Pages

Thursday, April 28, 2022

Bashungwa azindua usambazaji vifaa vya Tehama

bashungwaapic

By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa amesema ugawaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwa

vituo vya ualimu na shule teule utaongeza idadi ya walimu wanaopata mafunzo wakiwa kazini.

Bashungwa ameeleza hayo jana Jumatatu Aprili 25, 2022 wakati akizindua ugawaji na usambazaji wa vifaa hivyo vilivyogharimu Sh2.5bilioni, hafla hiyo iliyofanyika katika shule ya sekondari ya Benjamin Mkapa. Halfa hiyo iliyohudhuriwa na maofisa elimu wa mikoa na wilaya mbalimbali.

Akizindua mchakato huo, Bashungwa amesema uwekezaji huo utasaidia walimu kupata fursa ya kushiriki programu ya mafunzo ya ualimu kazini, kwa kutumia vituo hivyo, ukilinganisha na miaka ya nyuma, akisema awali walimu waliokuwa wakiteuliwa kwa ajili ya mafunzo walikuwa wachache.

Bashungwa amesema vifaa vitasambazwa na kupelekwa katika vituo vya ualimu 150 katika halmashauri 144 nchini. Amesema miongoni mwa vifaa hivyo ni pamoja na mashine za kudurufu 150 na kila kituo cha ualimu kitapata moja.

“Printer zipo 150 na kila kituo kitapata moja,  projector 150, kila kituo kitapata moja na kompyuta za mezani zipo 600 na kila kituo kitapata nne.Tunamshukuru Rais Samia Saluhu Hassan kwa kutupatia Sh2.5 bilioni za kununua vifaa hivi,” amesema Bashungwa.

“Utaratibu wa kutumia waliojifunza ili kuwafundisha wenzao waliobaki katika vituo vya kazi ni mzuri Lakini wale walimu waliopata mafunzo walikuwa hawafundishi wenzao walioko kwenye maeneo ya kazi.

“Lakini kwa kupeleka vituo kila halmashauri tutahakikisha kuna na ratiba ambayo haizuii mwalimu kufundisha lakini anapata fursa ya kwenda katika kituo kujengewa uwezo,” amesema Bashungwa.

Akizungumza kwa niaba ya maofisa elimu wa mikoa na wilaya waliohudhuria hafla hiyo, Germana Mng’ao alisema vifaa hivyo vitakwenda kugusa moja kwa moja  maeneo karibu na  walimu ili kuwa jengea uwezo na weledi wa  kufundisha kwa ufanisi.

“Sasa tutakuwa na sababu ya kuwauliza walimu wetu, kuhusu masuala mbalimbali yalipangwa ikiwemo mwanafunzi asifike darasa la pili kujua kusoma na kuandika.Tunakwenda kulifuta hilo kwa sababu walimu watakuwa na uwezo wa kupata mafunzo,” amesema Mng’ao.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nomba amesema, “kila uchwao sekta ya elimu tunashangilia mafanikio na leo tunagusa walimu kupitia vituo vya ualimu kupata vifaa vya Tehama vitakavyorahisisha ujifunzaji na ufundishaji”

Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rugwa amesema tukio hilo linagusa kiungo muhimu katika elimu ambalo ni walimu, huku akibainisha kuwa mkoa huo mbioni kujenga shule ya kisasa ya bweni itakayochukua wanafunzi 4,000 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

No comments:

Post a Comment