Pages

Monday, September 30, 2019

PUMA ENERGY TANZANIA YAMCHANGIA RC MAKONDA SHILINGI MILIONI 40 KUFANIKISHA MATIBABU YA MOYO KWA WATOTO 20 DAR



Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya mafuta ya Puma Energy imeunga mkono kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya  kuokoa maisha maisha watoto wanaogua ugonjwa wa moyo kwa
kuchangia Shilingi milioni 40 ili kufanikisha upasuaji kwa watoto 20.
Mbali na kutoa fedha hizo kwa ajili ya kusaidia matibabu ya moyo kwa watoto hao, Kampuni hiyo ya mafuta ya Puma Tanzania imetoa zawadi kwa shule ya Msingi Kibamba pamoja na mwanafunzi wa shule hiyo kwa kushinda mchoro wa elimu ya usalama barabarani.
Akizungumza leo Septemba 30,2019 jijini Dar es Salaam wakati wa kikabidhi fedha hizo Mkurugenzi wa Puma Energy Dominic Dhanah, amesema hatua ya kuunga mkono kampeni hiyo ni kuhakikisha wanaokoa maisha ya watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu.
Amesema kampuni hiyo inatambua dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kusadia makundi yenye mahitaji maalum na ndio maana wameona kuna kila sababu ya kumuunga mkono Makonda katika kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo ambao wanahitaji kufanyiwa operesheni.
Kuhusu mafunzo ya usalama barabarani kwa watoto wa shule za msingi, amesema yamesaidia kupunguza ajali katika maeneo ambayo wametoa mafunzo hivyo wanaamini kwa kufanya hivyo wanaokoa kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa elimu ya matumizi bora ya barabara inaendelea kusambaa.
Ameongeza kuwa lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto hao kuwa na uelewa wa matumizi ya barabara wakiwa bado wadogo. “Tunaamini kwa kufanya hivyo tunawaongezea uelewa kuhusu dhima nzima ya usalama barabarani kwa wa Tanzania wengi zaidi,” amesema Dhanah.
Amesema kazi hiyo kwa mwaka huu imefanyika katika mikoa ya Dodoma na visiwani Zanzibar ambapo jumla ya shule 34 zitafikiwa kwa mpango huu kwa mwaka 2019.
“Lengo letu kama kampuni ni kuongeza wigo ili kufikia shule nyingi Zaidi nchi nzima. Pia tutaendelea kuwekeza katika kampeni ya usalama barabarani ikishirikiana na serikali kupitia Jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya Watanzania,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuwa  Kampuni ya Puma, imetoa kiasi cha Sh milioni 40 kwa ajili ya kugharamia matibabu ya watoto 20 ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo lakini wazazi mwao hawana uwezo wa kulipia matibabu.
“Puma wameonesha njia ya kujali na kutusaidia kwenye moyo. Niliomba msaada huo katika mkutano wa SADC. Nina watoto 500 pale Muhimbili wanaumwa moyo.
“Mimi nikialikwa mahali ninaomba msaada kwa wananchi wangu. Dominic wa Puma nilimuomba na gharama za matibabu kwa kila mtoto ni Shilingi milioni mbili kwa kiasi hiki cha fedha Shilingi milioni 40 sasa tunakwenda kurudisha tabasabu kwa watoto 20.
“Watapata operesheni kwakuwa sehemu ya faraja na mafanikio kwa mtoto atakayefanyiwa opesheni. Hata nilipokutana na Balozi wa Dubai baada ya kumueleza hili, yeye alikwenda kuleta madaktari ambao walifanya upasuaji wa matibabu kwa watoto 50.
“Mwezi ujao nitaunda kamati ya watu saba kwa ajili ya kusaka Shilingi bilioni moja, ili mpaka tukifika Desemba mwaka huu watoto wote wawe wamefanyiwa upasuaji,” amesema Makonda
Kuhusu idadi ya watu wanaopata ajali za barabarani, alisema kuwa kwa sasa imepungua kutokana na elimu ya usalama barabarani.
“Tuna imani watoto 1m atakuwa na uelewa iwapo wataelimishwa na wenzao. Watumia vyombo vya moto watambue kila mmoja ana jukumu la kufuata usalama barabarani. Kabla ya Desemba kutakuwa na check up ya bure kwa wanaotaka kwenda likizo.
“Mafundi wa bure watakuwapo, nataka waende vizuri kula likizo na warejee tena Dar wakiwa salama. Trafiki kwenye mwendokasi inafanya vibaya,” amesisitiza.
Hata hivyo Makonda aliagiza kukamatwa kwa madereva wanaotumia barabara za mwendokasi.
“Wanatumia barabara ya mwendokasi wakamatwe hakuna gari, pikipiki wala mtu anayepaswa kuitumia, Mwakyoma (RTO),  apeleke trafiki hapo,” ameongeza.
Kwa kukumbusha tu mpaka sasa wanafunzi zaidi ya 20,000 shule za msingi katika shule tisa  za Jiji la Dar essalaam  wamepata mafunzo ya usalama barabarani ambapo katika mashindano hayo Shule ya Msingi Kibamba iliibuka mshindi wa kwanza na kuzawadiwa Sh.milioni nne.

No comments:

Post a Comment