*Asema waliouza eneo la hifadhi wawajibishwe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Majid Mwanga aende kata ya
Saadani na kukaa na uongozi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya
Saadani
ili watambue kwa pamoja mipaka iliyowekwa na Serikali.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo
wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Saadani na Matipwili wilayani
Bagamoyo, mkoani Pwani ambao walisimamisha msafara wake wakati akitoka
Hifadhi ya Taifa ya Saadani kukagua miundombinu.
“Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi,
Afisa Ardhi njoo na ramani yako na Mhifadhi Mkuu naye aje na ramani
yake, kaeni na Mwenyekiti wa Kijiji na kamati yake ya ardhi; muende beacon kwa beacon kwa
kutumia kifaa cha GPS ambacho kitawaongoza kubainisha huo mpaka
umepitia wapi. Nahitaji kupata taarifa kuhusu jambo hili kuwa
limetekelezwa,” alisema.
Alisema anazo taarifa kuwa baadhi
watu kwenye kijiji hicho wamewauzia ardhi wakazi kutoka Dar es Salaam
wakati wakijua kuwa ardhi hiyo ni mali ya hifadhi ya Saadani. “Hao watu
wasakwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria kwa sababu hakuna mtu
anayeruhusiwa kuuza ardhi ya hifadhi,” alisisitiza.
Alisema mikoa, wilaya, vijiji
kila kimoja kina mipaka yake ambayo inatambulika na ilikwishatolewa
kwenye gazeti la Serikali. “Vijiji vyote vina mipaka ambayo inatambulika
rasmi na ramani zake ziko ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kikiwemo na hiki
kijiji chenu. Lakini baadhi ya vijiji vina maeneo ya hifadhi. Tunataka
mtambue kuwa mipaka hiyo ipo rasmi, na kwamba inapaswa iheshimiwe,”
aliongeza.
Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi
hao kuwa alilazimika kupita Saadani wakati akitokea Wami, ili aweze
kufuatilia ni kwa nini hifadhi hiyo haitangazwi vya kutosha wakati iko
karibu na Dar es Salaam na watalii wengi wanapita hapo wakati wakirudi
makwao.
“Serikali imenunua ndege za
kuleta watalii wengi zaidi nchini lakini hadi sasa ni mbuga zilezile
ambazo zinapata watalii. Tunataka mbuga hii iliyoko karibu na Dar es
Salaam itangazwe na ijulikane zaidi ili wale ambao hawana muda wa kwenda
mikoa ya mbali waje hapa na kuona rasilmali tulizonazo,” aliongeza.
Hifadi ya Saadani ambayo iko
umbali wa km. 45 kutoka Bagamoyo na km. 100 kutoka Dar es Salaam, ina
mvuto wa kipekee kwani ndiyo hifadhi pekee unayoweza kuona wanyama
wakijivinjari katika fukwe za Bahari ya Hindi kwa vile imeunganisha
nyika na bahari.
Hifadhi hiyo iko kati ya mikoa ya
Pwani na Tanga, katika wilaya za Bagamoyo na Pangani, ikiwa na ukubwa
wa zaidi ya km. za mraba 1,000, ikijumuisha maeneo ya Mkwaja na misitu
ya Zaraninge na Tumbirini.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri
Mkuu alikuwa amefuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mkoa pwani, Eng. Evarist
Ndikilo, viongozi wa wilaya ya Bagamoyo na Mbunge wa jimbo hilo,
Ridhiwani Kikwete.
No comments:
Post a Comment