TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imesema kuwa katika uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika Novemba 26,
2017 katika kata 43 utagharimu kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC
Kailima Ramadhani, alisema msingi wa bajeti ya uchaguzi unategemea idadi
ya vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura walioandikishwa
katika kata husika. Amesema idadi ya Wapiga Kura ndio inatoa bajeti ya
mahitaji ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama karatasi za kura pamoja
na idadi ya vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua wanne.
Kailima alitoa ....
mfano kwamba Kata yenye vituo 41 ina bajeti kubwa kuliko
Kata yenye vituo vikubwa.
Alisema katika kituo cha
kupigia kura kina watendaji wanne ambao ni Msimamizi na Msimamizi
Msaidizi, karani mwongozaji na mlinzi wa kituo “lakini pia kuna watu wa
ziada kama Wasimamizi Wasaidizi wako ngazi ya kata na jimbo ambao
wanahusika kusimamia zoezi la Uchaguzi katika maeneo husika.
Alifafanua kuwa gharama
nyingine za uchaguzi ziko kwenye usafirishaji wa vifaa kutoka Tume
kwenda kwenye Halmashauri husika na kutoka Halmashauri kwenda kwenye
kata ambako uchaguzi unafanyika. Gharama hizo pia zanahusu utoaji wa
Elimu ya Mpiga Kura kupitia machapisho mbalimbali ya Elimu ya Mpiga
Kura, Maelekezo mbalimbali kwa Watendaji wa Uchaguzi n.k.
Elimu hiyo pia hutolewa
kupitia Vyombo vya Habari pamoja na machapisho mbalimbali yatakayotumika
kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura.
“Kwenye uchaguzi huu mdogo
bajeti yetu ni Sh bilioni 2.5. Sio kwamba kila kata itatumia gharama
sawa za fedha hizi, bali kuna kata itatumia milioni 20 kutokana na idadi
ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi
kwenye uchaguzi huu itatumia Sh milioni 150,” alisema Kailima.
Tume pia imeviasa Vyama vya
Siasa vinavyohusika kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kutekeleza maadili
ya uchaguzi ya 2015 waliyokubaliana kuyafuata na ameonya kuwa chama au
mgombea atakayekika maadili hayo atachukuliwa hatua kama ilivyoanishwa
kwenye maadili hayo ya uchaguzi.
Mkurugenzi huyo amesema Vyama
vya Siasa vinatakiwa kuhakikisha vinawaelemisha wafuasi,Wapenzi na
Wananchama wao juu ya kutekeleza maadili hayo katika kipindi chote cha
kampeni. Alisisitiza kuwa iwapo wafuasi wa vyama vya siasa watakikua
maadili hayo, chama husika pamoja na mgombea wake watachukuliwa hatua za
kinidhamu.
Alitaja baadhi ya vitendo vya
kuvunja maadili ya uchaguzi ni kuchana mabango ya wagombea, kutoa lugha
chafu wakati wa mikutano ya kampeni pamoja na kupitisha muda wa kufanya
mikutano ya kampeni.
Alisisitiza kamati za maadili
za kata na jimbo kuchukua hatua kali kwa chama au mgombea ambaye
atakikuka maadili hayo. Alisema kamati hizo zinatakiwa kuchukua hatua
ndani ya saa 48 mara chama au mgombea anapovunja maadili.
Alizitaja baadhi ya adhabu
zitazowakabili wagombea au chama ambacho kitavunja maadili ya uchaguzi
kuwa ni kuomba radhi wananchi hadharani, kutotumia vyombo vya habari kwa
muda fulani wakati wa kampeni, onyo la maandishi, kusimamishwa kufanya
kampeni, mgombea kutangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa yeye ni
bingwa wa kukikuka maadili ya uchaguzi au kutozwa faini Sh 100,000,
“Ni hatari kwa chama cha siasa
kukiuka maadili, hivyo navisihi vyama vya siasa kuheshimu na kuzingatia
maadili hayo,” alisema Kailima. “Pia niwaombe vyama vya siasa
vizingatie maadili kwenye mikutano yao, viende kuwaambia wananchi
watawafanyia nini katika kata zao na sio vinginevyo,”alisema Kailima.
Kailima pia alisema chama cha
siasa ambacho kinataka kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya
kampeni, lazima kimfahamishe msimamizi wa uchaguzi wa kata na ombi hilo
lazima lijadiliwe na vyama vyote vinavyoshiriki kwenye uchaguzi.
Kuhusu vitambulisho mbadala
vitakavyotumika wakati kupigia kura kwa wale ambao wamepoteza kadi ya
mpiga kura ambavyo ni vitambulisho vya taifa, leseni ya udereva na hati
ya kusafirisha; Kailima amesema vitambulisho hivyo vitatumika tu kwa
watu ambao wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika
kituo husika mwaka 2015, lakini pia bado wana sifa za kupiga kura.
“Masharti ya kutumia
vitambulisho hivyo mbadala ni ya kisheria chini ya Sheria ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa kifungu 62 (a). Masharti yake ni lazima mtu awe bado
na sifa ya kuwa mpiga kura, mfano mtu akishahukumiwa na kufungwa kwa
kosa la kukwepa kodi, au amechukua uraia wa nchi nyingine au amewekwa
kizuizini kwa mujibu wa sheria na katiba, mtu wa namna hiyo haruhusiwi
kupiga kura hata kama ana kadi ya mpiga kura au vitambulisho hivyo
vingine vitatu,”amefafanua Kailima.
Akizungumza Mikutano ya
Kampeni Kailima alitoa wito kwa vyama vya siasa kutambua kwamba Tume ya
Taifa ya uchaguzi imeruhusu mikutano ya kampeni na sio mikutano ya vyama
vya siasa. Amesema mtu anayeruhusiwa kwenye mikutano ya kampeni ni
mgombea mwenyewe, chama chake au mtu yeyote ambaye anaona anaweza
kumfanyia kampeni ndani ya katiba iliyopitishwa.
No comments:
Post a Comment