WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri na Manispaa nchini kuacha
kutoa fedha taslimu na kuwapa madiwani ili zikafanye kazi za maendeleo.
Badala yake amewataka waandae
mfumo maalum wa kutoa fedha hizo kama zinavyotolewa fedha za mfuko wa
Jimbo ambazo ni maalum kwa wabunge lakini zinatumika kwa shughuli za
maendeleo jimboni.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumatano, Januari 4, 2017) wakati akizungumza na viongozi na watendaji
wa mkoa wa Ruvuma mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu
ndogo Manispaa ya Songea.
“Nimepata taarifa kuwa fedha za
maendeleo kwa madiwani zinakabidhiwa mkononi. Hapana. Msiwape fedha
mkononi, bali zifuate mfumo wa utoaji fedha wa Serikali. Kama mlikuwa na
matumizi ya aina hiyo, mwisho wake ni jana,” amesisitiza.
“Fedha za mfuko wa Jimbo ni za
Mbunge lakini hapewi mkononi bali zinapelekwa kwenye Halmashauri na yeye
anahusika kwenye kikao cha maamuzi. Anakubaliana na madiwani wenzake ni
miradi ipi ipatiwe fedha, ambayo mara nyingi inakuwa
imekwishaidhinishwa na vikao husika,” ameongeza.
Alisema makusanyo ya fedha
yanayofanywa na Halmashauri hayana budi kuangaliwa pia na jinsi fedha
hizo zinavyotumiwa. “Lazima tukishakusanya tuangalie tumepata kiasi
gani, siyo kukaa na kuamua kutoa sh. laki tano tano kwa kila diwani.
Suala la matumizi ni muhimu sana, ni lazima fedha hizo ziende kwenye
miradi ya maendeleo,” amesisitiza.
Amesema kuna baadhi ya watu
wanaamua kugawana fedha kwa kigezo cha maendeleo lakini wanaishia
kutumia fedha hizo kwa kigezo cha kujengeana uwezo (capacity building).
“Hii si sahihi na jana nimepiga marufuku posho za aina hii pamoja na
fedha za vitafunwa kwa sababu zinaishia kwa wakubwa wachache na
waliozikusanya hawapati chochote,” ameongeza.
Akizungumzia kuhusu ukusanyaji wa
mapato kwenye Halmashauri, Waziri Mkuu amewataka waangalie baadhi ya
makampuni ambayo yanajitokeza kutoa vifaa vya kukusanya ushuru lakini
wanatumia software ambazo zinawanufaisha na wao pia.
“Tumieni watu wenu wa TEHAMA
kukagua mifumo hii kwani kuna baadhi ya watu wanaoleta zile mashine siyo
waaminifu. Watu wa TEHAMA wazikague na kujiridhisha kuwa hakuna mianya
ya wizi. Tumegundua wako wanaokusanya fedha, lakini asilimia 80 inangia
kwenye akaunti za Halmashauri na asilimia 20 inapelekwa sehemu
wanayoijua wao. Ukiangalia unaona mapato yanaongezeka lakini kumbe pia
unaibiwa. Jaribuni kuchunguza na mjiridhishe na hizo software zao,” amesisitiza.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, JANUARI 4, 2017.
No comments:
Post a Comment