Pages

Wednesday, May 29, 2019

SERIKALI YATOA UFAFANUZI BEI ZA TAULO ZA KIKE


Na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa nguvu ya soko pamoja na gharama nyingine zimechangia kutoshuka kwa bei ya taulo za kike licha ya Serikali kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika taulo hizo.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Sophia Mwakagenda, alietaka kujua sababu za taulo hizo kupungua bei wakati Serikali iliondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo hizo katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, pamoja na Serikali  kuchukua hatua ya kuondoa kodi za taulo hizo, imebainika kuwa hakuna mabadiliko ya bei katika soko jambo linalodhihirisha kuwa bei inaamuliwa na nguvu ya soko pamoja na gharama nyingine za uzalishaji na uendeshaji.
"Hatua ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taulo za kike (pads) ililenga kupunguza sehemu ya gharama za uzalishaji wa bidhaa na kwamba athari chanya ilitotegemewa ilikuwa ni kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo lakini hadi sasa hakuna mabadiliko ya bei katika soko" alisema Dkt. Kijaji
Alisema kuwa hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama za malighafi, mishahara, uwekezaji, mifumo ya uzalishaji, teknolojia, ushindani katika soko, umeme, maji safi na maji taka, usambazaji na ubora wa bidhaa.
"Hivyo basi, kutoshuka kwa kwa bei ya taulo za kike kunabainisha kuwa kodi inachangua sehemu ndogo sana katika kupanga bei ya bidhaa, kama ambavyo Serikali imekuwa ikisisitiza na kutoa ufafanuzi mbele ya Bunge lako Tukufu”, alifafanua Dkt. Kijaji.
Alisema Serikali ina mpango wa kutoa taulo za kike bure  ili kuondoa changamoto ya bei ya taulo hizo inayolalamikiwa kutoshuka na kuwataka wabunge kutolichukulia suala hilo la upatikanaji wa bidhaa hizo kisiasa kwani hata baadhi ya nchi zilizoondoa kodi kama hizo ikiwemo Botswana na Kenya, zoezi hili halikusaidia kushusha bei za taulo hizo.
Dkt. Kijaji alisema kuwa, kwa sasa mfumo wa uchumi ni wa soko huria na bei ya bidhaa huamuliwa na nguvu ya soko, yaani ugavi na mahitaji ya soko, hivyo fursa iliyopo ni kuhamasisha uwekezaji mkubwa kwa kutumia teknolojia yenye gharama nafuu katika kutengeneza taulo hizo, jambo linalotakiwa kwenda sambamba na  kuchochea ushindani wa bei katika soko na sio Serikali kuondoa kodi na kupanga bei ya bidhaa.
Serikali ilichukua hatua ya kuondoa kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye taulo za Kike ikiwa na lengo la kupunguza sehemu ya gharama za uzalishaji wa bidhaa na hivyo kushuka kwa bei, lengo ambalo halijafikiwa.

No comments:

Post a Comment