Pages

Wednesday, February 28, 2018

RC NDIKILO: MKOA WA PWANI UNATARAJIA KUZINDUA VIWANDA TISA WAKATI WOWOTE KUANZIA SASA


IMG-20180228-WA0014
Mkurugenzi wa kampuni ya Global Land Solution ,Zainuddin Adamjee, (mwenye kibagharashia )akimtembeza mkuu wa mkoa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, katika fukwe ya bahari kwenye eneo la uwekezaji  wa masuala ya utalii Palacha (dream city)kijiji cha Mpafu-Mkuranga,ambako kunatarajia kuwa mji wa kisasa ukitoa huduma za kitalii kupitia fukwe za bahari  .(picha na Mwamvua Mwinyi)
IMG-20180228-WA0016
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) akionyeshwa bidhaa zinazozalishwa na kampuni ya Lodhia Group of Companies ,Mkuranga ,anaemuonyesha bidhaa hizo ni mkurugenzi wa kampuni hiyo ,Arun Lodhia.(picha na Mwamvua Mwinyi)
IMG-20180228-WA0040
Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) akitembelea kampuni ya Lodhia Group of Companies ,Mkuranga inayojihusisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za chuma na plastiki, wa (kulia) ni mkurugenzi wa kampuni hiyo Arun Lodhia.(picha na Mwamvua Mwinyi)
……………………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga
MKOA wa Pwani, unatarajia kuzindua viwanda Tisa ambavyo vimeshakamilika, ikiwa ni muendelezo wa kasi ya kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji katika mkoa huo.
Aidha imewaelekeza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mkoa huo, kuhamasisha wawekezaji
watakaoweza kwenda kuwekeza kwenye eneo la sekta ya utalii hasa kwenye fukwe zilizopo mkoani humo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, aliyasema hayo wakati alipotembelea baadhi ya viwanda pamoja na eneo la uwekezaji  wa masuala ya utalii eneo la Palacha,kijiji cha Mpafu-Mkuranga.
Alisema wanatarajia kuzindua viwanda hivyo,wakati wowote kuanzia sasa ,ikiwa ni sanjali na kiwanda cha Sayona-Lugoba, Twyford kilichopo Pingo,KEDS na viwanda vitatu vinavyondeshwa na kampuni ya Lodhia Group of Companies inayojihusisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za chuma na plastiki iliyopo Mkuranga.
Mhandisi Ndikilo, alieleza wamejipanga kuinua sekta ya uwekezaji na viwanda hivyo kukamilika kwa viwanda hivyo inawapa imani ya kutimiza adhma ya mkoa huo kuwa ukanda wa viwanda.
Alielezea wanatekeleza sera ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ,kwa vitendo ambapo kwasasa kuna viwanda zaidi ya 300 ambavyo viko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na vingine vimeshaanza uzalishaji.
“Tunashukuru kuona wawekezaji wameboresha yale yote waliyotakiwa kuyafuata na kukamilisha ujenzi kwa asilimia 90, kwani viwanda vyote vikianza uzalishaji vitasaidia kuliingizia pato Taifa na kuwa mkombozi katika eneo la ajira.”alisema mhandisi Ndikilo.
Pamoja na hayo, mkuu huyo wa mkoa , aliziasa taasisi wezeshi ikiwemo Dawasco, Tanesco, TARURA na halmashauri mbalimbali kushirikiana na wawekezaji kwenye maeneo yao na kuondoa urasimu .
“Matarajio yetu ni  kupanua wigo katika ajira ,kuondokana na umaskini kwani wananchi watapata kazi na wengine wataanzisha huduma ndogondogo kwa wafanyakazi kwenye viwanda hivyo,” alisema mhandisi Ndikilo.
Hata hivyo, mhandisi Ndikilo alisema uendelezaji wa maeneo ya utalii utavutia watalii wengi na kuingiza mabilioni ya fedha kutokana na kodi na wageni kutoka nje.
Akielezea eneo la Palacha, alieleza itasaidia kuanzishwa kwa huduma za kijamii kama vile uwanja wa ndege, mahoteli, masoko na shule ambapo watalii watakuwa wakifanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuogelea, uzamiaji na michezo mingine ya baharini.
Nae mkurugenzi wa kampuni ya Global Land Solution ,Zainuddin Adamjee,aliushauri mkoa wa  Pwani, kuunda kamati ndogo ya mamlaka ya kuratibu uwekezaji kwenye fukwe ili kurahisha kukuza Utalii wa fukwe nchini.
Alisema kuwa ,wameanzisha mradi wa Palacha Dream City ambao ni mji utakaokuwa wa kisasa ukitoa huduma za kitalii kupitia fukwe za bahari zenye urefu wa kilometa nne,huko kijiji cha Mpafu ,Mkuranga.
“Mradi huu ulibuniwa miaka minane iliyopita ili kuchangia katika uendelezaji wa sehemu za utalii katika ukanda wa kusini na kuinua uchumi wa mkoa huo.”
“Mradi utakapokamilika utakuwa kiuongo muhimu cha sehemu zote za utalii katika ukanda wa kusini kwani utakuwa na kiwanja cha ndege ambacho mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania imeshakipitisha”alisema Adamjee.
Adamjee alielezea ,mradi huo unahitaji umeme mwingi hivyo wanaiomba REA awamu ya tatu iwafikie na huduma ya maji ya uhakika katika kijiji cha Mpafu eneo la Palacha na maji ya uhakika.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa kampuni ya Lodhia Group of Companies ,inayojihusisha na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za chuma na plastiki ,Arun Lodhia, alieleza wameshatoa ajira ya watu 1,500 wakiwemo vijana.
Alisema, mbali ya ajira hizo pia wameweza kujenga barabara ambayo inatumiwa na wananchi wanaozunguka kiwanda hicho.
“Tunaomba tupatiwe umeme wa uhakika na kuunganishwa kwenye gridi ya taifa ili kuwa na umeme wa uhakika ambao utasaidia kwenye shughuli zetu,” alisema Lodhia.

No comments:

Post a Comment