Katika albamu hii ya UWEKEZAJI TANZANIA, Muunganiko wa Wanamuziki Wakongwe na wa Kisasa wa Tanzania (Tanzania All Stars) wamefanya kazi kubwa sana. Hapa chini tunakufafanulia maudhui ya nyimbo zote tisa zilizoko kwenye albamu hii;
1. Kiswahili Kiingereza cha Afrika* - UNESCO ilikitambua kiswahili kama lugha ya kibiashara Afrika; kwa hiyo kitatumika katika maeneo yote muhimu, mathalani mahakama za juu zimeanza kutumia kiswahili kuweka kumbukumbu zake, mikutano mbalimbali ya kimataifa ya Afrika imekiidhinisha kuwa lugha ya kipekee, ndiyo kusema kiswahili ni zaidi ya lugha, ni maisha!
*2. Kuwajibika* - Viongozi na wenye dhamana za umma wanaaswa kuwa waadilifu na kuachana na masuala ya rushwa na kukosa uaminifu katika majukumu yao; jambo ambalo mara nyingi limepelekea serikali ipate hasara au wananchi wakose haki.
3. Mazingira ni Uhai* - Hivi karibuni dunia imekumbwa na janga la mabadiliko ya tabia nchi, mvua zinanyesha chini ya kiwango, mito inakauka, uoto wa asili unatoweka na madhara makubwa yanatokea. Ikiwa mazingira yataendelea kuharibiwa, uhai wa kila mwanadamu wa kizazi cha sasa na baadaye uko mashakani.
4. Uhuru wa Tanzania* - Tangu nchi ipate uhuru imepita katika miongo 6 na imo kwenye awamu ya 6 ya uongozi; nyakati zote hizo ni za milima na mabonde, mafanikio na changamoto nyingi na safari bado ni ndefu. Ukitafakari taifa lililotoka na linakoelekea unajifunza kuwa ili kufikia malengo ni muhimu watu waendelee kuishi kwa kuvumiliana katikati ya tofauti zao za kiitikadi, kidini, kiuchumi na katika hali zozote. Na ni wajibu wetu kuhakikisha mifumo ya uvumilivu wa kweli inaendelea kujengwa na kusimamiwa.
*5. Tanzania Music Clarification* - Wimbo huu umetungwa kwa ajili ya kulishukuru kundi la whatsup ambalo limeunganisha wanamuziki na wadau wa muziki Afrika Mashariki na Kati kwa ajili ya kushauri masuala ya maslahi na haki za wasanii; kukutanisha wanamuziki wa sasa na kizazi cha zamani na kuwafanya wawe na mawazo ya pamoja yanayohusu mustakabali wa muziki na wanamuziki, haki zao na matumaini yao ya mbeleni.
6. Rais Samia* - Wimbo maalum kwa ajili ya kumpongeza Rais wa awamu ya VI Dr. Samia Suluhu Hassan, Mwanamke wa Kwanza kuwa Mkuu wa nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati - kwa kazi anayofanya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo watanzania. Wimbo huu uko kwenye mahadhi na mtindo wa ZUKU/ZOUK.
7. Ushirikiano wa Kimataifa* - Mahusiano ya Tanzania na nchi za nje na namna Tanzania ilivyo kisiwa na kimbilio la wengi katika mahusiano ya kimataifa na nchi inaendelea kupiga hatua za maendeleo kwa sababu ya utulivu wake na kwa sababu ya kuishi vema na majirani tangu na kabla ya uhuru.
8. Utalii* - Vivutio vya Utalii Tanzania na kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea vivutio hivyo. Wimbo huu unaelezea pia juhudi za Rais SSH katika kukuza utalii wa Tanzania. Tofauti na nyimbo zingine kwenye albamu hii, wimbo huu umetengenezwa kwa mahadhi na mtindo wa singeli ambao unapendwa sana na vijana.
9. Uwekezaji Tanzania* - Wimbo huu unaweza kukushangaza, umeimbwa kwa lugha 8; Kilingara, kiingereza, kiswahili, kichina, kiswidi, kijerumani, kiarabu na kifaransa. Wimbo huu unahamasisha uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi pamoja na vivutio vya uwekezaji vya kifedha na visivyo vya kifedha.
Tunakukaribisha sana kuwasikiliza TANZANIA ALL STARS katika kazi iliyopo kny album hii iitwayo UWEKEZAJI TANZANIA iliyosheheni maudhui ya kudumu kwa miaka mingi ijayo.
No comments:
Post a Comment