Pages

Thursday, November 2, 2017

Tanzania Health Summit Kujadili Changamoto Sekta ya Afya

Pix 01
Rais wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Dkt. Omary Chillo (katikati) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la nne la kitaifa la afya, kushoto ni Katibu wa chama hicho Dkt. Rebeca John na kulia ni Afisa Tawala wa chama hicho Bw. Joseph Mhagama.
Pix 02
Afisa Tawala wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Bw. Joseph Mhagama akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la nne la kitaifa la afya, katikati ni Rais wa chama hicho Dkt. Omary Chillo na kushoto ni Katibu wa chama hicho Dkt. Rebeca John.
Pix 03
Katibu wa Chama cha watoa huduma za afya binafsi Dkt. Rebeca John (kushoto) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kongamano la nne la kitaifa la afya, katikati ni Rais wa chama hicho Dkt. Omary Chillo na kulia ni Afisa Tawala wa chama hicho Bw. Joseph Mhagama.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
………………

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Taasisi ya Tanzania Health Summit imeandaa Kongamano la Afya kwa ajili ya kujadili changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hiyo na...
k utoa mapendekezo ya utatuzi wa changamoto hizo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Rais wa Taasisi hiyo, Dkt. Omari Chillo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya kongamano hilo.
Dkt. Chillo amesema kuwa maandalizi ya Kongamano hilo yanaendelea vizuri hivyo mnamo  Novemba 14-15 mwaka huu wanategemea kufanya Kongamano katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JNICC).
“Lengo kuu hasa la mkutano huu ni kuchangia juhudi za Serikali katika kuboresha afya kwa kujadiliana changamoto zinazokabili sekta ya afya na kuishia na mapendekezo yanayoonyesha suluhisho la majadiliano hayo ambayo huandikwa kwenye kitabu na kusambazwa kwa taasisi husika za afya na kufuatilia utekelezaji wa yaliyoandikwa kwa taasisisi hizo,” alisema Dkt. Chillo.
Ameongeza kuwa, Kongamano la mwaka huu litahusisha vipengele mbalimbali vikiwemo vikao vitakavyogusa mada kama maendeleo ya huduma za afya, hotuba kutoka kwa wataalamu wazoefu wa afya, kuwasilisha matokeo ya uchunguzi na majadiliano katika vikundi.
Vile vile kutakuwa na maonesho ya huduma na bidhaa kutoka kwa wasambazaji wa huduma za afya na mashirika ya umma na binafsi.
Dkt. Chillo amefafanua kuwa katika siku mbili hizo za mkutano wanatarajia kupata wadau wa afya takribani 500 kutoka ndani na nje ya nchi wakiwemo manesi, madaktari, wafamasia, watunga sera, watafiti wa magonjwa ya afya, wachumi, wasambazaji wa vifaa tiba na dawa, wawekezaji katika sekta ya afya pamoja na wadau wote wa maendeleo ya afya.
Kwa upande wake Katibu wa Taasisi hiyo, Dkt. Rebeka John amesema kuwa Kongamano hilo linatoa fursa chache za udhamini na maonyesho hivyo wanaohitaji kushiriki wanatakiwa kujaza fomu ya maombi inayoweza kupakuliwa kupitia tovuti ya www.ths.or.tz., kutuma barua pepe kwenda info@ths.or.tz, au kwa namba ya simu +2555 684 244 377.
“Ningependa kutoa wito kwa wadau wa afya kutoka serikalini na mashirika binafsi, mahospitali, asasi zisizo za kiserikali, taasisi za kitaaluma, watengenezaji wa bidhaa za afya, wasambazaji, wawekezaji na washirika wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika mkutano wa mwaka huu,” alisema Dkt Rebeka.
Pia, amewashukuru wadhamini wao wakuu wa kongamano hilo wakiwemo Tindwa Medical And Health Services, Chuo cha Mtakatifu Joseph, Gazeti la The Guardian, Chuo cha Afya Muhimbili, Blogu ya Issa Michuzi na Medico Press.
Huu ni Mkutano wa nne kufanyika nchini ukiwa na kauli mbiu inayosema “Ni jinsi gani tunaweza kufikia malengo ya kuimarisha upatikanaji wa afya bora kwa kuunganisha tafiti za kisayansi, ubunifu na sera za afya”.

No comments:

Post a Comment