Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
yaani 2021/22 - 2025/26 ambao utagharimu kiasi cha Sh Trilioni 114.8 am ambapo Sh Trilioni 74.2 zitatokana na Fedha za Umma na Sh Trilioni 40.6 zikichangiwa na sekta binafsi.Mpango huo umezinduliwa leo jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Spika wa Bunge, Job Ndugai, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Mikoa nchini.
Akizungumza wakati wa kuzindua Mpango huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema fedha hizo zinajumuisha mikopo na misaada ya wabia wa maendeleo na kuwahakikishia watanzania kuwa fedha hizo zitapatikana na malengo yaliyowekwa yatatekelezwa.
Amesema kupitia mpango huo, Serikali ina lengo la kuinua uchumi kutoka kuwa Taifa lenye uchumi wa kati wa chini hadi kuwa Nchi yenye uchumi wa kati uliokomaa na kwamba wamejipanga kujenga uchumi shindani kwa ajili ya maendeleo ya watu na Nchi.
" Mpango huu tunaouzindua leo una nia ya kuimarisha uchumi wetu na kuufanya uwe uchumi wenye ushindani unaotokana na viwanda kwa maendeleo ya watu na umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi.
Tumepanga kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu, na kuendeleza rasilimali watu," Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Katika kutimiza malengo ya mpango huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali haitomfumbia macho mtu yeyote ambaye atajaribu kukwepa Kodi, uzembe makazini, matumizi mabaya ya fedha na ulaji rushwa huku akiahidi kuwa watapokea maoni yenye lengo la kuboresha Mpango huo.
Amesema kupitia mpango huo pia wataendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ilishaanzishwa ikiwemo miradi ya Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Ujenzi wa Bomba la mafuta, Ujenzi wa bandari mbalimbali na ununuzi wa meli.
“ Nitoe wito kwa Wizara ya Fedha na Mipango kuendelea na utaratibu wa kutoa elimu ya kutosha ili kumwezesha kila mmoja kushiriki kikamilifu katika utekelezaji. Aidha, ninaagiza Wizara, Taasisi za Umma, Idara Zinazojitegemea Wakala za Serikali, Sekta Binafsi na Wadau wote wa maendeleo kuhakikisha ofisi zao zina nakala ya Mpango huu na kuanza kuutekeleza," Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Awali akizungumzia mpango huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mpango huo uliozinduliwa leo ni muendelezo wa utaratibu wa Serikali kuimarisha rasilimali zake mbalimbali za ndani na uimarishaji wa Mipango yake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuimarisha upangaji mipango na kusimamia rasilimali za ndani ya nchi ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, ardhi, fedha na rasilimali watu kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.
" Mhe Waziri Mkuu katika kuhakikisha tunatekekeza Mpango huu kwa ubora na kufikia malengo tumeandaa muongozo wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo," Amesema Tutuba.
No comments:
Post a Comment