Dar es Salaam. Jumatatu ya Aprili 18, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan aliandika
historia nchini Marekani baada ya kushiriki uzinduzi wa filamu ya The Royal Tour. Ni filamu iliyoibua matumaini ya kuleta mageuzi makubwa katika ukuaji wa sekta ya utalii na shughuli nyingine za kibiashara nchini ikiwemo uwekezaji. Uzinduzi wa filamu hiyo aliyotayarishwa na Peter Greenberg kwa maudhui ya kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji wa Tanzania, utafanyika tena leo Aprili 21, 2022 jijini Los Angeles, Marekani kabla ya Aprili 28 jijini Arusha na Mei 7, 2022 kule Zanzibar huku Greenberg akiahidi kutazamwa katika mataifa yote duniani ikiwa na tafsiri ya maandishi ya Kiswahili.
Hata hivyo, wakati uzinduzi ukiendelea, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela anaeleza namna benki hiyo ilivyoanza kunufaika na muhimu wa filamu hiyo katika biashara kimataifa.
Nsekela ambaye ni miongoni mwa waliomsindikiza Rais Samia katika uzinduzi huo, anasema filamu hiyo itachochea ongezeko la watalii na uwekezaji nchini, pia mtandao wa kitaifa na kimataifa katika mchango wa ukuaji wa uchumi kama ilivyotolewa wakati akipigia chapuo vivutio vya utalii nchini.
“Tunategemea filamu hii itachochea malengo ya kuitangaza Tanzania iwe kinara wa vivutio vya watalii duniani, hatua itakayowavutia watalii wengi kuja nchini, pia itachochea ukuaji wa shughuli za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine yatakayokuja kuwekeza nchini,” anasema Nsekela.
Wakiwa kwenye Royal Tour, ujumbe wa CRDB ulikutana na mtendaji mkuu kutoka Citibank na Pegasus, ambapo walijadili masuala ya biashara ambayo yanaweza kuwanufaisha Tanzania na Watanzania kwa ujumla.
Ujumbe wa Benki ya CRDB pia uliitembelea Moody's na kufanya majadiliano ya hali ya juu kulingana na msimamo wa soko, ikijumuisha kuwajengea uwezo, kupata taarifa na ufuatiliaji wa viwango vya mikopo.
Mkutano na watendaji wakuu wa Citibank ulijadili vipaumbele muhimu vya kukuza na kusaidia uwezeshaji wa kiuchumi katika biashara ndogo na za kati, ikilenga wanawake na vijana, uwekaji digitali na ajenda ya uchumi wa Buluu.
Pia wamejadili msaada wa kiufundi kwa benki ya CRDB ili kuimarisha uwezo wake katika kuhudumia na kukidhi mahitaji yanayokuwa kwa kasi. Citibank kuwa benki mshirika wa CRDB katika biashara ya sarafu ya dola za Kimarekani.
Katika kikao na watendaji kutoka Pegasus, ambayo imewekeza kwenye shughuli endelevu na zenye manufaa katika utatuzi wa sekta ya biashara walieleza nia ya kuingia katika soko la Tanzania huku wakionyesha dhamira ya kushirikiana na CRDB.
Wazo la filamu
Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania zinaonyesha katika kipindi cha mwaka unaoishia Februari 2022, mapato ya fedha za kigeni sekta ya utalii yaliongezeka hadi dola 1.457 bilioni kutoka dola 645.4 milioni katika kipindi kama hicho mwaka jana ikiwa ni juhudi za kuponya majeraha ya ugonjwa wa Uviko 19.
Ongezeko hilo lilitokana na ongezeko la asilimia 87.9 ya watalii waliowezesha kufikia 958,173 katika mwaka unaoishia Februari 2022.
Nsekela anasema wazo la Greenberg, limeonekana kubeba ujumbe unaoelewesha ulimwengu kuhusu maliasili nyingi za Tanzania, ikiwa ni pamoja na maeneo yake ya kitamaduni na urithi wa asili.
"Tuna madini pekee ya Tanzanite, tuna hifadhi kubwa ya gesi asilia, makaa ya mawe, mito, maziwa, bahari na mapori ya akiba. tuna zaidi ya makabila 100 yanayoishi kwa amani, tuna utamaduni tajiri na mila, vyakula asilia, historia na mavazi yetu. Haya yote yanaunda fursa ya kiuchumi kutumika," anasema.
No comments:
Post a Comment