Nairobi. Rais Uhuru Kenyatta, amewataka Wakenya wampigie makofi kwa
kuwaletea suluhu ya bima ya afya, kuongeza mishahara kisha wawapigie kelele wanaotaka kumrithi.Uhuru pia amewaambia wananchi kuwa Kenya inahitaji mtatuzi wa changamoto zinazowakabili, sio mzungumzaji tu.
Japokuwa hakutaja jina la mtu, hoja za Uhuru zinamgusa Naibu Rais, William Ruto kwa kauliyake kwamba “kazi uliyonayo sasa hauifanyi, imekushinda, unatoka kwenda kuongea matatizo. Ukishasema matatizo wananchi wanakuuliza sasa nini? Wananchi wa Kenya wanataka mtu atakayetatua changamoto zao.”
Maneno ya Uhuru ni dongo kwa Ruto kwa sababu mara kwa mara Uhuru amekuwa akirudia kusema kazi alipewa Ruto kuwa naibu Rais imemshinda na kwenda barabarani kulalamika.
Kauli ya Uhuru inazidi kujenga tafsiri ya wengi kwamba anajipa hadhi ya kuwa mwandaa marais (kings maker). Kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 9, ameamua kusimama na Raila Odinga.
Uhuru hafungamani na Ruto ambaye walikuwa wamoja kwenye uchaguzi wa mwaka 2013 uliowaingiza Ikulu halafu wakashitakiwa pamoja katika mahakama y akimataifa ya The Hague kwa kuchochea vurugu kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007.
Rais Uhuru amekuwa akisisitiza kuwa Wakenya wanapaswa kumshitukia Ruto na kujiweka kando naye kwa kuwa hana uwezo wa kushughulikia matatizo yao bali ni mlalamikaji kama wengine tu.
Uhuru anaamini Kenya itakuwa salama chini ya Raila aliyetimiza miaka 77 Januari 7 mwaka huu.
Mwaka 2013, ushirikiano wa Uhuru na Ruto ulioitwa Uhuruto ulisisitiza kuwa ilikuwa zamu ya vijana kuongoza kwamba wazee na mawazo yao yamepitwa na wakati.
Wakati huo, Uhuru alikuwa na umri wa miaka 51 na Ruto 47. Vijana wengi waliwaelewa. Uhuru na Ruto walipendeza hata walivyovaa mbele ya uso wa jamii. Ghafla, Uhuru kabadilika, anawaambia Wakenya Raila ndiye anayefaa leo.
Uhuru amekuwa akimsifu Raila kwamba ana busara kwa umri wake hivyo atakuwa Rais mzuri huku akimsema Ruto kwamba hafai kuongoza nchi. “Hii kazi aliyonayo imemshinda, hiyo anayoiomba tuna uhakika kuwa haitomshinda?” amehoji Uhuru mara kadhaa.
Uhuru anawachezesha Wakenya. Raila alikuwa na umri wa miaka 68 mwaka 2013 lakini Uhuru akasimama na Ruto kuwaambia Wakenya mawazo yake yalikuwa yamechoka. Sasa, Raila mwenye miaka 77 eti ndiye mtu sahihi kwa Kenya.
Hata ushawishi wa Uhuru kwa viongozi wa Umoja wa Vyama vya OKA (One Kenya Alliance), ulijengwa na hoja kuwa Raila ndiye mtu sahihi kuwaongoza Wakenya.
Viongozi wa OKA ni Gideon Moi, Moses Wetang’ula, Musalia Mudavadi, Martha Karua na Kalonzo Musyoka. Tayari Gideon, Kalonzo na Martha walishajiunga kwenye timu ya Raila wakati Wetang’ula na Mudavadi wakienda kwa Ruto.
Raila anagombea kupitia Azimio la Umoja One Kenya, na anatarajiwa kulitangaza jina la mgombea mwenza kabla ya Aprili 28 katika kipindi ambacho nguvu ya Ruto inazidi kuwa tishio japo kura za maoni zinaonyesha Raila ana nafasi kubwa zaidi ya kushinda.
Hata hivyo, mpaka sasa hakuna mwenye uhakika wa kushinda zaidi ya asilimia 50 ya kura zote hivyo kukidhi masharti ya Katiba ya Kenya inayotaka Rais kuchaguliwa walau kwa kura zaidi ya asilimia 50. Kwa jinsi mchuano ulivyo mkali kati ya Raila na Ruto, ni vigumu kumtabiiria mtu kupata kura za kutosha kwa sasa.
Ruto na chama chake kipya cha United Democratic Alliance (UDA) amepata umaarufu wa ghafla nchini Kenya. Umaarufu wa UDA ni kielelezo cha nguvu nyingi za ushawishi alizonazo Ruto kwenye mbio hizo za urais. Ruto atagombea urais kupitia UDA.
Kulikuwa na dhana kuwa Ruto angewania urais kupitia ushirika wa Kenya Kwanza lakini mpaka Aprili 9, siku ya mwisho ya kusajili ushirika wa vyama kwa ajili ya uchaguzi, Kenya Kwanza haikuwa imesajiliwa.
Awali, UDA kilikuwa kikiitwa Party of Development and Reforms (PDR), kilichosajiliwa mwaka 2012. Mwaka 2020, PDR walifanya usajili mpya na kubadili jina kuwa UDA. Kuanzia Januari mwaka jana, UDA kilipata umaarufu baada ya kuanza kuhusishwa na Ruto kabla baadaye hajaweka wazi na kutwaa uongozi wa chama hicho.
Japo Ruto haonekani kuungwa mkono na wanasiasa wengi mashuhuri kama ilivyo kwa Raila, kitendo cha UDA kupata umaarufu mkubwa ghafla ni kipimo cha msuli wake kisiasa. UDA imepata bahati kama ACT-Wazalendo cha Tanzania kilipopata nguvu mwaka 2019 baada ya Hayati Seif Sharif Hamad kuhamia akiwa na kundi la wanachama kutokea CUF.
Kwa sasa, Ruto analipigia hesabu eneo la Mlima Kenya lenye kaunti 10 kati ya 47 za nchi hiyo likiwa na makabili makubwa.
No comments:
Post a Comment