Na: Frank Shija, MAELEZO.
WATANZANIA watakiwa kufanya
jitihada za makusudi katika suala zima la utunzaji wa mazingira ikiwa ni
hatua za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Hali ya hewa na Tabia
nchi.
Rai hiyo imetolewa leo na Makamu
wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifungua Tamasha la
Kimataifa linalohusu Mabadiliko ya Tabia ya Nchi linalowakutanisha
Wanasayansi, Watafiti na wadau wa mazingira chini ya Usimamizi wa Kigoda
cha Mwalimu Julius Nyerere cha Mazingira na Mabadiliko ya Tabia ya
nchi.
Amesema kuwa suala la Mabadiliko
ya Hali ya Hewa na Tabia nchi siyo hadithi ni jambo ambalo lipo wazi
kuwa ni janga ambalo ipo haja ya kuchukua hatua za makusudi katika
kutatua changamoto zake.
“Wadau wote tuone haja ya
kuyatunza mazingira yetu mwananchi na wadau wa mazingira kwa ujumla, ni
muhimu kwa umoja wetu tukaongeza jitihada za kupanda miti katika maeneo
yetu ili kukabiliana na hali tete ya uharibifu wa mazingira
nchini”.Alisema Mama Samia.
Aidha alisema kuwa wakati sasa
umefika wa kuacha uharibifu wa mazingira kuanzia leo na kuanza kuyatunza
ili kukabiliana na athari za Mabadiliko hayo ya Hali ya Hewa na Tabia
nchi.
Awali akimkaribisha Makamu wa
Rais, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella
Manyanya amesema kuwa umefika wakati wakuitazama upya mitaala yetu ili
kutoa fursa kwa elimu ya mazingira inaingizwa katika masomo kuanzia
ngazi ya msingi.
Aliongeza kuwa elimu ikitumika
vizuri inaweza kusaidia kwa kuongeza uelewa miongoni mwa jamii hali
itakayopelekea wananchi kutambua namna ya kukabiliana na athari za
mabadiliko hayo na ikiwa ni pamoja na namna ya kuyahifadhi.
Mhandisi Manyanya alisema kuwa ni
faraja kuona Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinamuenzi Mwl. Nyerere kwa
Kuwa na Kigoda cha Mwalimu kinachohusiana na Mazingira kwani ni ukweli
kwamba Mwalimu alikuwa Mwanamazingira na Muhifadhi wa Mazingira ndiyo
maana utaona aliweza kuweka maeneo mengi ya Hifadhi za Taifa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala alisema kuwa
imekuwa ni kawaida duniani kote kuwa na Vigoda ambavyo utumiwa kama njia
ya kuwaenzi baadhi ya watu kwa michango yao.
Wao kama Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam wanamuenzi Baba wa Taifa kwa kuwa na Kigoda cha Mwalimu ambacho
kilianzishwa mwaka 2008 kikiwa kimoja na kuongeza kuwa mpaka kufikia
sasa vimeanzishwa Vingine viwili ambacho kimoja kinahusu Elimu ya
Maendeleo na kingine ndicho hiki cha Masuala ya Mazingira ambacho
kinafanya kazi nzuri sana.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha
Mafunzo ya Mabadiliko ya Tabia ya nchi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
amabye pia ndiye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha
Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi, Profesa Pius Yanda amesema
mkutano huo wa siku TANO utakuwa na jukumu kubwa la kujadili kwa kina
namna bora ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabia ya nchi.
No comments:
Post a Comment