WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wananchi kuacha tabia ya kuhifadhi fedha nyingi majumbani na
badala yake wajenge utamaduni wa kuzipeleka benki kuepusha kuhatarisha
usalama wao.
Ametoa ushauri huo jana (Jumatatu,
Desemba 5, 2016) wakati akifungua tawi la benki ya Biashara ya Uchumi
lililopo wilayani Karatu mkoani Arusha akiwa katika ziara yake ya kikazi
mkoani hapa.
Alisema tabia ya baadhi ya
wananchi kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha majumbani si nzuri kwa sababu
wanahatarisha usalama wao, hivyo ni vyema wakatumia benki mbalimbali
zilizoko kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutunza fedha zao.
Akizungumzia kuhusu kufunguliwa
kwa tawi la benki ya Uchumi wilayani Karatu, Waziri Mkuu alisema
unaashiria ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo kwa kuwa benki ni kichocheo
cha maendeleo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
aliushauri uongozi wa benki ya Uchumi kuangalia uwezekano wa kupunguza
kiasi cha riba wanachokitoza katika mikopo wanayoitoa ili kuwawezesha
wananchi kukopa na kupata tija.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi wa benki hiyo Bw. Wilson Ndesanjo alisema benki hiyo
inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mtaji mdogo jambo
linalowasababisha washindwe kufungua matawi katika mikoa mingine.
“Changamoto nyingine ni baadhi ya
wateja kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati, ambapo hatua za kisheria
zikichukuliwa wanakimbilia mahakamani. Matukio haya yanadhoofisha kasi
ya utoaji wa huduma kwani kesi zinachukua muda mrefu,” alisema.
Bw. Ndesanjo alisema kuna baadhi
ya kesi zimechukua miaka sita bila ya kumalizika hivyo kuzuia fedha
ambazo kama zingerejeshwa kwa wakati zingezungushwa kwa wananchi
wengine.
Benki ya Uchumi ilianzishwa
Septemba 22, 2005 ikiwa na mtaji wa sh. milioni 372. Hadi kufikia
mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2016 mtaji huo umefikia sh. bilioni 5.4 hivyo
umeongezeka mara 14.5 zaidi ya ule wa awali uliokuwepo wakati wa
uanzishwaji wake.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMANNE, DESEMBA 6, 2016.
No comments:
Post a Comment