Wakulima mkoani Shinyanga wakipatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya Mizani kabla ya msimu kuanza.
Wakulima mkoani Geita wakipatiwa Elimu
Afisa wa Vipimo Mkoani Kagera akitoa elimu na kuwaonesha wakulima mizani iliyo hakikiwa.
Maafisa wa Vipimo wakitoa elimu mkoani Shinyanga.
Meneja wa wakala wa Vipimo mkoani Mwanza akitoa elimu kwa Wakulima na wafanya Biashara.
- 3,070 Iliyo Hakikiwa yakutwa Salama.
Na Atley Kuni – Mwanza.
Jumla ya mizani 3,070 Iliyo
Hakikiwa katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa ajili ya matayarisho ya
ununuzi wa pamba kwa msimu wa 2017/2018 imekutwa salama mara baada ya
kuhakikiwa
na wakala wa Vipimo nchini.
Akizungumza nami Jijini Mwanza,
kaimu Meneja Sehemu ya Elimu, Habari na Mawasiliano Bi. Irene John,
amesema, Wakala wa vipimo Tanzania ( WMA) chini ya usimamizi wa Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeendelea kutoa elimu kwa wakulima
pamoja na kuhakiki mizani itakayotumika kununulia zao la Pamba ikiwa ni
maandalizi ya msimu wa ununuzi wa Pamba kwa mwaka huu.
Bi. Irene amesema, Dhumuni kuu
la utoaji elimu kwa wakulima wa zao la Pamba Kanda ya Ziwa ni
kuwawezesha wakulima kutambua mizani
iliyosahihi (inayoruhusiwa kwa biashara) na
ile iliyochezewa (isiyoruhusiwa kwa biashara) ili waweze kujilinda
wenyewe pindi maafisa vipimo wanapokuwa hawapo katika vituo vya kuuzia
Pamba yao, lakini pia ni kuwawezesha wakulima kupata faida ya thamani
kamili ya jasho lao.
Ameongeza kuwa, katika maandalizi
ya msimu mpya wa ununuzi wa Pamba zaidi ya mizani 1,402 imekaguliwa
katika mkoa wa Shinyanga, mkoa wa Simiyu wamekagua zaidi ya mizani
302, mkoa wa Geita jumla ya mizani 40 tayari imekaguliwa, ilihali
katika mkoa wa Mwanza wamekagua mizani 448, mkoa wa Mara mizani 690,
mkoa wa Tabora wamekagua mizani 164 pamoja na mkoa wa Kagera
wamekagua jumla ya mizani 24 ikiwa ni maandalizi ya ununuzi wa zao la
Pamba.
Katika hatua nyingine Irene
amesema, sheria ya Vipimo Sura 340 inawataka Wakala wa Vipimo kuhakiki
na kupiga chapa vipimo vyote vinavyotumika katika biashara ikiwa ni
pamoja na kuweka sticker kwa kipimo kitakachokuwa tayari
kimehakikiwa na kukutwa kikiwa sahihi ili iwe rahisi kwa wakulima kuona
na kutambua mizani iliyokaguliwa na kuruhusiwa kwa biashara kwa mwaka
husika.
“Wakala wa Vipimo nchini
itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza wakati wowote baada ya msimu
wa ununuzi wa Pamba kuanza ili panapokuwa na malalamiko kutoka kwa
wananchi kuhusu uonevu katika mizani yaweze kutatuliwa wa haraka”
amesema Irene
Aidha amewataka wakulima
wanaolalamikiwa kuweka maji, kokoto pamoja na mchanga kwenye Pamba kwa
ajili ya kuongeza uzito waache tabia hiyo mara moja sababu Sheria ya
vipimo ipo na inafanyakazi kwa pande zote mbili muuzaji na mnunuzi wote
kwa pamoja hawatakiwi kufanya udanganyifu wowote katika biashara.
Bi Irene hakusita kutaja faini
itakayotozwa kwa wote watakao banika kufanya udanganyifu “faini itaanzia
laki moja badala ya elfu kumi kama ilivyo zoeleka hadi milioni
ishirini endapo mkosaji atakubali kosa, endapo kesi itafikishwa
mahakamani na mlalamikiwa akakutwa kweli alikosa kulingana na ushahidi
utakaokuwa umetolewa “ na kusema “mshitakiwa atatozwa faini kuanzia laki
tatu hadi milioni hamsini au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa
pamoja”.
Irene alisema Tanzania ya viwanda
itafanikiwa endapo Mkulima, Mfanyabiashara watazingatia matumizi ya
vipimo sahihi kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji wa mazao, utumiaji
wa pembejeo, uuzaji, usafarishaji, upokeaji wa mazao, ufungashaji hadi
utumiaji wa mazao yenyewe.
Wakala wa Vipimo itaendelea kutoa
elimu kwa wakulima na wafanyabiashara ili wajue thamani ya kuuza kwa
kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni pamoja na
kumsaidia mkulima kupata fedha kulingana na thamani ya mazao yake,
kufanya biashara ya haki na kuepusha migogoro/migongano, kukuza uchumi
wa mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla
Bi. Irene alisema “elimu kwa
pande zote mbili (Mkulima na Mfanyabiashara) ni muhimu lakini zaidi kwa
mkulima kwani, mbali ya kutumia muda wake mwingi katika kuandaa
shamba, kulima, kupalilia na hata kuvuna bado ameoneka kuwa mnyonge
kwenye mazao yake ndiyo maana kwa sasa tunazunguka Kanda ya Ziwa mikoa
inayolima Pamba kwa wanunuzi na wakulima kwa ajili ya kutoa elimu ya
matumizi sahihi ya mizani kabla ya uuzaji wa zao la Pamba kuanza.
Afisa huyo amesema kuanzia hatua
ya awali ya kuandaa shamba hadi kuvuna mkulima anahitaji matumizi sahihi
ya vipimo lakini wakati wa kuuza mazao, umakini wa matumizi sahihi
ya vipimo unahitajika sana, ambapo kipimo kikiwa sahihi na kikatumiwa
kwa usahihi, kitatoa matokeo sahihi kumwezesha muuzaji (mkulima) kupata
fedha sawa na thamani ya bidhaa aliyouza.
Hivyo, nia na lengo la utoaji wa
elimu pamoja na uhakiki mizani ni kuwasaidia wakulima kabla ya msimu
wa Pamba kuanza wapate elimu ya kutosha hatimaye mkulima aweze
kupata fedha kulingana na thamani ya bidhaa atakayoizalisha na
kuwasilisha sokoni. “Mwaka huu tutajitahidi kuongeza elimu zaidi kwa
wakulima ikiwa ni pamoja na kuongeza kaguzi za kushutukiza ili
kuwadhibiti baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kuchezea mizani
kwa lengo la kuwaibia wakulima” alisema Kaimu Meneja Bi Irene.
No comments:
Post a Comment