Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- DOMOMA
SERIKALI
kupitia Wizara ya Afya imetangaza kuanza kuwachukulia hatua Waajiri
wote ambao wanavunja Sheria kwa kugandamiza haki ya kupata likizo ya
uzazi kwa wanawake pindi anapojifungua.
Hayo
yamesemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya
unyonyeshaji Duniani yaliyofanyika katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini
Dodoma, yenye kauli mbiu ya “Wawezeshe wazazi kufanikisha
unyonyeshaji”.
“Haki
ya Mwanamke Kuzaa na kupata likizo ya uzazi ni haki yake ya asili,
haitakiwi kuwekewa vikwazo au changamoto yoyote, kwahiyo nitoe wito kwa
wanawake ambao wanafanya kazi, ni haki yako kupata likizo, asije mtu
anakwambia anaijaza kazi yako kwakuwa umetoka likizo ya kujifungua,
tuambie sisi, tutachukua hatua, na huyo Mwajiri tutamtangaza kuwa ni
adui wa Wanawake na Watoto wa Tanzania “.Amesema Waziri Ummy.
Waziri
Ummy aliendelea kusema kuwa Serikali ipo katika mpango wa kuanzisha
dawati la kutoa malalamiko litaloshughulikia kupigania na kutetea haki
za wanawake kupata likizo ya uzazi, jambo litalosaidia kudhibiti tabia
za baadhi ya Waajiri kukandamiza haki za wanawake baada ya kujifungua.
Kwa
upande mwingine, Waziri Ummy amesema kuwa takribani asilimia 97 ya
watoto wenye umri chini ya miaka miwili wananyonyeshwa maziwa ya mama,
hii inaonesha kuwa hali ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama imepungua
ikilinganishwa na takwimu ya mwaka 2015/2016 ambayo ilikuwa ni asilimia
98.
Aidha,
Waziri Ummy amesema kuwa idadi ya watoto wanaoanzishiwa kunyonyeshwa
maziwa ya mama kwa wakati sahihi (ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa)
ni asilimia 53 ikilinganishwa na asilimia 51 ya mwaka 2015/2016
Aliendelea
kusema kuwa, idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila
kupewa maji, vinywaji na vyakula vingine katika kipindi cha miezi sita
ya mwanzo baada ya kuzaliwa ni asilimia 58 ikilinganishwa na asilimia 59
ya mwaka 2015/2016.
Hata
hivyo, Waziri Ummy amesema kuwa Idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6
hadi 23 wanaolishwa chakula kinachokidhi vigezo vya ubora kilishe ni
35%, huku kiwango kikionekana kuongezeka ikilinganishwa na asilimia 10
kwa mwaka 2015/2016.
Mbali
na hayo, Waziri Ummy amesema kuwa, takwimu za utafiti wa hali ya lishe
nchini za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa asilimia 31 ya watoto walio chini
ya umri wa miaka mitano wamedumaa ikilinganishwa na asilimia 34 ya mwaka
2015/2016, huku sababu kubwa ya ikiwa ni ulishaji usio sahihi ambao
huchangiwa na majukumu mengi yanayomkabili mama na hivyo kukosa muda wa
kutosha wa kumtunza mtoto.
Naye
Mwakilishi kutoka UNICEF Bw. James Gitau amesema kuwa, unyonyeshaji ni
moja ya njia muhimu kuhakikisha Afya Bora kwa maisha ya mtoto, hivyo
kutoa wito kwa wanahabari kuhakikisha wanapeleka Elimu kwa wananchi
hususan wanawake kuhakikisha wanafahamu umuhimu wa kunyonyesha Watoto
mfululizo miezi sita ya mwanzo,
Pia,
Bw. James Gitau ametoa wito kwa Serikali kuongeza nguvu katika
uhamasishaji juu ya umuhimu na haki ya Watoto kunyonyeshwa, amesema
jambo hili litasaidia kuokoa watoto kupata magonjwa yanayotokana na
kukosa virutubisho kutoka kwa maziwa ya mama.
No comments:
Post a Comment