Muonekano wa
baadhi ya Taa za barabarani zinazowekwa katika barabara mpya ya
Emmaus-African Dream jijini Dodoma, Taa hizo zinawekwa kufuatia agizo la
Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli, aliyetaka fedha zilizokuwa
zimetengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa mwaka huu, kiasi
cha Shilingi milioni 308, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara za
jiji hilo.
AGIZO LA RAIS MAGUFULI KUHUSU FEDHA ZA MASHUJAA KUTUMIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BARABARA LATEKELEZWA
Mnamo mwezi Juni, mwaka 2018, Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alitoa taarifa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli,
ameagiza) fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya siku ya
Mashujaa
kiasi cha Shilingi milioni 308, zitumike kuboresha miundombinu
ya barabara jijini Dodoma.
Kufuatia agizo hilo, Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini (TARURA), walipata kiasi cha Shilingi milioni 288 kwa
ajili kuweka taa 57 kwenye barabara ya Emmaus-African Dream na taa 42
kwenye barabara ya Kisasa. kiasi cha shilingi milioni 20 walipewa Wakala
wa Barabara Dodoma (TANROADS), kwa ajili ya kuhamisha taa ya kuongoza
magari kutoka njia panda ya Area D na kuwekwa kwenye makutano ya
barabara ya Emmaus.
Tayari TARURA wameanza kutekeleza agizo
hilo kwa kuweka taa kwenye barabara ya Kisasa na Emmaus-African Dream.
Kwa upande wa TANROADS-Dodoma, zoezi la kuhamisha taa ya kuongoza magari
limetekelezwa, ambapo wakandarasi watakabidhi kazi hizo rasmi mwezi
Agosti mwaka huu.
Akiongea wakati wa ukaguzi wa kazi hiyo
katika barabara ya Emmaus-African Dream Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora alifafanua kuwa, kuwekwa
kwa taa kwenye barabara hizo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais
aliyetaka miundombinu ya barabara jijini Dodoma kuboreshwa, hali
inayoongeza usalama kwa watumiaji wa barabara hizo pamoja na kupandisha
hadhi ya jiji na makazi ya maeneo husika.
“Taa hizi ni za kisasa na zitasaidia
uhifadhi wa mazingira kwakuwa zinatumia mwanga wa jua, Serikali
inajitahidi kuboresha miundo mbinu ikiwemo barabara hii, hivyo wananchi
ambao barabara inapita katika makazi yao hawanabudi kuilinda miundombinu
ya taa hizi. Fedha za walipakodi zimetumika hapa itasikitisha kuona
miundo mbinu ya taa hizi kukuta imeharibiwa” amesisitiza Kamuzora.
Awali, akielezea shughuli zinazoendelea
katika barabara ya Emmaus-African Dream, Meneja wa Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe
alibainisha kuwa taa hizo ni za kisasa na zina uwezo wa kuhifadhi umeme
hivyo zitasaidia kupunguza ghrama za uendeshaji na uhakika katika
matumizi ya barabara hizo.
Kampuni ya Mionzi Jua Ltd ndiyo inayofanya
kazi ya kuweka taa katika barabara za Kisasa na Emmaus-African Dream,
ambapo jumla ya kiasi cha Shilingi milioni 287.1 zitatumika kukamilisha
kazi hiyo.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILINO SERIKALINI
OFISI YA WAZIRI MKUU
No comments:
Post a Comment