Pages

Monday, July 11, 2022

KISWAHILI LUGHA RASMI TUZO ZA SHEKHE HAMAD, QATAR

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA,)  Bi. Consolatha Mushi akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kuteuliwa kwa lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi katika tuzo za Shekhe Hamad za nchini Qatar na kueleza kuwa  fursa za lugha adhimu ya Kiswahili ni nyingi na watanzania wazitumie kwa manufaa binafsi na Taifa kwa ujumla na kupitia tuzo hizo BAKITA itawapokea washiriki kwa ushauri pamoja na uchambuzi wa mada walizochagua, Leo jijini Dar es Salaam.
 
 

* zimelenga uga wa tafsiri ya lugha za Kiswahili na Kiarabu, mshindi kujinyakulia kitita cha dola laki moja

*BAKITA yafungua milango kwa washiriki, kuwasaidia katika uchambuzi wa mada

 

BAADA ya ulimwengu kuanza kuadhimisha siku ya Kiswahili duniani Julai 7, mwaka huu  fursa zaidi zimeendelea kufunguka ambapo kwa mara ya kwanza Kiswahili kimeteuliwa kuwa lugha rasmi katika tuzo za tafsiri za Shekhe Hamad 2022 zinazotolewa nchini Qatar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA,)  Bi. Consolatha Mushi amesema fursa za lugha adhimu ya Kiswahili ni nyingi na watanzania wazitumie kwa manufaa binafsi na Taifa kwa ujumla na kupitia tuzo hizo BAKITA itawapokea washiriki kwa ushauri pamoja na uchambuzi wa mada walizochagua.

Bi. Consolatha amesema kuwa, Tuzo hizo zinahusisha uga tafsiri yaani,  kuhamisha ujumbe kutoka lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiarabu au kutoka lugha ya Kiarabu kwenda lugha ya Kiswahili kwa njia ya maandishi na mshindi atatunukiwa  zawadi nono ya dola laki moja.

Amesema, dirisha la ushiriki wa tuzo hizo limefunguliwa na litafungwa Agosti 15 mwaka huu na kazi za tafsiri zitakazowasilishwa mwaka huu zimefungamanishwa na uga wa  masuala ya kibinadamu na sayansi za jamii.

‘’Ushiriki wa tuzo hizi unaweza kuwa wa mtu binafsi au taasisi yaani mashirika ya uchapishaji, vituo vya utafiti, taasisi za tafsiri na idara za vyuo vikuu, tafsiri moja pekee itapokelwa kutoka kwa mtu binafsi na taasisi zitawasilisha hadi kazi tatu zilizofanywa na wafasiri tofauti na kazi itakayoingia katika kinyang’anyiro hicho lazima iwe imechapishwa miaka mitano kabla ya kutangazwa kwa tarehe ya tuzo.’’ Amesema.

Akieleza namna ya kushiriki katika tuzo hizo Bi. Consolatha amewataka washiriki kuingia katika tovuti ya www.hta.qa/en na kupakua fomu na kuijaza na kutuma nakala nne za makala lengwa (iliyotafsiriwa) ambazo hazitarejeshwa kupitia anwani ya Shekhe Hamad Award for Translation and International Understanding, P. O. BOX 1223 Doh. Qatar na kwa mawasiliano zaidi mshiriki anaweza kupiga simu namba +974 665 703 49.

Amesema, tuzo hizo zimelenga kuimarisha fani ya tafsiri na kujenga maarifa mapana ya mawanda ya kimataifa, kutambua na kuthamini mchango wa wafasiri na jukumu lao la kuunganisha watu wa mataifa mbalimbali kupitia tafsiri,  kuhimiza watu binafsi, wachapishaji, asasi na taasisi za Kiarabu  na kimataifa kuongeza jitihada zaidi katika tafsiri zenye ubora na ubunifu pamoja na kutambua mchango unaotolewa na watu binafsi na taasisi katika kusambaza utamaduni unaozingatia amani sambamba na kusheheneza utamaduni kupitia tafsiri za kibunifu.

 ‘’Dira ya tuzo hizi ni kutambua na  kazi nzuri na kubwa inayofanywa na wafasiri na kuthamini mchango wao katika kujenga na kuimarisha umoja wa undugu na ushirikiano miongoni mwa watu na mataifa mbalimbali ulimwenguni, kujenga heshima kwa tasnia ya tafsiri, kuhimiza ubunifu pamoja na kushirikisha masuala mtambuka ya kiutamaduni kati ya lugha ya Kiarabu na lugha nyingine duniani kupitia tafsiri.’’ Amesema.

 Vilevile amesema kuteuliwa kwa lugha ya Kiswahili katika tuzo hizo ni jambo linaloongezea fahari na faraja kwa kuwa tangu zianze kutolewa mwaka 2015, mwaka huu wameona wajumuishe lugha ya Kiswahili kutokana na namna lugha ya Kiswahili inavyocheza vizuri na kupokekelewa vizuri ulimwenguni.

Amesema vigezo vya jumla vya  ushiriki wa tuzo hizo ni pamoja na umahiri wa lugha za Kiswahili na kiarabu pamoja na  umuhimu wa kazi iliyotafsiriwa katika utamaduni wake wa asili kigezo chenye alama 30, usahihi na ufasaha wa kazi iliyotafsiriwa alama 40 na mtindo wa uelezaji wa  jambo kwa ufasaha na matumizi faafu ya sarufi na usomekaji chenye alama 30.

 Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2015 Doha, Qatar na kutangazwa mapema kila mwaka  zinasimamiwa na vyombo vitatu ambavyo ni bodi ya wadhamini, kamati ya usimamizi na jopo huru la majaji na mshindi atakayeibuka kidedea BAKITA itatoa tuzo kwa kuleta heshima katika Taifa.

No comments:

Post a Comment