Jovina Bujulu- MAELEZO.
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona mabango ya matangazo barabarani ambayo wanayatilia shaka.
Haya yanasemwa jijini
Dar-es-salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Ajira na watu wenye Ulemavu Mh. Janista Mhagama alipokuwa akizungumzia
uwepo kwa
utitiri wa mabango ya ajira yanayoambatana na ahadi za uongo
kwenye mishahara.
Alisema kuwa sheria za uwekaji
mabango barabarani zinazoongozwa na mamlaka husika zikiwemo Serikali za
Mitaa, Halmashauri ya Jiji na Miji ambazo huweka kanuni na taratibu za
mabango hayo.
“Mamlaka husika zina wajibu wa
kujiridhisha na kuhakikisha mabango yanayopewa ruhusa kubandika
barabarani ni sahihi, yanatangaza ukweli na yanafuata maadili” alisema
Mhe. Mhagama.
Waziri Mhagama aliongeza kuwa
ikibainika kuwa mabango hayo yanakwenda kinyume na utaratibu
waliokubaliana, mamlaka husika wana wajibu wa kuyafuatilia na kuyaondoa
mabango hayo ili kuondoa usumbufu usiowa lazima kwa wananchi.
Akizungumzia suala la mabango
yanayotangaza ajira yanayoambatana na ahadi za uongo, Mhe. Mhagama
amesema kuwa kuwa wizara yake ndiyo yenye dhamana ya ajira, inabidi
wawasiliane na mamlaka husika ambazo zimeruhusu mabango hayo ili
wafuatilie na kuchukua hatua stahiki.
Aidha, alizungumzia ukaguzi
unaofanywa na wizara yake mahali pa kazi alisema kuwa wao hawafuatilii
mabango bali huenda kufuatilia kama mwajiri anafuata sheria za kazi
ikiwemo mikataba, mishahara, afya na kupeleka michango ya wafanyakazi
katika mifuko ya hifadhi za jamii.
“Tunapokuta malalamiko ya
wafanyakazi, au kukuta mwajiri hapeleki michango ya wafanyakazi kwenye
mifuko ya jamii, kuna adhabu za hapo kwa hapo kama vile kumtoza mwajiri
pesa” alisema Mhe. Mhagama.
Katika kuhakikisha utendaji kazi
unaridhisha na maridhiano sehemu za kazi Mhe. Mhagama alisema kuwa wao
kama wasimamizi wakuu wa ajira nchini wanafanya kazi kwa karibu na
shirikisho la vyama vya wafanyakazi na waajiri, ili kutatua kero za
wafanyakazi katika sehemu zao za kazi.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa
jiji la Dar-es-Salaam Mhe. Isaya Mwita alisema kuwa utaratibu wa kuweka
mabango upo kisheria katika halmashauri ila usumbufu mkubwa ni kuwa
matangazo madogo madogo ambayo mengi yanawekwa kwenye karatasi za A4
ambayo yanabandikwa kwenye kuta za nyumba, nguzo za umeme na miti bila
kufuata utaratibu.
“Kwa sasa tunafanya utaratibu wa
kukutana na viongozi wa jiji wakiwemo madiwani, wenyekiti wa
halmashauri, wenyekiti wa wilaya na wengine ili kuweka utaratibu wa
kudhibiti matangazo hayo, pamoja na kuweka sheria ndogo ndogo, na hivyo
kuwapunguzia kero wananchi ambao wanaumizwa na matangazo hayo” alisema
Mhe. Mwitta
No comments:
Post a Comment