Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Bw. Doto James (kulia), akizungumza na Balozi wa Japan
nchini, Mhe. Masaharu Yoshida na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara
Nchini-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale. baada ya tukio la kusaini
mkataba wa msaada wa Shilingi bilioni 77.3 zilizotolewa na Serikali ya
Japan kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya njia ya nne ya New Bagamoyo
Road kutoka Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James (kulia), na Balozi wa Japan nchini, Mhe.
Masaharu Yoshida, baada ya tukio la kusaini mkataba wa msaada wa
Shilingi bilioni 77.3 zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya
Mradi wa upanuzi wa Barabara ya njia ya nne ya New Bagamoyo Road kutoka
Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James, akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari
wakati wa tukio la kusaini mkataba wa msaada wa Shilingi bilioni 77.3
zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili yaMradi wa upanuzi wa
Barabara ya njia nne ya New Bagamoyo Road kutoka Morocco hadi Mwenge,
Jijini Dar es Salaam. Anayeangalia makaratasi nyuma ni Balozi wa Japan
nchini, Mhe. Masaharu Yoshida.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
…………………………………………………………………………………….
Serikali ya Japan kupitia Shirika
lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania ruzuku ya Yen bilioni 3.78
sawa na Shilingi bilioni 77.3 kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya New
Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo
yametiwa saini Februari 28, 2018, Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali, na
Balozi wa
Japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida na kushuhudiwa na
Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), Toshio
Nagase na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini-Tanroads, Mhandisi
Patrick Mfugale.
Mradi wa barabara hiyo yenye
urefu wa kilometa 4.3 utahusisha barabara yenye njia nne pamoja na
kuanza kwa awamu ya nne ya ujenzi wa barabara itakayotumiwa na mabasi ya
mwendo wa haraka (BRT phase IV).
Akizungumza baada ya kutiwa saini
wa makubaliano hayo, Bw. Doto James amesema kuwa barabara hiyo
ikikamilika itasaidia kutatua changamoto ya msongamano wa magari
yanayotoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Upanuzi wa Barabara ya New
Bagamoyo si tu kwamba utaondoa msongamano wa magari, bali pia ni kiungo
muhimu cha Bandari ya Bagamoyo ambayo itarahisisha usafirishaji wa
abiria, mizigo na huduma kutoka Jiji la Dar es Salaam, mkoa wa Pwani na
mikoa mingine nchini” Alisema Bw. Doto James.
Ameishukuru Japan kwa msaada
mwingine uliotolewa mwezi Septemba, 2017 wa kiasi cha fedha za Japan
(Yen) milioni 69 sawa na shilingi bilioni 1.4 ambazo zimetumika kwa
ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa barabara hiyo itakayoanza kujengwa
Bw. James ameeleza kuwa awamu ya
kwanza, Japan ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 99.5. kujenga barabara
ya njia nne katika kipande cha kilometa 12.9 kutoka makutano ya barabara
ya Tegeta na makutano ya barabara ya Mwenge pamoja na kukamilisha
ujenzi wa madaraja ya Mlalakuwa, Lugalo na Tegeta.
“Si mara ya kwanza kwa Japan
kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu katika makutano ya Tazara,
ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Babati
mkoani Manyara (km 188.15), Tunduru-Mangaka – Mtambaswala (km 202) na
barabara ya Iringa hadi Dodoma (259.9)” alisisitiza Bw. Doto James.
Balozi wa Japan, Mhe. Masaharu
Yoshida ameeleza kuwa kutolewa kwa msada huo ili kuwezesha awamu ya pili
ya ujenzi wa barabara kuanza kutayafanya matokeo ya kujenga barabara
hiyo kuanza kuonekana dhahiri ikiwemo kupunguza msongamano wa magari kwa
kiasi kikubwa ili kuokoa fedha nyingi zinazotokana na changamoto za
msongamano huo.
“Ili kukamilisha usanifu wa kina
wa mradi huu, nilisaini mkataba wa usanifu wa kina wa mradi wa upanuzi
wa barabara ya new Bagamoyo (Awamu ya Pili) miezi mitano iliyopita,
hatimaye sasa ninasaini mkataba wa sehemu kuu ambayo ni ujenzi wenyewe”
Alisema Balozi Yoshida.
Balozi huyo wa Japan hapa nchini,
amesema mradi huo utasaidia kuboresha ukuaji wa uchumi na kupunguza
umasikini nchini na kwamba msaada huo ni mwendelezo wa kudumisha
uhusiano mzuri uliopo kati ya Japan na Tanzania.
Utafiti uliofanyika hivi karibuni
unaonesha kuwa Barabara ya Bagamoyo ndiyo yenye msongamano mkubwa wa
magari yanayokadiriwa 52,000 yanayopita kila siku katika barabara hiyo.
No comments:
Post a Comment