Pages

Tuesday, May 3, 2022

OFISI YA RAIS-UTUMISHI KUTEKELEZA KWA WAKATI MAELEKEZO YA MHE. RAIS YA KUPANDISHA MISHAHARA YA WATUMISHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya kuwapandisha mishahara Watumishi wa Umma yaliyotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani 2022 yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

………………………………………………….

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amesema ofisi yake imejipanga kupandisha mishahara ya

Watumishi wa Umma kwa wakati kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani 2022 yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo ya kuwapandisha mishahara Watumishi wa Umma, Mhe. Jenista amesema ofisi yake itafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ifikapo Julai, 2022 kila mtumishi wa umma anapata mshahara mpya. Hivyo amewataka watumishi wa umma kuwa watulivu wakati zoezi hili likiendelea kushughulikiwa na Serikali.

“Mimi na watendaji wangu tumeanza kupitia taarifa za Watumishi katika Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara ili kushirikiana na Wizara ya Fedha katika kukamilisha zoezi la kupandisha mishahara ya Watumishi wa Umma, itakapofika Julai 2022 kila mtumishi atakuwa amepata mshahara mpya kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa ahadi ambazo Mhe. Rais amekuwa akizitoa kwa watumishi wa umma zimekuwa zikitekelezwa kwa wakati, hivyo jambo hili la mishahara litatekelezwa kama alivyokusudia.

Katika kuhakikisha mishahara ya watumishi wa umma inapanda kwa mujibu wa maelekezo ya Mhe. Rais, Waziri Jenista amewataka Maafisa Utumishi wote katika taasisi za umma nchini kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo kila mwongozo utakaotolewa na ofisi yake kwa lengo la kukamilisha zoezi la upandishaji wa mishahara ya watumishi.

“Maafisa Utumishi hakikisheni mnatekeleza maelekezo yatakayotolewa na ofisi yangu kwa uzalendo na uadilifu wa hali ya juu kwani atakayekwenda kinyume hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa kukiuka maelekezo halali ya Mhe. Rais,” Mhe. Jenista ameongeza.

Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo mengine aliyoyatoa Mhe. Rais likiwemo la watumishi walioondolewa kutokana na vyeti vya kughushi, Mhe. Jenista amesema wameshafanya mawasiliano na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu ili jambo hilo nalo lifanyiwe kazi ndani ya muda mfupi kwa mujibu wa maelekezo ya Mhe. Rais.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inasimamia na itaendelea kusimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma ili kuwajengea ari na morali ya utendaji kazi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment