Pages

Friday, May 1, 2015

UKIUKAJI WA SHERIA: Selcom yazuiwa kuuza Luku

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene. 
Na Suzan Mwillo, Mwananchi
Kwa ufupi
  • Serikali imeiagiza Tanesco kumtafuta mzabuni mwingine wa kuuza umeme kwa wateja kwa kushirikiana na Maxcom

Dar es Salaam. Serikali imefuta mkataba wake na kampuni ya Selcom iliyokuwa inauza umeme wa Luku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni ubabaishaji katika kutoa huduma hiyo.
Pia kampuni hiyo, ambayo imekuwa ikinunua umeme wa jumla kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imesitishiwa mkataba huo kutokana na kukiuka sheria na taratibu za ulipaji wa kodi.
Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa Selcom, Sameer Hirji hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
“Siwezi kuzungumzia chochote kuhusu hilo (mkataba). Tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (leo),” alisema.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene aliitaka Tanesco kufuata uamuzi wa Serikali kwa kuwa Selcom imekuwa ikilalamikiwa na wateja kuwa na matatizo ya kiufundi kila wanaponunua umeme, hasa ifikikapo mwisho wa mwezi.
“Hatuwezi kuendelea kuvumilia hali hii kwa sababu hafai. Hiyo nafasi tumeiondoa, tunawapa wengine. Utendaji wao mbovu na umekuwa ukisababisha wananchi kukosa umeme.
“Mteja anafika kwa wakala kununua umeme, anaambiwa hakuna, tunarekebisha mitambo yetu,” alisema.
Selcom na Maxcom ndiyo kampuni pekee zilizoshinda zabuni za kuuza nishati hiyo na kuingia mkataba na Tanesco wa kununua umeme wa jumla na kuuza kwa rejareja. Hata hivyo imeelezwa kuwa Maxcom imekuwa ikifanya vizuri kuliko Selcom.
Simbachawene, ambaye amechukua nafasi iliyoachwa na Profesa Sospeter Muhongo, alisema pia wameichukulia hatua za kisheria kampuni hiyo kutokana na kukuika taratibu za kulipa kodi.
“Kwa mujibu wa sheria za kodi hawawezi kuendelea kutoa huduma na hili wala halina athari zozote kwa sababu wao ndiyo wamevunja sheria... naomba wananchi wanunue umeme katika vituo vya Maxcom hadi pale tutakapopata muuzaji mwingine,” alisema
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo walipokea barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiwataka wasitishe mkataba wao na Selcom.
“Ukiachilia mbali malalamiko yaliyokuwa yanatolewa na wananchi. TRA walituambia tusifanye kazi na hao jamaa huku wakiwatuhumu kwa kugushi nyaraka na kukiuka taratibu za kulipa kodi.

No comments:

Post a Comment