Pages

Friday, August 30, 2019

JKCI YAWEKA HISTORIA: KWA MARA WAMWEKEA MGONJWA MWENYE UMRI WA MIAKA 101 KIFAA MAALUM CHA KUREKEBISHA MAPIGO YA MOYO (PACEMAKER) ILI YAWE SAWA.


Madaktari, wauguzi na mafundi sanifu wa moyo wa mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa chumba cha Cathlab wakiwa na nyuso za furaha mara baada  ya kumaliza kumwekea mgonjwa  kifaa maalum cha kurekebisha  mapigo ya moyo ili yawe sawa (kwa jina la kitaalamu Pacemaker) ambacho kimewekwa kwa mgonjwa mwenye umri wa miaka 101 kifaa hicho huwekewa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimi 30 kwa dakika.


Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye na Khuzeima Khanbai wakiangalia kifaa maalum cha kurekebisha mapigo ya moyo ili yawe sawa (kwa jina la kitaalamu Pacemaker) ambacho kimewekwa kwa mgonjwa mwenye umri wa miaka 101 kifaa hicho huwekewa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimi 30 kwa dakika. Tangu kuanza kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 hii ni mara ya kwanza kwa mgonjwa mwenye umri huo kuwekewa kifaa hicho.(PICHA NA JKCI)
 Na Ales Mbilinyi -JKCI
Kwa mara ya kwanza madaktari bingwa  wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamwekea mgonjwa mwenye umri wa miaka 101 kifaa maalum cha kurekebisha  mapigo ya moyo ili yawe sawa (kwa jina la kitaalamu Pacemaker).
Kifaa  hicho kisaidizi cha moyo huwekewa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimi 30 kwa dakika.
Akizungumza baada ya kumfanyia upasuaji mdogo na kumwekea mgonjwa kifaa hicho  Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Yona Gandye alisema mara nyingi  wanawawekea kifaa hicho  wagonjwa wenye umri wa miaka 80 kushuka chini lakini leo hii wamevunja rekodi na  na kuweka kwa mgonjwa wa umri wa  miaka 101.
“Kabla ya kufanya upasuaji tulimfanyia mgonjwa uchunguzi wa kina na kugundua  mfumo wake wa umeme wa moyo unahitilafu na mapigo ya moyo yapo chini ya asilimia 20 hivyo tumemuwekea kifaa ambacho kitausaidia moyo kuongeza mapigo yake na mara baada ya kumwekea kifaa hiki  mapigo yake ya moyo yako vizuri kati ya asilimia 60 na 100 kwa dakika”, alisema Dkt. Gandye.
Akizungumza kwa furaha mara baada ya baba yake kuwekewa kifaa hicho Saimoni Maina alisema  matatizo ya baba yake yameanza mwaka mmoja uliopita na kutibiwa katika hospitali mbalilmbali Mkoani Manyara na Arusha ambapo waligundua kuwa mapigo yake ya moyo yapo chini  hivyo kumpa rufaa kwa ajili ya kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Baba alikuwa akianguka na kupoteza fahamu mara kwa mara ndipo tukaamua kumpeleka hospitalini kwa ajili ya matibabu ili kufahamu  anasumbuliwa na tatizo gani, tunashukuru sana uwepo wa Taasisi hii kwani baba yetu ameweza kufanyiwa upasuaji na hali yake inaendelea vizuri kama mnavyomuona”, alisema Maina.
Kwa upande wake Mzee Benedict Maina alisema  kabla ya kufanyiwa kwa upasuaji huo alikuwa akipata maumivu makali sehemu za moyo, kuanguka, kupoteza fahamu na kushindwa kutembea lakini baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali yake imebadilika na maumivu kupungua ukilinganisha na ilivyokuwa awali na anaamini siku chache zijazo atarudi katika hali yake ya kawaida.

No comments:

Post a Comment