Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imesema haitasita kuwachukulia hatua watu wanaowanyanyasa watoto kwa kukiuka Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009.
Hayo yamesemwa leo, Bungeni
Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Josephat Kandege alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Mgebi Jadi Kadika juu ya mikakati ya
Serikali ya kuondoa tatizo la kuwakosesha watoto haki za msingi na
malezi bora kwa kuwatumia katika kutoa huduma ya kubeba mizigo na kupewa
ujira mdogo.
“Huduma za ulinzi wa mtoto
zinatekelezwa kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009. Katika
kusimamia utekelezaji wa Sheria hiyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa
zinatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya
Wanawake na Watoto ulioanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa Fedha 2017/18
hadi 2021/22,” amesema Kandege.
Ameendelea kusema, tathmini
imebaini kuwa watoto wengi wanaojihusisha na kazi za kubeba mizigo
masokoni ni matokeo ya umaskini uliokithiri kwa baadhi ya Kaya,
kuondokewa na wazazi wao kwa maambukizi ya UKIMWI, migogoro ya ndoa na
ukatili dhidi ya watoto.
Amesema, mkakati unaotekelezwa na
Serikali ni kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za msingi za mtoto kupata
elimu na malezi bora. Aidha, utoaji wa elimu msingi bila malipo umetoa
fursa kwa watoto wengi wenye umri wa kwenda shule kuandikishwa kuanza
elimu ya awali kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi.
Aidha ametoa wito kwa wazazi
kutimiza wajibu wao wa kuwalea, kuwatunza na kuwalinda watoto ambao ni
Taifa la kesho kwa kutowatumikisha katika kazi ambazo haziendani na umri
wao.
No comments:
Post a Comment