Na Mwandishi Wetu,
Umoja wa Vijana wa Chama
Cha Mapinduzi (UVCCM) umewataka watendaji na watumishi wa Makao Makuu
ya jumuiya hiyo kuanza kujipima, kujitathmini na kujipanga upya
kimamakati kwa sababu muda wa kupiga maneno haupo ila vinavyohitajika
ni uwezo binafsi na vitendo.
Pia umoja huo
umewasisitiza watendaji , wahudumu na watumishi wa jumuiya hiyo
kuongozwa na msingi ya nidhamu, uwajibikaji kazini na kuacha tabia za
mzaha na masikhara wakati wa kazi.
Kaimu Katibu Mkuu UVCCM
Taifa Shaka Hamdu Shaka alitoa maelezo hayo jana alipokutana na
kufanya kikao na watumishi wa UVCCM Makao Makuu kwa ajili kutathmini
utendaji wa jumuiya kwa mwaka 2016 na kupanga mikakati ya utekelezaji wa
majukumu kwa mwaka 2017.
Shaka alisema pamoja na kusikiliza michango , maoni , ushauri ,
mawazo na changamoto zinazowakabili watumishi na namna ya kuzitatua kwa
mwaka 2017 lazima uwe mwaka wa vitendo na mafanikio.
“Tutabadili kila kona
yenye kasoro au dosari , lengo si kukomoana ila ni katika kujipanga tena
upya, asiyeweza aseme hawezi ili akae kando , kama mtu hajimudu
hatapewa dhamana yoyote kwasababu ya ushikaji na urafiki “Alisema Shaka.
Aidha Kaimu Katibu Mkuu
huyo alisema makao makuu inahitaji kuwa kama kioo, sifa ya kioo ni
kujiona na kujitambua, kama umechafuka jisafishe ili uwe nadhifu na
makini bila mtu kusukumwa.
Alisema kila
aliyepangiwa kazi yake aifanye kwa mujibu wa hadidu za rejea na
maelekezo ya kikanuni hivyo asiyetaka kujituma na kutimiza wajibu wake
atakuwa haitakii mema jumuiya na hivyo hatavumiliwa na kutazamwa.
“Tukijipanga vyema hapa
Makao Makuu, kila mmoja akatimiza wajibu wake naamini mambo yakaenda
kama inavyotakiwa, hakuna urasimu wala njoo kesho, wenzetu wilayani na
mikoani watatueheshimu, tukiwatuma watatumika na kutupatia majawabu
chanya “Alieleza
Hata hivyo Shaka
aliwataka wana jumuiya mahali popote walipo nchini wajione na
kujihesabu wao ni ndugu wa tumbo moja, wapendane, wasikubali kukaribisha
majungu au hasama kwasababu zama hizo zimepita na hazitarejea tena.
Pia aliwakumbusha
watendaji hao wa makao makuu kutunza siri za ofisi, nyaraka muhimu
ikiwemo na kujiandaa vyema kufanikisha uchaguzi Mkuu ujao kwa mujibu
wa taratibu, kanumi na katiba ya ccm.
“Ukipewa jukumu la
kusimamia tenda haki, timiza wajibu wako bila upendeleo, ukiharibu na
kuvurunda utaadhibiwa bila huruma na si hasha ukajifukuzisha kazi
mwenyewe kwa ukiukaji wako wa maadili na kanuni ya utimishi”alisisitiza
Shaka .
Kaimu huyo Katibu Mkuu alimsifu na
kuwashukuru Mwenyekiti wa UVCCM sadifa Juma Khamis, Makamo Mwenyeliti
Mboni Mhita , manaibu makatibu wakuu wake, wakuu wa idara na watendaji
wote wa jumuiya hiyo kwa kumpa ushirikiano katika kutimiza majukumu
na kuifanya jumuiya yao kuendelea kukamilisha mabadiliko makubwa ya
kimfumo na kiutawala.
No comments:
Post a Comment