Historia yake
Mwigulu Lameck Nchemba alizaliwa Januari 7, 1975
mkoani Singida, hivyo alifikisha miaka 40 Januari 7, mwaka huu. Kwa sasa
yeye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) upande wa
Tanzania Bara na ni Naibu Waziri wa Fedha.
Mwigulu alianza masomo yake katika Shule ya Msingi
Makunda wilayani Iramba, Singida mwaka 1987 na kuhitimu mwaka 1993.
Alijiunga na Shule ya Sekondari Ilboru kwa masomo ya kidato cha I – IV
mwaka 1987 – 1993 kisha akafaulu na kuanza kidato cha V na VI Mazengo
Sekondari, Dodoma.
Baada ya kukamilisha masomo yake ya kidato cha
sita, Mwigulu alichaguliwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
akisomea masuala ya Uchumi. Alihitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi mwaka
2004 na kupata daraja la kwanza, akaunganisha kusomea Shahada ya Uzamili
ya Uchumi ambayo aliikamilisha mwaka 2006.
Baada ya kukamilisha masomo yake, Mwigulu
alijiunga na utumishi wa umma katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
kitengo cha sera za uchumi, akiwa mchumi daraja la I na wakati huohuo
akiendelea na harakati za siasa ndani ya CCM.
Nyota yake kisiasa ilianza kung’ara mwaka 2001
alipochaguliwa kuwa mjumbe wa vijana wa Wilaya ya Iramba, mwaka 2008
akawa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) na mwaka huohuo,
akachaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu kupitia Umoja wa Vijana
(UVCCM). Mwigulu ameoa na ana watoto.
Mbio za ubunge
Mwigulu anatoka katika familia ya kawaida ya
wazazi wasio na uwezo sana. Yeye mwenyewe anasema kama isingelikuwa
“sera ya kutoa mikopo kwa wanafunzi,” basi asingelisoma. Pamoja na
umasikini wa familia yake, yeye alikuwa na ndoto kubwa, alihitaji kuwa
mwakilishi wa wananchi wa jimbo alilozaliwa ili atumie elimu na uzoefu
wake kuwasaidia wananchi.
Mwaka 2010, Mwigulu aliacha kazi nzuri pale BoT
akajitosa kwenye kinyang’anyiro cha kuusaka ubunge wa Jimbo la Iramba
Magharibi. Alitumia vizuri udhaifu wa Mbunge wa Iramba Magharibi wakati
huo, Juma Hassan Kilimba, akaomba ridhaa kwa chama chake na kufikia
hatua ya kura za maoni ambako alimshinda Kilimba kwa kura chache na
kufanikiwa kuteuliwa na CCM kuwania nafasi hiyo.
Katika uchaguzi wa jumla, nguvu ya Mwigulu
iliamsha uimara wa CCM akapata asilimia 87.6 dhidi ya asilimia 9.4 za
vyama vyote vya upinzani, akawa Mbunge wa Jimbo la Iramba.
Mwigulu aliendelea na safari yake ya utumishi kwa
wana Iramba Magharibi na ilipofika Aprili 2011, Katibu Mkuu wa CCM wa
wakati huo, Yussuf Makamba na sekretarieti nzima walipojiuzulu ili
kutekeleza ile dhana ya “kujivua gamba,” chama hicho kilimteua Mwigulu
kushikilia wadhifa wa Katibu wa Uchumi na Fedha chini ya Katibu Mkuu
mpya, Wilson Mkama.
Katika uchaguzi mkuu wa viongozi wa CCM Novemba
2012, Mkama alipumzishwa katika majukumu yake na CCM ilijiunda upya,
sekretarieti ikiwekwa chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana. Mwigulu
alipanda kisiasa na kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara.
No comments:
Post a Comment