Pages

Monday, July 30, 2018

MAKAMU WA RAIS AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI MBEYA


01
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson akiteta jambo na Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki wakati wa mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sabasaba wilaya ya Chunya ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara ya Makamu wa Rais mkoani Mbeya. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)03 (1)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Naibu Waziri wa Kilimo Dkt. Mary Mwanjwelwa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha majumuisho ya ziara yake katika Ukumbi wa Mkapa mkoani Mbeya. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
02 (1)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa Chunya kwenye uwanja wa Sabasaba ikiwa ni siku ya kuhitimisha ziara yake mkoani Mbeya. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amehitimisha
ziara yake ya siku 6 mkoani Mbeya ambapo ameupongeza mkoa huo kwa kutunza mazingira.
“Naomba sana ule utaratibu wa Machifu kusimamia Mazingira uendelee”
alisema Makamu wa Rais.
Katika ziara hiyo ya siku 6 ya kukagua na kuhamasisha shughuli mbali mbali za kimaendeleo, Makamu wa Rais amesema Uchumi wa Viwanda unaunganishwa na miundombinu hivyo Mbeya imekidhi vigezo kwani pamoja na kuwa na barabara nzuri pia ina meli tatu ambazo kati ya hizo mbili ni za mizigo na moja ya abiria na mizigo.
Mapema leo Makamu wa Rais alifanya ziara katika wilaya ya Chunya na kujionea Viwanda vinavyojishughulisha na uchenjuaji madini ya dhahabu ambapo alitoa Maagizo kwa Uongozi wa Mkoa, Halmashauri pamoja na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kuhakikisha viwanda vya uchenjuaji madini  vina vibali vyote muhimu kabla ya kupatiwa leseni.
Wakati huo huo Waziri wa Madini Mhe. Angellah Kairuki amesema Serikali imeweka zuio la usafirishaji wa Kaboni ambazo zinabeba madini ya dhahabu kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine kwa lengo kubwa la kuweka ulinzi na usalama na kusema kitakachotoka kutoka  mmoja kwenda mwingine ni dhahabu ambayo imeshachenjuliwa.
Waziri Kairuki amesema kuwa Wote wenye leseni za Uchimbaji na hawajaendeleza maeneo yao watafutiwa leseni hizo na kupatiwa watu wengine.
Mwisho, Makamu wa Rais alihitimisha ziara yake kwa kufanya kikao cha majumuisho na Uongozi wa Mkoa wa Mbeya ambapo aliupongeza kwa kuwa na vituo vya afya 316, chakula cha kutosha lakini pia alisisitiza Uongozi huo wa mkoa kufanya jitihada za kutoa elimu ya lishe kwa jamii kwani kiwango cha udumavu kwa watoto ni kikubwa.

No comments:

Post a Comment