WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zote
zilizotengwa kwa ajili ya posho mbalimbali zisizokuwa za kisheria
zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Ametia agizo hilo leo (Jumanne,
Januari 3, 20017) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa ya
Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.
“Kuanzia sasa marufuku Wakurugenzi
kutoa posho zisizotambulika kisheria zikiwemo za mazingira magumu,
kujenga uwezo na vitafunwa katika halmashauri zenu na badala yake fedha
hizo zitumike kwenye miradi ya maendeleo,” amesema.
Agizo hilo litawezesha Jiji la Dar
es Salaam kuokoa sh bilioni 130 zilizokuwa zitumike na Halmashauri na
Manispaa za jiji hilo, ambazo kwa sasa zitaingizwa kwenye miradi na
shughuli za maendeleo.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka
watumishi wa umma nchini kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuacha
kutumia fedha kinyume cha utaratibu na watakaobainika Serikali haitosita
kuwachukulia hatua kali za kisheria.
“Katika halmashauri zetu kila
mtumishi anashiriki katika ukusanyaji wa mapato hadi walinzi, lakini
mwisho wa siku vitafunwa huliwa na wachache wanaojiita wakubwa huku
wengine wakisikilizia kwa nje. Jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesisitiza kwamba
Mkurugenzi yeyote atakayebainika kulipa posho hizo baada ya siku ya leo
atakuwa amejifukuzisha kazi.
Aidha, ameagiza fedha zilizokuwa
zikitolewa kwa madiwani kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo zisitolewe
moja kwa moja kwa madiwani na badala yake zipelekwe kwenye kata husika
na zifuatiliwe matumizi yake.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amezionya
halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila fedha zinayopelekwa kwenye
halmashauri hizo inatumika kama ilivyokusudiwa na atakayebainika
kutumia kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Pia amewataka watumishi wote wa
umma nchini kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha wanawatumikia vyema
mwananchi ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi na kujiingiza kwenye
vitendo vya rushwa na ufisadi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa
siku tatu kwa watumishi 10 wa halmashauri hiyo ambao wamehamishiwa
kutoka wilaya ya Temeke wawe wameripoti katika Manispaa hiyo, vinginevyo
watakuwa wamejifukuzisha kazi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni
Bw. Hashim Mgandilwa wakati akiwasilisha taarifa ya wilaya hiyo kwa
Waziri Mkuu, alisema hadi sasa asilimia 98 ya watumishi waliotakiwa
kuhamia kwenye halmashauri hiyo wameripoti isipokuwa 10 na hakuna
taarifa zozote juu yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
- L. P. 3021,
JUMANNE, JANUARI 3, 2017
No comments:
Post a Comment