Pages

Monday, July 23, 2018

PROFESA JANABI AWAONGOZA WAFANYAKAZI WA JKCI KATIKA SHEREHE YA KUMUAGA AFISA MUUGUZI MWANDAMIZI MSAAFU MAMA HADIJA MRADI BAADA YA KUSTAAFU IUTUMISHI WA UMMA

  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi (kushoto) akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake katika utumishi wa umma kwa kufanya kazi kwa miaka 41 Afisa Muuguzi Mwandamizi Mstaafu Mama  Hadija Mradi katika  hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika leo jijini Dar Es Salaam.Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi Robert Mallya

  Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akimlisha keki Afisa Muuguzi Mwandamizi Mstaafu Mama  Hadija Mradi wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika leo katika  ukumbi wa mikutano wa  Taasisi hiyo uliopo jijini Dar ES Salaam . Anayeshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi.

  Afisa Muuguzi Mwandamizi Mstaafu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mama  Hadija Mradi (kulia) akikata keki wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika leo katika ukumbi wa Mikutano wa  Taasisi hiyo ilizopo jijini Dar Es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uuguzi  Robert Mallya

  Afisa Muuguzi Mwandamizi Mstaafu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mama  Hadija Mradi (kulia) akifuatilia yaliyokua yakiendelea wakati wa hafla fupi ya kumuaga iliyofanyika leo katika Taasisi hiyo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Delila Kimambo.


Baadhi ya wafanyakazi  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokua yakiendelea wakati wa hafla fupi ya kumuaga Afisa Muuguzi Mwandamizi Mstaafu Hadija Mradi (hayupo pichani) iliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo uliopo jijini Dar Es Salaam.(PICHA NA JKCI)

NA MWANDISHI MAALUM

WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kufanya kazi zao za kutoa huduma kwa wagonjwa kwa uadilifu huku wakifuata sheria na kanuni za utumishi wa Umma.

Rai hiyo Imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati wa hafla fupi ya kumuaga Afisa Muuguzi Mwandamizi Mama Hadija Mradi aliyestaafu utumishi wa Umma hivi karibuni.

Prof. Janabi alisema  wananchi hasa wagonjwa wanategemea kupata huduma bora za matibabu ya moyo kutoka kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo hivyo basi wajitahidi kufanya kazi zao kwa kufuata maadili yaliyopo.

“Leo hii tunamuaga Mama Mradi ambaye amefanya kazi ya Uuguzi  kwa muda wa miaka 41, kama mama huyu asingefuata maadili ya kazi yake  siajabu angefukuzwa kazi mapema lakini kutokana na uadilifu wake amefikia hatua ya kustaafu salama hongera sana  Mama kwa kujitoa kwako kuwahudumia wagonjwa kwa miaka yote hiyo”, alisema Prof. Janabi.

Akizungumzia jinsi anavyomfahamu Mama Mradi  Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi  ya Uuguzi Robert Mallya alisema mfanyakazi huyo alikuwa mfanyakazi bora ambaye alijituma katika kazi zake bila ya kushinikizwa.

Mallya alisema , “Ukimpangia majukumu ya kazi Mama Mradi atayatekeleza bila ya kusimamiwa na kiongozi wake, kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi ndiyo maana amefanya kazi muda mrefu hadi kufikia hatua ya kustaafu utumishi wa umma  ni muhimu kwa wauguzi tuliobaki kazini tuige mfano wake”.

Kwa upande wake Mama Mradi alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji, Viongozi pamoja na  wafanyakazi wote wa Taasisi hiyo kwa ushirikiano wao waliouonyesha kwa kipindi chote walichokuwa wanafanya kazi pamoja na kuomba shirikiano huo uendelee.

Taasisi hiyo ilimzawadi Mama Mradi  zawadi zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni saba  ambazo ni mabati 100 na mifuko 100 ya smenti hii ikiwa ni shukrani ya kutambua mchango wake wa ufanyaji kazi alioutoa kwa utumishi wa Umma.

No comments:

Post a Comment