zimehamia
Dodoma.
Uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma
haukupewa kipaumbele kwa zaidi ya miaka 40 iliyopita tangu ulipoasisiwa
na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye 1970.
Kutokana na umuhimu wa kuhamia Dodoma watumishi wa serikali waliokuwa
makao makuu walihamia Dodoma. Hili ni funzo kwetu ambapo tukiamua
tunaweza kwani ndani ya matumizi na mazingira yetu ya kawaida
inawezekana tukapanga na tukatekeleza mambo yetu wenyewe kwa ufanisi.
Akitoa mfano juu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kufua umeme katika Mto Rufiji Dkt. Kahyoza amesema “Licha
ya mradi huu utakaozalisha kilowati 2115 za umeme kupingwa na
kukabiliwa na vizingiti ndani na nje ya nchi, Rais Magufuli ameweza
kuvunja vizingiti hivyo ambapo Julai mwaka huu alizindua rasmi ujenzi wa
bwawa la mto Rufiji utakaogharimu fedha za Tanzania za shilingi
trilioni 6.5.
Suala lingine ambalo rais Magufuli
aliahidi kupambana nalo ni ukusanywaji wa kodi ambapo ukaguzi kwa kila
sekta umekuwa mkubwa na matokeo yake ni kuongezeka kwa mapato ya taifa
kutoka shilingi milioni mia nane kwa mwezi hadi kufikia shilingi
trilioni 1.7 Septemba, 2019.
Rais alisema“unapouza toa risiti na unaponunua dai risiti”.
Alianza kwa kusisitiza kwa mtu mmoja mmoja kudai risiti kwa kila huduma
anayopatiwa na baadaye akahimiza wafanyabiashara kulipa kodi ikiwa ni
pamoja na taasisi za serikali kulipa kodi baada ya kupatiwa huduma au
bidhaa.
Hali hii imeleta mageuzi kwa kila mfanya biashara kuwa na mashine ya EFD (Eletronic Fiscal Divice) kitu ambacho hakijawahi kutokea miaka iliyopita. Amemalizia Dkt. Kayhoza
Naye Projestus Rwegarulila
Mkurugenzi wa Mradi wa Utamaduni na Uzalendo anasema, Rais Magufuli
amekuwa mstari wa mbele kutumia lugha ya Kiswahili kwenye mikutano
mbalimbali ya Kimataifa anayoshiriki jambo halijawahi kufanyika kwa
viongozi wetu hivi karibuni.
“Kitendo cha Rais kuongea
Kiswahili kwenye mikutano ya kimataifa kimewalazimu wasiojua lugha hiyo
kutafsiriwa na wengine kuamua kujifunza Kiswahili”. Anasema Rwegarulila.
Anasema, pamoja na watu kuvutiwa
na kile anachozungumza Rais kwenye mikutano, kasi ya maendeleo ya
Tanzania kwenye sekta mbalimbali ndiyo inawavuti wageni kuja kujifunza
namna ambavyo nchi imepiga hatua kama vile mradi kama vile mwendo kasi,
kuanzishwa kwa sera sera mpya ya madini, ujenzi wa bwawa kubwa la
kuzalisha umeme ni baadhi ya baadhi ya mambo yanayoamsha kiu ya mataifa
mengine kujifunza kutoka kwetu.
Na hakuna lugha nyingine isipokuwa kutafsiri Kiswahili katika lugha zao.
Naye mwanafunzi Hamida Khamis wa
shule ya msingi Bunge jijini Dar es Salaam amesema kabla ya serikali ya
awamu ya tano shule yao haikuwa na madawati ya kutosha, wanafunzi
walikuwa wanasukumana kutafuta nafasi za kukaa kwenye dawati lakini
mpango wa elimu bure umefanikisha shule kupata madawati ya kutosha.
Mkazi wa Mugumu Serengeti Herman
Peter yeye anasema, kabla Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani
huduma za afya zilipatikana katika Halmashauri ya Serengeti tu lakini
sasa huduma zimesogezwa karibu baada Serikali kujenga Kituo cha Afya
katika kata yao ya Nata kwa gharama ya shilingi milioni 400.
Nimalizie kwa kusema vema
tukafahamu Rais John Pombe Magufuli ameweza kuondoa taratibu zilizokuwa
zikichelewesha nchi kusonga mbele. Hakuleta sheria mpya au sera mpya,
alichokifanya ni kuhakikisha yeyote anayepewa dhamana ya uongozi
anatimize wajibu wake, anaposhindwa kuleta mabadiliko ndani ya muda
mfupi anamwondoa katika madaraka aliyokuwa nayo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
No comments:
Post a Comment