Pages

Thursday, August 29, 2019

SERIKALI INA NIA THABITI KUSHIRIKIANA NA WADAU WA TASNIA YA NAFAKA KUKOMESHA CHANGAMOTO-WAZIRI HASUNGA


Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akifungua mkutano na wafanyabiashara na wasindikaji wa mazao ya nafaka katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano JNICC Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Agosti 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya mgeni rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati akifungua mkutano na wafanyabiashara na wasindikaji wa mazao ya nafaka katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano JNICC Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Agosti 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumzia fursa zilizopo katika tasnia ya nafaka wakati akifungua mkutano na wafanyabiashara na wasindikaji wa mazao ya nafaka katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano JNICC Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Agosti 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa Mhe Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina nia njema kabisa ya kuhakikisha kuwa inashirikiana na wadau wote katika kuhakikisha kuwa tasnia ya nafaka inaendelea na kuondoa changamoto zinazojitokeza.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 29 Agosti 2019 wakati akifungua mkutano na wafanyabiashara na wasindikaji wa mazao ya nafaka katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano JNICC Jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa, Serikali peke yake, haiwezi kuziondoa changamoto hizo bila wafanyabiashara, wasindikaji na wasafirishaji kushirikiana na Serikali.

Katika mkutano huo waziri Hasunga amezitaja fursa zilizopo kwenye tasnia ya Nafaka kama ambazo ni pamoja na eneo linalofaa kwa kilimo ambalo linakadiriwa kuwa hekta milioni 44. Kati ya hizo, hekta milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Eneo hilo, linafaa kwa kilimo cha mazao yote ya biashara na chakula, yakiwemo mazao ya nafaka kama mahindi, mtama, mpunga, ngano na mengineyo.

Fursa nyingine alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, inajitahidi sana kufikisha umeme vijijini ambako ndiko nafaka zinapatikana. Hadi sasa asilimia 70 ya vijiji nchini, vimepatiwa umeme. Umeme huo unatakiwa utumike pia katika eneo la usindikaji. Hadi sasa, sehemu ndogo ya maghala kwenye usindikaji wa mpunga na mahindi kupitia mashine za kukoboa mpunga na mahindi.

Mhe Hasunga alisema kuwa Kuna baadhi ya maeneo, maghala mazuri yamejengwa  kwa usimamizi wa Serikali ili kuwa na uhifadhi mzuri wa nafaka. Mfano, maghala mengi yaliyojengwa wakati wa BRN bado hayajaweza kutumika ipasavyo.

Alisema Nchi yetu ina ikolojia tofauti tofauti, hali hii inasababisha baadhi ya maeneo kuwa na mvua za kutosha, na maeneo mengine kuwa na uhaba wa mvua. Maeneo yanayopata mvua za kutosha huzalisha chakula cha kutosha pamoja na ziada. Kwa maeneo ambayo yamezalisha ziada, wanayo fursa nzuri ya kupeleka ziada hiyo kwenye maeneo mengine ambayo hayazalishi vizuri.

“Vilevile, nchi yetu imezungukwa na nchi ambazo hazina fursa kubwa ya kilimo kama tuliyonayo. Miongoni mwa nchi hizo ni kama Uganda, Kenya, Congo, Sudan na nyinginezo. Hii ni fursa nyingine ya soko kwani tukizalisha vizuri, uhakika wa soko la nje, ni mkubwa pia” Alikaririwa Mhe Hasunga

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amezitaja mada zitakazojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na Fursa ya biashara ya mazao ya nafaka katika soko la Afrika na uwezo wa Tanzania kuzalisha nafaka na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu, Upotevu wa mazao ya nafaka baada ya mavuno, mkakati wa Taifa wa kudhibiti na matokeo ya utafiti wa hali ya maghala yalivyo hapa nchini, Uongezaji thamani katika mazao na kuboresha mazingira ya biashara ya nafaka na Mfumo wa masoko na uzoefu.

Alisema kuwa mada hizo zitatoa nafasi pia ya kuelewa vizuri tasnia ya nafaka ili kuwa na maazimio ambayo yatajibu changamoto mbalimbali hususani ya upatikanaji wa taarifa na utumiaji vizuri wa fursa zilizopo katika tasnia hiyo.

“Nitoe rai kwa washiriki wote, tusikilize kwa makini, tuwe wawazi, na kwa uhuru tujadili mada hizo kwa mapana na marefu, ili baada ya siku mbili hizi, tutoke na maazimio yatakayojibu changamoto za tasnia hii ya Nafaka” Alisisitiza Mhe Hasunga

MWISHO

No comments:

Post a Comment