Waziri wa Mambo ya ndani na Mbunge
wa jimbo la Iramba Mkoani Singida Mwigulu Nchemba akiwasha gari la
kubebea wagonjwa (ambulance), katika kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago
jimbo la Iramba.
Waziri wa Mambo ya ndani na Mbunge
wa jimbo la Iramba mkoani Singida Mwigulu Nchemba akizungumza kwenye
hafla ya kukabidhi gari la kubebea wagonjwa (ambulance) katika kijiji
cha Urughu tarafa ya Ndago jimbo la Iramba.
Mkazi wa kijiji cha Urughu jimbo
la Iramba mkoani Singida Jumanne Hatibu akizungumza kwenye hafla ya
makabidhiano ya gari la kubebea wagonjwa lililotolewa na serikali
kupitia wizara ya afya jinsia, wazee na watoto.
…………………………………..
Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge
wa jimbo la Iramba Mkoani Singida Mwingulu L. Nchemba, amekabidhi gari
la kubebea wagonjwa mpya na la kisasa ambalo limetolewa na
serikali
kupitia Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kituo cha afya cha
Ndago kilichopo Wilayani Iramba.
Mwigulu ameagiza gari hilo
lisitumike kama taksi au gari la kubebea mkaa, bali litumike kwa kazi
iliyokusudiwa ambayo ni kubebea wagonjwa na akina mama wajawazito tu.
Mbunge huyo ameyasema hayo juzi
wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi ‘ambulance’ hiyo
iliyofanyika katika kijiji cha Ndago jimbo la Iramba na kuhudhuriwa na
mamia ya wananchi.
Aidha, amesema ni marufuku
wagonjwa kuombwa kuchangia mafuta ya ambulance hiyo au gharama yo yote
ile, gari hili wagonjwa walitumie bure.
“Gari hilo lipatikane kituoni
wakati wote. Liwe na mafuta ya kutosha na dereva awepo. Gari hili ambalo
ni la kisasa, litunzwe na kulindwa ili liweze kutumika kwa miaka mingi
ijayo”, alisema Mwigulu.
Mbunge huyo ameishukuru serikali
ya awamu ya tano chini ya rais Magufuli na waziri Ummy kwa msaada huo
ambao utaokoa wapiga kura wake na wananchi kwa ujumla.
Awali mganga mfawidhi wa kituo cha
afya cha Ndago, Dkt Lyoce Mgelwa, alisema kituo hicho kinahudumia
tarafa nzima ya Ndago yenye wakazi 89,882.
Pia alisema kituo hicho kinapokea wagonjwa wanaopata rufaa katoka kwenye zahanati 10 zilizopo katika tarafa ya Ndago.
Dkt Lyoce alisema msaada huo wa
kupatiwa gari la kubeba wagonjwa ambulance, utapunguza kero
zinazowakabili wagonjwa wanaopewa rufaa kuchelewa kufika kwa wakati
katika hospitali ya wilaya.
“Wagonjwa wanaopewa rufaa
watawahishwa hospitali ya wilaya ili kuokoa maisha ya wagonjwa na hasa
akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano. Upunguzaji wa
vifo hivyo, wilaya itakuwa imepiga hatua kubwa kufikia lengo namba nne
na tano la maendeleo ya milenia hadi kufika mwaka 2020”, alisema.
Aidha, Dkt Locye ametumia fursa
hiyo kuomba wadau mbalimbali kuwaunga mkono katika kukamilisha jengo lao
la kulaza wagonjwa (wodi).
“Wananchi wa jimbo la Iramba,
tunaendelea kukushukuru wewe mbunge wetu Mwingulu kwa misaada mingi
unayoendelea kuitoa kwenye maeneo mbalimbali katika kuboresha huduma za
jamii, ikiwemo huduma muhimu za afya”, alisema.
Kwa upande wake Jumanne Hatibu
mkazi wa kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago alisema kabla ya ujio wa
ambulance hiyo kijiji hicho kilikuwa kinakabiliwa na tatizo sugu la
usafiri kwa wagonjwa hasa akina mama wajawazito.
“Kijiji chetu kwa miaka mingi
tulikuwa tukitegemea usafiri wa basi na lilikuwepo basi moja tu.
Likiondoka asubuhi kwenda Singida hakuna tena usafiri kwa siku husika
hadi kesho asubuhi. Kwa hiyo kwa wagonjwa na hasa akina mama wajawazito,
ilikuwa ni changamoto kubwa. Ambulance hii, itaokoa maisha ya wakazi wa
tarafa ya Ndago na maeneo jirani”, alisema Hatibu ambaye ni mlemavu wa
miguu.
Wakati huo huo, Mbunge Mwingulu ameahidi kuchangia ujenzi wa wodi ya kituo cha afya Ndago kwa kutoa mifuko mia moja ya saruji.
No comments:
Post a Comment