Na Farida Ramadhani na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali imeleeza kuwa
imeshawalipa Wazabuni 2048 kiasi cha Shilingi 199 tangu kutolewa kwa
tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli tarehe 3 Januari, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam la kutaka
Wazabuni wote wanaoidai Serikali
walipwe.
Hayo yameelezwa Bungeni jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji,
alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa
Iringa (CCM), Mhe. Ritta Kabati, aliyetaka kujua baada ya tamko la Mhe.
Rais kuhusu Wazabuni wote wanaoidai Serikali walipwe ni Wazabuni wangapi
wameshalipwa.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji
alieleza kuwa kati ya Wazabuni 2048 waliolipwa na Serikali, Wazabuni
1,277 walihudumia Sekretarieti za Mikoa na 771 walihudumia Wizara,
Taasisi na Wakala za Serikali.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa
Shilingi 3,729,605,175 zimetumika kulipa Wazabuni waliotoa huduma kwa
Sektretarieti za Mikoa na Shilingi 195,334,409,791.64 zimetumika kulipa
Wazabuni wa Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali.
“Ikumbukwe kuwa madeni yote haya yalilipwa baada ya uhakiki kufanyika”, alisisitiza Dkt. Kijaji.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea
kulipa madai mbalibmali ya wazabuni kulingana na upatikanaji wa fedha,
sambamba na uhakika wa madai husika.
Dkt. Kijaji amesema kuwa ili
kukamilisha zoezi la uhakiki kwa wakati, wazabuni wote wanatakiwa kutoa
ushirkiano, hususan kuwasilisha taarifa na vielelezo sahihi vya madai
yao pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.
Katika swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Kabati alitaka kujua vigezo vilivyotumika kuwalipa wazabuni hao.
Akijibu swali hilo la nyongeza
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa
vipo vigezo vingi ambavyo Serikali imevitumia kulipa madeni hayo moja
ikiwa umri wa deni, madeni ambayo yamekaa kwa muda mrefu na ambayo
tayari yamehakikiwa ndiyo yanapewa kipaumbele katika malipo.
Aliongeza kuwa kigezo cha pili ni
riba Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa madeni ambayo riba yake
inakuwa kulingana na muda, ili Serikali isiendelee kuumia wala mwananchi
asiendelee kuumia.
No comments:
Post a Comment