Pages

Friday, March 4, 2022

WAZIRI UMMY, WAKUU WA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA YA AFYA "ZAANIKA" MAFANIKIO LUKUKI

 
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita. Mkutano huo unafanyika katika Ofisi za Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).Machi 4, 2022. 










JAMHURI WA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA

 

Tanzania Coat of Arms 

TAARIFA YA MAFANIKIO YA WIZARA YA AFYA KATIKA KIPINDI CHA

MWAKA MMOJA WA UONGOZI WA AWAMU YA SITA CHINI YA RAIS

MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN (KUANZIA MACHI 2021, HADI FEBRUARI 2022).

 

1.0     UTANGULIZI

Wizara ya Afya ina jukumu la kuandaa Sera, Miongozo na Sheria mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya.  Utekelezaji wa majukumu hayo umejikita katika kufanikisha Dira na Dhamira ya

Wizara katika kumuhudumia Mtanzania.

 

Dira

Kuwa na Jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo binafisi na ya nchi. 

Dhamira

Kutoa huduma muhimu za afya zenye uwiano wa kijiografia, viwango vya ubora unaokubalika, gharama nafuu na zilizoendelevu. Kwa mujibu wa Hati Idhini iliyotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2021 wakati akiunda Serikali ya Awamu ya Sita, baadhi ya Majukumu ya Wizara Afya ni pamoja na yafuatayo: -

i. Kutunga Sera na kusimamia utekelezaji wake. ii. Kusimamia utoaji wa Huduma za Kinga na Tiba

iii. Kusimamia ubora wa dawa na vifaa tiba. iv. Kununua na kusambaza dawa na vifaa tiba

v.          Kukuza huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala

vi.        Kuratibu mashirika yasio ya Kiserikali yanayojihusisha na shughuli za Sekta ya

Afya vii.           Kuratibu mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na shughuli za Sekta ya Afya

viii.        Kusimamia Huduma za maabara za Afya

ix.           Kuratibu Tafiti za afya na lishe

 

 

2.0   UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika Sekta ya Afya katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuingia madarakani ambapo jumla ya shilingi bilioni 891.5 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Wizara ya Afya. Vilevile Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha za kutekeleza miradi ya Maendeleo chini ya sekta ya afya kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo Taarifa imeshawasilishwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI. Miradi ya maendeleo ya kipaumbele iliyotekelezwa moja kwa moja na Wizara ya Afya ni pamoja na;

 

1.    Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika

Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalumu na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo kiasi cha shilingi bilioni 90.4 zilitolewa. 

 

a.    Kuendeleza ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa 8 ya Njombe, Geita, Simiyu, Songwe, Katavi pamoja na kuendeleza ujenzi wa Hospitali mpya za Rufaa za Mikoa ya Mara, Singida, na Shinyanga kwa lengo la kusogeza huduma za rufaa karibu na wananchi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 29. 

b.    Ukarabati wa majengo ya kutolea huduma katika Hospitali 13 za Rufaa za Mikoa katika vyumba vya upasuaji, wodi za kulaza wagonjwa, Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na wodi za wazazi na watoto na kuwekewa vifaa vya kisasa vya upasuaji na maabara; Hospitali hizo ni; Mwananyamala (DSM), Iringa, Mawenzi (Kilimanjaro), Ligula (Mtwara), Bombo (Tanga), Manyara, Maweni (Kigoma), Mbeya, Sekou Toure (Mwanza), Songea (Ruvuma), Sumbawanga (Rukwa), Kitete (Tabora), na Tumbi (Kibaha Pwani). Utekelezaji wa miradi hii upo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa na jumla ya shilingi bilioni 13 zimetolewa.

c.    Kuendeleza ujenzi wa majengo muhimu ya kutolea huduma katika Hospitali za Rufaa za Kanda za Mtwara, Mbeya, Chato, KCMC and

Bugando ambapo shilingi bilioni 37.4 zimetolewa

d.    Ujenzi wa majengo ya kutolea huduma Hospitali ya Taifa ya Muhimbili shilingi bilioni 3.9; 

e.    Ujenzi wa majengo katika Hospitali Maalumu ikiwemo Hospitali ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Magonjwa ya Akili Mirembe na Hospitali ya Magonjwa Kibong’oto ambapo kiasi cha shilingi bilioni 7.1 kimetolewa

 

2.    Ukarabati wa majengo ya kufundishia katika Vyuo vya Afya - kiasi cha shilingi biloni 6.3 kimetolewa

3.    Ununuzi na usambazaji wa Dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa ajili ya Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Halmashauri na Hospitali zilizo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Wizara ya Afya jumla ya shilingi bilioni 333 zimetolewa. 

4.    Ununuzi na Usambazaji wa Chanjo za Watoto jumla ya shilingi bilioni 45.03 zimetolewa

5.    Kununua vifaa Tiba vya Uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya shilingi 34.7

a.    Kukamilisha kwa uwekaji wa mitambo ya kuzalisha hewa tiba katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 7 (Geita, Manyara, Dodoma, Dar es Salaam-Amana, Mtwara, Ruvuma-Songea, Mbeya). Mradi huo umegharimu jumla ya shilingi bilioni 8.7

b.    Kukamilisha ufungaji wa mtambo wa kisasa wa pili wa Cathlab na Carto 3 wenye thamani ya Shilingi bilioni 4.6 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Mtambo huu utatumika kufanya uchunguzi na kutibu magonjwa ya moyo katika ubora wa hali ya juu sana.

c.    Kukamilisha ufungaji wa mashine kwa ajili ya kupasua ubongo bila kufungua kichwa (Angio Suite iliyogharimu 7.9 bilioni) katika Hospitali ya Mifupa ya MOI ambapo Huduma zimeanza kutolewa.

d.    Kuendelea na maandalizi ya usimikaji wa Pet Scan katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inayogharimu shilingi bilioni 18 ambapo shilingi  bilioni 1.7 imetolewa kipindi cha awamu ya 6  

e.    Kununua Vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 12 chini ya Mradi wa ORIO (MRI, CT Scan, Fluoroscopy, Digital X-ray, ultrasound, mama na mtoto, upasuaji, utakatisaji, incinerator) ambavyo tayari vimeshasimikwa katika hospitali 11 hapa nchini ambazo ni; Hospitali ya Kanda Bugando, Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Kigoma (Maweni), Temeke, Mwanayamala, Kagera (Bukoba RRH), Mara RRH, Hospitali ya Wilaya Misungwi, Hospitali ya Wilaya Bukombe, na Hospitali ya Wilaya Chato.

 

6.    Kuimarisha huduma za upatikanaji wa Damu salama shilingi bilioni 6.2 zimetolewa. Fedha hizi zimetumika kujenga kituo cha damu salama kanda ya

Dodoma na vituo 5 vya Mikoa ya Tanga, Njombe, Rukwa, Manyara na Kigoma.

 

7.    Kugharamia posho za wanafunzi watarajali (Interns) 3,518 wa Udaktari, Udaktari wa Meno na Wataalamu wengine wa Afya ambapo jumla ya shilingi bilioni 49.9 zimetolewa. 

 

8.    Kulipia gharama za masomo kwa ajili ya Madaktari bingwa (Specialists) na Madaktari bingwa Bobezi (Super Specialists) ndani na nje ya nchi ambapo jumla ya shilingi billion 4.4

 

9.    Kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (ikiwemo ununuzi wa dawa ARVs, Dawa za Malaria na vitendanishi) ambapo kiasi cha shilingi bilioni 117 kimetolewa. Fedha hizi pia zimetumika kununua Kliniki tembezi tano (5) zenye x-ray pamoja na mashine za gene ambazo zinatoa huduma mkoba za uchunguzi na matibabu ya Kifua Kikuu ambapo kufikia mwezi Desemba, 2021 wananchi 14,000 wamepimwa na miongoni mwao, wamegundulika wagonjwa wa Kifua Kikuu 1,076 sawa na asilimia 7 na kuanzishiwa matibabu. Vilevile fedha hizi zimetumika kuimarisha utoaji wa huduma za afya hasa za Kifua Kikuu na Ukoma ambapo Serikali imenunua pikipiki 160  na kuzisambaza kwa Halmashauri mbalimbali.  

 

10. Kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19  ikiwemo kuimarisha huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum, huduma za maabara, ununuzi wa CT Scans (29), MRI (4), ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) 253, ununuzi wa magari  kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za afya 250 ngazi ya Wizara, mikoa na Halmashauri zote nchini, magari ya damu salama 8 na magari 30 ya kusambazia chanjo ambapo kiasi cha shilingi bilioni 204.4 imeshatolewa kati ya shilingi bilioni 263.

 

3.0                MATOKEO YALIYOPATIKANA 

 

A. Kuboreshwa kwa Miundombinu ya kutolea Huduma za Afya

 

1.    Kukamilika na kuanza kutoa huduma za awali katika Hospitali mbili za Rufaa za Kanda ambazo ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mtwara na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Chato.

 

2.    Kukamilika kwa baadhi ya majengo ya kutolea huduma na kuanza kutoa huduma kwa Hospitali 2 za Rufaa za Mikoa ambazo ni Songwe na Hospital ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere - Mara, ambapo kwa upande wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere huduma zilizoanza kutolewa ni pamoja na huduma za kuchuja damu (dialysis) ambapo wagonjwa 14 wanapatiwa huduma katika Hospitali na hivyo kuwapungua umbali wa kusafiri kwenda Dar es salaam au Bugando kwa ajili ya kupata huduma hii.

 

3.    Ukarabati wa majengo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 13 umewezesha kupatikana kwa huduma za kibingwa ambazo zilikuwa hazipatikani katika hospitali hizo. Huduma hizo ni pamoja na huduma za kuchuja damu, huduma za dharura, huduma za kibingwa za afya ya mama na mtoto na hivyo kuokoa maisha ya watanzania.

 

B. Kuimarika kwa Upatikanaji wa Huduma za Matibabu ya Ubingwa Bobezi (Super specialized) nchini

 

1.    Mwezi Novemba, 2021, Hospitali ya Taifa Muhimbili - Upanga kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili - Mloganzila ilianza kutoa huduma ya upandikizaji wa Uloto (bone marrow transplant) ambapo jumla ya wagonjwa kumi na moja (11) hadi sasa wamefanyiwa upandikizaji huo. Huduma hii ni mara ya kwanza kufanyika nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati. Huduma hii inafanyika kwa wastani wa shilingi milioni 70 kwa mgonjwa mmoja na kama angepelekwa nje ya nchi jumla ya shilingi milioni 250 zingetumika kwa kila mgonjwa.

 

2.    Katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu (angiosuite) ilikamilika na kuanza kufanya kazi ambapo wagonjwa 120 wenye matatizo ya uvimbe kwenye mishipa ya damu kichwani, mishipa ya damu iliyoingiliana kichwani na sehemu nyingine za mwili wameweza kuhudumiwa kwenye maabara hii. Gharama za matibabu haya hapa nchini ni milioni 10 hadi milioni 15 kwa mgonjwa mmoja na endapo mgonjwa huyu angetibiwa nje ya nchi zingetumika shilingi milioni 40 hadi milioni 60.

 

3.    Huduma ya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua (catheterization producer) imeanza kutolewa ambapo jumla ya wagonjwa 10 wamefanyiwa upasuaji huo kwa gharama ya shilingi milioni 8 kwa mgonjwa katika Taasisi ya MOI ukilinganisha na shilingi milioni 40 kwa mgonjwa kama itafanyika nje ya nchi.  

 

4.    Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeweza kufanya upasuaji mgumu wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Cathetarization procedure) kwa wagonjwa 1,456 ikilinganishwa na wagonjwa 882 mwaka 2020.

 

C.    Kuimarika upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa Tiba, vitendanishi katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya.

 

1.            Katika kipindi cha Machi, 2021 hadi Februari 2022 Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 333 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendenashi. Dawa hizi ni pamoja na ununuzi wa aina 290 wa dawa za kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambikiza.

 

2.            Serikali ya awamu ya sita baada ya kufanya upimaji wa upatikanaji wa dawa kwa kutumia aina 30 za dawa muhimu na hivyo kuonyesha kuwa upatikanaji wa dawa ni kwa zaidi ya asilimia 95. Hatahivyo kutokana na kuendelea kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kuhusu upatikanaji wa dawa muhimu, Serikali imeamua kupima upatikanaji wa dawa hizi kwa kuongeza aina ya dawa muhimu zinazotakiwa kupimwa kufikia aina 290 za dawa muhimu kutoka 30 za awali.  Upimaji huu wa aina 290 za dawa kwa sasa upatikanaji utatuwezesha kujua hali halisi ya upatikanaji wa dawa kwa wananchi. 

 

3.

Ujenzi wa viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba katika eneo la Idofi katika Halmashauri ya Makambako Mkoani Njombe umeendelewa kusimamiwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kupunguza ununuzi wa dawa kutoka nje ya nchi. Hatua hii itasaidia kuimarisha upatikanaji wa dawa kwa wakati na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kununulia dawa nje ya nchi na hivyo fedha itakayookolewa itaelekezwa katika kutatua kero nyingine za afya zinazowakabili wananchi.

 

D.   Kuimarika kwa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto. 

 

1.            Utoaji wa chanjo kwa Watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja ulikuwa asilimia 97 kwa kutumia kigezo cha PENTA-3 (kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda, homa ya ini na homa ya uti wa mgongo) hivyo kuvuka kiwango cha asilimia 90 kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ikilinganishwa na asilimia 95 iliyokuwa imefikiwa mwaka 2020.

 

2.            Asilimia 99.7 ya akinamama wajawazito walifanya mahudhurio manne au zaidi katika kipindi hiki ikilinganishwa na asilimia 85.1 katika kipindi kama hiki kwa mwaka 2020.

 

3.            Asilimia 81.5 ya wajawazito walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, ukilinganisha na asilimia 80 waliojifungulia vituo vya kutolea huduma kwa kipindi kama hiki kwa mwaka 2020.

 

E. Kuendelea kupunguza Idadi ya Wagonjwa na Vifo vinavyotokana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu (TB)

 

1.    Serikali ya Awamu ya Sita imehakikisha Watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (WAVIU) wanapata bure dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na vitendanishi kwa ajili ya vipimo vya VVU. Hivyo Serikali imewezesha upatikanaji wa bidhaa hizi kwa asilimia 100. Hadi kufikia Februari, 2022, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 1,700,000 wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ambapo, WAVIU milioni 1,491,147 sawa na asilimia 88 ya WAVIU wote walikuwa wanatambua hali zao za VVU ikilinganishwa asilimia 83 mwezi Machi 2020. Vilevile kati ya WAVIU Milioni 1,471,450 sawa na asilimia 99 ikilinganishwa na WAVIU asilimia 98.6 Machi 2021 wako katika tiba endelevu ya ARV na asilimia 95.8 walikuwa wamefubaza VVU ikilinganishwa na asilimia 94.8 Machi 2022. Hii imetokana na kwamba Tanzania imeendelea kujipima kwa malengo ya 95-95-95, ambapo asilimia 95 ya WAVIU wanatakiwa kujua hali zao za maambukizi, asilimia 95 ya wanaojua hali zao wawe wameanza dawa za kufubaza VVU na asilimia 95 ya walio kwenye dawa wawe wamefubaza VVU chini ya kopi 1000 ifikapo 2025.

 

2.    Idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na malaria imepungua kwa asilimia 25 kutoka wagonjwa milioni 5.9 mwaka 2020 hadi wagonjwa milioni 4.4 mwaka 2021. Vilevile Idadi ya vifo vitokanavyo na malaria vimepungua kwa asilimia 26 kutoka vifo 2,460 mwaka 2020 hadi vifo 1,811 mwaka 2021. 

 

3.    Katika kupunguza maambukizi ya Kifua Kikuu nchini, kwa kipindi cha mwaka 2021, wagonjwa 87,132 waligunduliwa kuwa na kifua kikuu ikilinganishwa na wagonjwa 85,597 waliogunduliwa na Kifua kikuu kwa mwaka 2020. Asilimia 95 ya wagonjwa walitibiwa na kupona na kuendelea na majukumu yao ya uzalishaji mali. 

 

 

F. Kudhibiti Ugonjwa wa UVIKO-19 

 

1. Kuanzisha rasmi utekelezaji wa Afua ya Chanjo ya UVIKO 19 na kuratibu upatikanaji wa chanjo hizo ambapo mpaka kufikia 28 Februari, 2022, jumla

ya dozi 9,845,774 zimepokelewa nchini, dozi 5,426,840 sawa na asilimia 55 zimesambazwa mikoani. Jumla ya watu waliopata dozi kamili ni 2,571,724 sawa na asilimia 4.5 ya Watanzania wote 57,637,628.  Aidha Serikali ya awamu ya 6 imewezesha Wizara kutumia rasilimali za mapambano dhidi ya UVIKO 19 kuboresha mifumo ya utoaji huduma za afya  nchini ikiwemo kujenga na kunua vifaatiba kwa ajili ya wagonjwa mahututi na wagonjwa wa dharura. 

            

G. Ajira kwa Watumishi na Udahili wa Wanafunzi

1.            Katika kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi sasa, jumla ya watumishi 758 (wakiwemo madaktari, wauguzi, wafamasia na wataalumu wa maabara) wa mikataba ya Kudumu waliajiriwa na Wizara ya Afya katika utumishi wa Umma na kupangiwa maeneo mbalimbali nchini. Aidha, jumla ya ajira za mikataba kwa watumishi wa Afya 639 kupitia miradi mbalimbali ya Serikali zilitolewa. 

 

2.            Kufuatia maboresho ya miundombinu ya Vyuo vya Afya nchini yamewezesha ongezeko la wanafunzi katika vyuo vya afya ambapo katika kipindi cha Machi 2021 hadi sasa, jumla ya wanafunzi 29,519 walidahiliwa katika vyuo vya mafunzo ya kati ikilinganishwa na wanafunzi 25,077 mwaka 2020. Aidha wanafunzi 24,254 walihitimu mwaka 2021 ikilinganishwa na wanafunzi 11,953 mwaka 2020

 

4.0       MWELEKEO WA SEKTA YA AFYA NCHINI

Kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo, Mpango Mkakati wa Sekya ya Afya, Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Serikali ya Awamu ya 6 itaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya Afya kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kwa wananchi hususani wa kipato cha chini, ikiwa ni pamoja na:-

1.    Kuhakikisha ubora wa huduma katika hospitali zetu kwa kuendelea kuboresha miundombinu, kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba sambamba na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinazingatia viwango vilivyowekwa

2.    Kuanzisha huduma za Bima ya Afya kwa wote ili kuwawezesha Watanzania wote kupata huduma za matibabu pasipo kuwa na hitaji la kuwa na fedha mfukoni

3.    Kuendeleza watumishi wa afya ikiwemo kutoa mafunzo kazini. 

4.    Kupanua huduma za kibingwa na ubingwa bobezi ili kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi pamoja na kufikia ngazi ya tiba utalii

5.    Kuimarisha huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum

6.    Kuimarisha huduma za maabara, mionzi na Tiba mtandao 

7.    Kuimarisha huduma za chanjo dhidi ya UVIKO-19 

8.    Kuimarisha elimu ya afya kwa umma ili kuwezesha wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza 

9.    Kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ikiwemo huduma za uzazi wa dharura katika vituo vya afya ya msingi 

10. Kufanya tafiti za kitaalam kuhusu magonjwa ya kuambukiza na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na tafiti za kuwajengea uwezo watoa huduma za afya. 5.0 SHUKRANI

Tunaishukuru serikali ya Awamu ya 6 chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya. Tunaahidi kuendelea kusimamia utekezaji wa majukumu yetu ya kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote. Kipekee tunapenda kuwashukuru Watumishi wa Afya katika ngazi zote kwa kuendelea kutekeleza wajibu wao katika kuwatumikia watanzania. Ninawaasa waendelee kuzingatia weledi, miiko na maadili ya utoaji huduma za afya. Vilevile tunapenda kuwashukuru wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali na Taasisi za dini kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali za kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya.  

 

KAZI IENDELEE – #AFYAKWANZA #JALI AFYA YAKO.

 

Imetolewa na;

 

Ummy Ally Mwalimu (Mb)

Waziri wa Afya 

4 Machi 2022

No comments:

Post a Comment