Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa pazia kuweka Jiwe la Msingi la Kiwanda cha Maji cha Watercom Kinyikani Mchangamdogo Pemba kushoto kwa Rais ni Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi na kulia kwa Rais ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe.Omar Said Shaban, hafla hiyo imefanyika katika kiwanda hicho ikiwa ni shamrashamra za kusherehekekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema dhamira ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la uwekezaji linaanza kufikiwa kwa kuwepo viwanda viwili vikubwa ndani ya mwaka mmoja wa Uongozi wake.
Alieleza kuwa amefarijika kuona wamejitokeza wawekezaji wa ndani kuwekeza Kisiwani humo na wananchi kuonesha utayari wao kwa kushirikiana na wawekezaji hao ili kuona wanapata maendeleo katika maeneo yao.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Januari 3,2022 huko katika kijiji cha Kinyikani Mchangamdogo, Wilaya ya Wete, wakati akihutubia wananchi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha maji safi cha Watercom(T) LTD, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar.
Amewataka wananchi wa maeneo hayo yaliojengwa kiwanda hicho kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wawekezaji wakati Viwanda hivyo vikianza uzalishaji kwani kufanya hivyo kutaendelea kumpa moyo na kuona kuwa amekuja kuwekeza sehemu sahihi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipiga makofi baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Kiwanda cha Maji cha Watercom Kinyikani Mchangamdogo Pemba (kushoto kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na (kulia kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shaban, hafla hiyo imefanyika katika kiwanda hicho ikiwa ni shamrashamra za kusherehekekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akihutubia baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Kiwanda cha Maji cha Watercom Kinyikani Mchangamdogo Pemba (kushoto kwa Rais) ni Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na (kulia kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe.Omar Said Shaban, hafla hiyo imefanyika katika kiwanda hicho ikiwa ni shamrashamra za kusherehekekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).
“Ni dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuona kuwa kisiwa cha Pemba kimekuwa eneo maalumu la uwekezaji na imepiga hatuwa katika maendeleo ya viwanda na kiuchumi kwa kuweka mikakati maalumu ambayo kila muwekezaji itamvutia na kuwa na hamu ya kuekeza katika kisiwa hichi,”alisema.
Alisema kuwa, Serikali pamoja na kuimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji imeweka vivutio maalumu ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji .
Rais Dkt.Mwinyi aliwatoa hofu wawekezaji kwamba Pemba iko salama na eneo zuri na linawavutia wawekezaji na anawahamasisha watu wenye nia ya uwekezaji kuelewa kwamba Pemba kuna fursa ya uwekezaji ambazo hazijafanyiwa kazi hususan katika uchumi wa Bahari.
Alisema kuwa, uchumi wa bahari ndio muelekeo na Sera ya Serikali ya awamu ya nane, ambapo kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar ni Uchumi wa Buluu kwa maendeleo endelevu..
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwakilishi wa Kampuni ya Watercom,Abubakary Ally akitoa maelezo ya ujenzi wa kiwanda cha Maji Safi cha Watercom,baada ya kuweka Jiwe la Msingi,ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na (kulia kwa Rais) Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shaban, hafla hiyi imefanyika katika eneo la kiwanda hicho Kijiji cha Kinyikani Mchangamdogo Mkoa wa Kaskazini Pemba.(Picha na Ikulu).
“Nawakaribisha wawekezaji wote kuekeza katika eneo hili ambalo linajumuisha miradi inayohusiana na utalii, uvuvi na mazao mengine ya baharini kama vile Mwani , bandari na shuhuli za mafuta na gesi asilia,”alieleza.
Alisema kuwa, Serikali imekwishaandaa na kuongeza jitihada za kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje na kuona namna bora za kuwaondolea urasimu na kuhakisha wanashuhulikiwa kwa haraka katika kuhakikisha wanakamilisha taratibu za uwekezaji kwamuda mfupi sana.
Alisema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeiimarisha Mamlaka ya ZIPA kwa kuanzisha kituo cha pamoja cha kutowa huduma (onestop center) kwa masuala yote muhimu yanayohitajika kwa muwekezaji ili kumuondolea usumbufu.
Wanafunzi wa Skuli ya Msingi Konde Pemba wakiimba wimbo wa ukombozi wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Kiwanda cha Maji Safi cha Watercom kinachojengwa katika kijiji cha Kinyikani Mchangamdogo Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Dkt.Mwinyi alieleza hatua hiyo itamuwezesha mwekezaji aliyekwisha kamilisha masharti kupata kibali cha uwekezaji sio zaidi ya siku tatu tu.
Alifurahi kusikia kwamba kiwanda hicho kitakapoanza uzalishaji kitachangia ajira zaidi ya 550 zitakazotokana na mnyororo wa thamani katika uzalishaji wa maji hatua ambayo itaendana na dhamira ya kutoa ajira laki tatu.
“Ni matumaini ya Serikali kuwa tunaweza kulifikia lengo hilo kwa kutokana na mipango mizuri tulioiandaa na ile tulioanza kuitekeleza ni wazi fursa hizo zitatoa mchango pia katika kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuchangia sana kunyanyuwa uchumi wa taifa kwa ujumla,”alieleza.
Aliwataka wananchi kuelewa kwamba sekta ya viwanda ni chachu ya mafanikio kwa maendeleo ya kiuchumi katika nchi mbali mbali duniani, kwani nchi nyingi zilizoendelea na zile zinazoendelea kwa kasi zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali katika kuhakisha zinawekeza kwenye sekta ya viwanda na hivyo Serikali imeamuwa kuweka maeneo maalumu ya viwanda yakiwemo maeneo ya Dunga na Nungwi kwa Unguja na Chamanangwe kwa upande wa Pemba.
Mwakilishi wa Jimbo la Kojani Pemba, Mhe. Hassan H.Omar, akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha maji cha Watercom kinachojengwa katika Kijiji cha Kinyikani Mchangamdogo Pemba, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Alisema, lengo la kuwepo maeneo hayo ni kuimarisha sekta ya viwanda ambayo itafunguwa fursa mbalimbali ikiwemo kupatikana ajira kwa wananchi, kuchangia pato la Taifa kupitia kodi na tozo mbali mbali , kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kutowa soko zuri la bidhaa za kilimo , uvuvi na ufugaji.
Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea na jitihada za kuleta maendeleo ya Viwanda nchini, ikiwemo kujenga kiwanda cha Mwani katika eneo la Chamanangwe ambapo tayari kupitia mfuko wa Uviko 19 imetenga jumla ya fedha TZS Bilioni 2.5 ambazo zitapatiwa mkopo Kampuni ya mwani Zanzibar ili kuhakikisha ujenzi wa kiwanda hicho inaanza na kukamilika ndani ya mwaka huu 2022.
Alieleza mara kiwanda hicho kitakapo kamilika na kuanza kazi kitatowa ufumbuzi wa changamoto wa bei ya mwani kuongeza thamani ya zao hilo na bidhaa zake na kila mwenye nia ya uwekezaji Serikali atawapatiwa kila aina ya msaada anaohitaji ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaimarika Zanzibar na mchango wa sekta ya Viwanda unaongezeka.
Viongozi na Wananchi Kisiwani Pemba wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akihutubia katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha maji cha Watercom kinachojengwa na muwekekezaji katika Kijiji cha Kinyikani Mchangamdogo Pemba, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).
Aliwataka vijana wa kisasa kutafsiri Mapinduzi ya mwaka 1964, kwa vitendo kwa kuchangamkia fursa za kiuchumi na kuleta maendeleo ya nchi yao.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliahidi kutekeleza ombi la wananchi wa eneo hilo la kutiliwa lami barabara yao inatoka Mzambauni kupitia Kinyikani hadi Mchangamdogo.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema uwepo wa viwanda vya vinywaji vitakuwa mkombozi mkubwa wa kisiwa cha Pemba na wananchi wake kwa kupata ajira.
“Maji ni muhimu sana mwekezaji vizuri kupeleka maji hayo nje ya Tanzania, kwa lengo la kuyatangaza maji ya Pemba katika baadhi ya nchi ikiwemo Kenya,”alisema.
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shaban akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmin Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi kuzungumza na Wananchi wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha maji safi cha Watercom Kinyikani Mchangamdogo Pemba.(Picha na Ikulu).
Aidha, alimshukuru mwekezaji huyo mzalendo kwa jihudi zake za kuekeza ndani ya kisiwa cha Pemba, kupitia vinywaji mbali mbali nchini, huku akimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwamba ndani ya uongozi wake tayari viwanda viwili vimeshajengwa ndani ya kisiwa hicho.
Aidha, alisema Wizara ya Biashara bado inaendelea kuwa na imani na uongozi wake wa awamu ya nane, katika mikakati ya kukitangaza kisiwa cha Pemba kuwa ni eneo la uwekezaji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema kumalizika kwa miradi hiyo itatoa faida kubwa kwa vijana wa Kisiwa cha Pemba, hususan wazawa na wataalamu kunufaika na ajira ya moja kwa moja na ile isiyo ya moja kwa moja.
Akitoa salamu za wananchi wa Jimbo la Kojani Mbunge wa Jimbo la Kojani, ambaye pia, ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad Hassan Chande alimshukuru mwenkezaji huyo kwa kuekeza kiwanda chake katika Jimbo la Kojani, kwani asilimia 75 ya ajira wanufaika wa kwanza ni wananchi wa Jimbo hilo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakimsikiliza Bi.Maryam Omar,akitowa matatizo ya maradhi ya Mtoto wake Aisha Ali Mussa (10) baada ya kumaliza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha maji katika kijiji cha kinyikani mchangamdogo Mkoa wa Kaskazini Pemba.(Picha na Ikulu).
Aidha, aliwataka wananchi kutambua kuwa tayari mwekezaji mwengine kutoka kampuni ya Alhasab yupo njiani kuekeza katika meneo hayo, kujenga kiwanda cha Juisi kitakachotoa fursa kwa wananchi kuuza bidhaa zao moja kwa moja katika kiwanda hicho zikiwemo embe.
Mwakilishi wa Jimbo la Kojani Hassan Hamad Omar, alisema wananchi wa Jimbo la Kojani na Pemba nzima, bado wanaendelea kuwa na imani na Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi, kutokana na mikakati mbali mbali aliyoiweka ikiwemo katika eneo la uwekezaji na uchumi wa buluu.
Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Dk. Islam Seif Salim alisema mradi huo wa kiwanda cha maji ulianza Oktoba 2 mwaka 2021, kufuatia maelekezo yake na Mamlaka ya ZIPA kuhamasika kuhimiza wawekezaji na kuondosha urasimu katika eneo la kimkakati la kisiwa cha Pemba.
Alifahamisha kuwa mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu TZS Bilioni 1.2, kiwanda kikijumuisha maeneo mbali mbali pamoja na kisima cha kuzalisha lita 30 elfu za maji kwa saa, huku kikitarajiwa kuanza kuzalisha maji mnamo mwezi Machi, 2022.
Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akimsalimia mtoto Aisha Ali Mussa akiwa na Mama yake Bi.Maryam Omar, baada ya kupata matatizo yanayomsumbua mtoto na (kulia )Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Mhe.Salama Mbarouk.(Picha na Ikulu).
Katibu huyo alisema uwezo wa kiwanda ni kuzalisha maji lita 72 elfu kwa saa 12 au lita laki moja na 44 kwa siku, huku bidhaa zitakazozalishwa ni maji, soda, ice cream na kuuzwa katika masoko mbalimbali ya Tanzania Bara na nje ya Tanzania.
Alisema sekta ya Viwanda imekua ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa nchi nyingi duniani, Zanzibar uwepo wa vianda vya kati vinaweza kutoa ajira kwa wasiopungua 230 na viwanda vikubwa vimeweza kutoa ajira 10417 2019 hadi 11601 2020.
Naye mwakilishi kutoka kampuni ya Watercom (T), Aboubakar Ali Faraji, alisema uwepo wakiwanda hicho ni kuunga mkono Uchumi wa buluu na juhudi katika kukipa kisiwa cha Pemba maendeleo.
Alisema kukamilika kwake kitatoa ajira za moja kwa moja 50 na zisizo za moja kwa moja 500, na kuzalisha maji 72000 kwa saa.
Katika hafla hiyo burudani mbalimbali zilitumbuiza ikiwa ni pamoja na burudani ya vijana kutoka Micheweni.
No comments:
Post a Comment