Pages

Tuesday, August 1, 2017

KUWAIT YATOA VIFAA VYA UPASUAJI VYENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI MIATATU.

Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jasen Al Najem akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (kulia) akiangalia baadhi ya zawadi za watoto wenye matatizo ya moyo toka kwa Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jasen Al Najem (kushoto) wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete mapema hii leo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza na baadhi ya wazazi wenye watoto wenye matatizo ya moyo wakati wa hafla ya kupokea vifaa tiba toka Ubalozi wa Kuwait kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jasen Al Najem.


Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jasen Al Najem (katikati) akimkabidhi mmoja ya watoto wenye matatizo ya moyo zawadi ya madaftari wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (kulia) akimkabidhi mmoja ya watoto wenye matatizo ya moyo zawadi ya madaftari wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa tiba kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete mapema hii leo jijini Dar es Salaam, katikati ni Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jasen Al Najem.



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla ya makabidhiano ya ...vifaa tiba kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jasen Al Najem na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi.
 

Na Thobias Robert - MAELEZO

Serikali ya Kuwait imetoa msaada wa vifaa vya upasuaji vyenye thamani ya Shilingi Milioni 325 kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuboresha huduma za upasuaji katika Taasisi hiyo.

Hayo yamebainishwa leo, Jijini Dar es Salaam na Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Jasem Al Najem wakati wa hafla ya  makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyika katika Taasisi hiyo. 

“Leo tumekuja hapa kutoa msaada wa vifaa vya upasuaji kwa ajili ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, lakini pia Serikali ya Kuwait itatoa msaada wa zaidi ya dola milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Mnazi Mmoja Visiwani Zanzibar,” amesema Balozi Jasem.

Ameongeza kwa kueleza kuwa Serikali ya nchi yake kupitia shirika lisilo la kiserikali la Help Patient Society litasaidia kutoa msaada wa damu salama katika Taasisi ya Mifupa (MOI) na kwamba zoezi hilo litafanyika  mwezi huu wa Agosti.

Vile vile amesema kuwa Kuwait inatarajia kutoa mabeseni 1,000 yenye vifaa mbalimbali vya kujifungulia kwa ajili ya mama na mtoto katika hospitali mbalimbali za Serikali hapa nchini, ambapo mpaka sasa mabeseni 250 yameshatolewa kwa hospitali za Mbagala Zakhem na Mkurunga.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa msaada huo ambao utaimarisha utoaji wa huduma katika Taasisi hiyo.

Aidha amesema kuwa, msaada huo uliotolewa na Serikali ya Kuwait utasaidia utoaji wa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa sita kwa siku kutoka idadi ya wagonjwa watatu iliyokuwepo hapo awali.

“Ninaridhishwa na huduma zinazotolewa na JKCI, ambapo kwa sasa tumepunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya Nchi hasa wagonjwa wa Moyo, kutoka wagonjwa 85 mwaka 2015/2016 hadi Wagonjwa 17 kwa mwaka 2016/2017,” ameeleza Ummy.

Ameendelea kwa kusema kuwa, hapo awali Taasisi hiyo ilikuwa ikifanya upasuaji wa wagonjwa 15 kwa mwezi lakini kwa sasa inatoa huduma ya upasuaji kwa wagonjwa 30 kwa mwezi. Kuongezeka kwa vifaa vilivyotolewa na Serikali ya Kuwait vitaongeza utoaji wa huduma ya upasuaji kwa zaidi ya wagonjwa 120 kwa mwezi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janubi amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Taaasisi hiyo mwaka 2005 imesaidia kutoa huduma ya upasuaji kwa zaidi ya wagonjwa 700. Hivyo kutolewa kwa msaada wa vifaa vipya utasadia kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa ambao hawajapata huduma hiyo kwa wakati.

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imekuwa msaada kwa Wananchi wa Tanzania lakini pia hata kwa Mataifa ya nje ikiwemo Kenya, Uganda na Malawi ambao wanaitumia Taasisi hiyo kama hospitali ya Rufaa.

No comments:

Post a Comment