Prof. Kahyarara ameyasema hayo alipokutana na kuongea na wasambazaji wa bidhaa za vifaa vya ujenzi Dodoma, Februari 3, 2022 kuhusu sababu za upandishaji wa bei na kupokea maoni ya jinsi ya kukabiliana na suala hilo ili kukuza biashara na kuwalinda walaji na kutimiza lengo la Serikali katika kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya taifa na wananchi.
Aidha, Katibu Mkuu huyo, aliwashauri wafanyabiashara na wasambazaji hao kujiandaa na kufanya biashara kwa ushindani pamoja na kuchangamkia fursa za Mkataba wa Kuanzisha Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambao Tanzania imeridhia na kujiunga. Mkataba huo unalenga kuwezesha uwekezaji na ufanyaji biashara baina ya nchi na nchi katika soko lenye watu takribani bilioni 1.3 linalotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kibiashara na kijamii barani Afrika
Nao, Wasambazaji wa bidhaa za ujenzi hususan saruji, nondo na mabati jijini Dodoma, walipata fursa ya kutoa sababu zinazochangia kupanda kwa bei ya bidhaa hizo ikiwa ni pamoja na kununua bidhaa hizo kwa bei kubwa kutoka kwa wasambazaji wakubwa, gharama kubwa za usafirishaji wa bidhaa hizo kutoka viwandani hadi maeneo yao husika pamoja na kupanda kwa bei ya malighafi za kutengenezea mabati kutoka nje ya nchi, bei kubwa ya kusafirisha malighafi hizo kutoka nje ya nchi.
Aidha, wakitoa mapendekezo mbalimbali ya jinsi ya kukabiliana na upandaji wa bei za vifaa vya ujenzi, Wasambazaji hao waliishauri Serikali kuanzisha mfumo bei elekezi ya saruji kulingana na maeneo waliopo kijiografia pamoja na kuwashauri wamiliki wa viwanda kuboresha mfumo wa usambazaji wa bidhaa kwa kuruhusu kuwa na wasambazaji wa bidhaa zao wengi badala ya kuwa na wasambazaji wakubwa wachache.
Akipokea maoni na mapendekezo hayo, Prof. Kahyarara aliwapongeza wasambazaji hao kwa maoni na mapendekezo yao muhimu na kuahidi kuyafanyia kazi huku akiwashauri kipunguza bei za bidhaa za vifaa vya ujenzi kuwa katika hali halisi bila kuwaumiza walaji wa mwisho ili kujenga uchumi imara.
No comments:
Post a Comment