Pages

Monday, October 1, 2018

UTOAJI HATI MILIKI ZA ARDHI TANZANIA WAONGEZEKA KWA KASI- MABULA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akionesha Ripoti ya Utafiti kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania mara baada ya kuizindua, kushoto ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa.

NA MUNIR SHEMWETA, DODOMA 
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula amesema kasi ya utoaji hati za umiliki wa ardhi na makazi imeongezeka kwa kasi ambapo hadi kufikia septemba mwaka huu 2018 jumla ya hati 25,463 zimeandaliwa. Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa uwasilishwaji matokeo ya utafiti kuhusu haki na usalama na umiliki wa rasilimali ardhi na makazi jijini Dar es salaam leo Mabula alisema jumla ya hati 17,680 zilikuwa zimewasilishwa ofisi za kanda kwa ajili ya usajili na hati 9,739 zimeshakamilika. Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na Wizara yake katika kutoa hati lakini takwimu zinaonesha kuwa hati nyingine zimeandaliwa katika halmashauri lakini zilizowasilishwa kwenye ofisi za kanda husika ni chache  kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kuandalia hati. Kwa mujibu wa Mabula, kuna hati nyingi zinaonekana kuwasilishwa ofisi za kanda lakini hati zilizokamilika ni chache kutokana na hati nyingi zilizowasilishwa katika ofisi za kanda kuwa na upungufu mbalimbali na hivyo kusababisha hati hizo kutokamilika kwa wakati. Akigeukia suala la haki na usalama na umiliki wa rasilimali ardhi na makazi kwa wananchi waishio vijijini, Mabula alisema hadi kufikia Mei 2018 jumla ya vipande vya ardhi 96,257 vimepimwa katika vijiji 91 na hati za kimila 20,583 zimeandaliwa na vijiji 20 vimeandaliwa na mipango ya makazi ambapo jumla ya viwanja 18,224 vimepimwa kwa ajili ya kuandaliwa hati ya haki miliki ya kimila. Kwa mwaka 2018/2019 Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imejipanga kuandaa hati za kimila 120,000, mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji 30 na mpango wa kina kupima viwanja 20,000 kwa lengo kumuwezesha mwananchi wa kawaida kuwa na uhakika na usalama ya miliki yake na kuepusha migogoro.

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akimkabidhi Afisa Habari wa Idara ya Habari MAELEZO Frank Mvungi Ripoti ya Utafiti kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akimkabidhi Ripoti ya Utafiti kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati Ezekiel Kitilya mara baada ya kuizindua ripoti hiyo.

Baadhi ya washiriki waliohudhuria uzinduzi wa Ripoti ya Utafiti kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi.(PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE-WANMM).

No comments:

Post a Comment