Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa (kushoto) wakati
alipokagua kazi ya kusafirisha korosho kwemye bandari ya Mtwara, Oktoba
1, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw.
Renatus Mkinga wakati alipotembelea bandari ya Mtwara kukagua kazi ya
usafirishaji wa korosho, Oktoba 1, 2019.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ametembelea bandari ya Mtwara na ameshuhudia shehena ya korosho
ziliyonunuliwa na kampuni ya Tang Long zikipakiwa katika meli kubwa
yenye
jina la AS Christiana kwa ajili kusafirishwa kwenda nchini
Vietnam.
“Ni faraja kuona mzigo wa
korosho ukiondoka na kutoa nafasi ya kuingiza mzigo mwingine mpya wa
korosho utakaopatikana baada ya kuanza msimu mpya mwezi huu. Na mnunuzi
huyu ameahidi kununua tani 100,000 katika msimu wa mwaka huu.”
Waziri Mkuu ametembelea
Bandari ya Mtwara leo (Jumanne, Oktoba 1, 2019) kwa ajili ya kujionea
kazi ya usafirishaji wa korosho inavyofanyika na amesema kwamba
ameridhishwa na kasi na utaratibu unaoendelea badarini hapo.
Amesema kampuni ya Tang Long
ya nchini Vietnam licha ya kuahidi kununua korosho katika msimu wa mwaka
huu, pia imeomba kupatiwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha
kubangua korosho nchini na kwamba wapo tayari kuanza hata Desemba, 2019.
Waziri Mkuu amesema suala la
ujenzi wa viwanda vya kubangulia korosho nchini litaongeza thamani na
kuwezesha dunia nzima kutambua kuwa korosho hizo zimetoka Tanzania kwa
sababu kwenye vifungashio watakuwa wameandika, hivyo kuongeza soko.
Akizungumzia kuhusu msimu wa
uuzaji wa korosho wa mwaka huu, Waziri Mkuu amesema kipaumbele cha
kwanza watapewa wenye viwanda vya ndani na kisha tani zinazobaki
zitauzwa kwa wanunuzi kutoka nje.
“Wito wa Rais Dkt. John
Magufuli wa ujenzi wa viwanda unalenga katika kuongeza ajira kwa
wananchi kwa kuwa viwanda vinaajiri watu wengi wenye kada tofauti. Wakuu
wa mikoa endeleeni kurahisisha mazingira ya uwekezaji.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Geoffrey Mwambe amesema licha
ya kampuni ya Tang Long kununua korosho nchini pia imeomba ikodishwe
kiwanda kimojawapo cha Serikali ili waweze kuanza ubanguaji wa korosho
ikiwa ni mpango wa muda mfupi na katika mpango wao wa muda mrefu
wameomba eneo kati ya mkoa wa Lindi au Mtwara ili wajenge kiwanda cha
kubangua korosho. Taratibu zinaendelea.
No comments:
Post a Comment