Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB akionyesha bango
linaloonyesha zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwa washindi wa CRDB Bank
Marathon 2021. Wengine pichani ni Mkurugenzi
wa Uendeshaji wa EFM, Denis Busulwa (kulia), Meneja Masoko wa Strategis, Lilian
Malakasuka (wapili kulia) na Mkuu wa Kitengo cha BancAssurance Alliance General,
Osward Tellis.
======= ====== ========
Dar es Salaam 29 Juni, 2021 – Benki ya CRDB imetangaza zawadi za washindi wa msimu wa pili wa
CRDB Bank Marathon 2021 ambapo jumla ya shilingi milioni 45.4 zitatolewa kwa
washindi 32. Akitangaza zawadi hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya
CRDB, Tully Mwambapa alisema kwa mwaka huu zawadi zimeongezwa ili kuendana na
hadhi ya kimataifa ambayo CRDB Bank Marathon ilipewa mwaka huu baada ya
kusajiliwa na Chama cha
Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AMIS) kwa kushirikiana na Shirikisho
la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics).
“Mwaka huu sio marathon tu
ni ya kimataifa, hata zawadi pia ni za kimataifa zaidi. Tumejipanga kutoa
zawadi nono kwa washindi, kwa mbio kubwa za kilometa 42 mshindi wa kwanza
atapata shilingi milioni 5, mshindi wa pili shilingi milioni 3, mshindi wa tatu
shilingi mili 2 na mshindi wa nne shilingi milioni 1. Hizi ni zawadi kubwa
zaidi kupata kutokea katika mbio zote nchini,” alisema Tully huku akibainisha kuwa
wingi wa zawadi unatokana na kuongezeka kwa namba ya washiriki ambapo ambapo
matarajio ni kupata washiriki 5,000 kutoka ndani nan je ya nchi.
Tully aliwataka Watanzania
kujitokeze kwa wingi kujisajili katika mbio hizo za CRDB Bank Marathon kwani
pamoja na kuwa mbio hizo sasa hivi ni za kimataifa lengo kubwa ni kukuza
uzalendo miongoni mwa Watanzania kwa kuwaleta pamoja kutatua changamoto katika
jamii. “Wakimbiaji wengi wa kimataifa wanajisajili ma mia kwa mamia kuja
kushiriki kusambaza tabasamu nchini kwetu, lakini tungependa zaidi kuona
Watanzania wakishiriki kwa wingi kwani hii ni marathon yetu na tungependa pia
kuona zawadi hizi zikibaki nyumbani,” aliongezea.
Akizungumzia fursa
zitokanazo na mbio hizo ambazo sasa hivi zimesajiliwa kimataifa, Tully alisema
mbio hizo zitakwenda kuchochea uchumi wa Jiji la Dar es Salaam na kulitangaza
jiji hilo pamoja na Tanzania kwa ujumla duniani kote. Alisema mbio hizo
zitatumika kutangaza vivutio na historia ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo
utamaduni wa pwani (swahili culture). “ Pamoja na hivyo mbio hizi pia zitasaidia
kuonyesha vipaji vya wakimbiaji duniani kwani mbio hizi zitaonyeshwa live na TVE
ambayo ipo DSTV. Tunakwenda kufunguka zaidi kwenye anga za dunia,” alisisitiza
Tully.
Akikumbushia lengo la
kuandaa marathon hiyo, Tully alisema mbio hizo zinalenga kuwaleta pamoja
Watanzania kuchangia watu wenye uhitaji katika jamii pamoja na kutatua
changamoto nyengine zinazoikabili jamii. Alisema mwaka huu lengo ni kukusanya
shilingi milioni 500 ambazo zitaelekezwa katika kusaidia watoto wenye uhitaji
wa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ujenzi wa
kituo cha mawasiliano “Call Center” katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road na
kampeni ya utunzaji mazingira ya “Pendezesha Tanzania” ambapo miti milioni 1
inatarajiwa kupandwa ndani ya miaka 3.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa
EFM na TVE, Denis Busulwa (Ssebo) alisema kampuni yao inajivunia kuwa washirika
wa CRDB Bank Marathon kutokana na mbio hizo kujikita zaidi katika kuhamasisha
watu kusaidia jamii. “Tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kuandaa mbio hizi
zinazowaleta Watanzania kushiriki katika kutatua changamoto katika jamii. EFM
na TVE ni vyombo vya habari vya jamii hivyo tunakila sababu ya sisi kushiriki
katika mbio hizi ikiwa ni sehemu yetu ya kusaidia jamii,” alisema Ssebo huku
akihamasisha Watanzania kujisajili kwa wingi.
Naye Katibu Mkuu wa
Shirikikisho Riadha Tanzania, Jackson Ndaweka aliipongeza Benki ya CRDB kwa
kuandaa mbio hizo kwa viwango vya kimataifa huku akimhakikishia Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa kuwa zawadi zote zitabaki nchini
kwani wanariadha sasa hivi wanajifua kuelekea tarehe 15 Agosti 2021 siku ya
marathon. “Wanariadha wetu wana kiu kubwa ya kushindana baada ya mbio nyingi za
kimataifa kuahirishwa kutokana na changamoto ya COVID-19. Zawadi hizi zimekuja
wakati muafaka na wanariadha wetu wapo wanajifua kuchuana na wanariadha wa
kimataifa,” alisema Ndaweka.
Hafla hiyo ya kutangaza
zawadi ilihudhuriwa washirika mbalimbali wa CRDB Bank Marathon ikiwamo kampuni
za bima za Sanlam, Alliance (Life na General), Heritage, Mayfair na Britam,
pamoja na viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Chama cha Baiskeli
Tanzania (CHABATA) na klabu za riadha Dar es Salaam. Viongozi hao walipongeza
juhudi zinazofanywa na Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Marathon na kuahidi
kuendelea kushirikiki katika mbio hizo.
Kujisali na kuchangia katika CRDB Bank
Marathon washiriki wanatakiwa kutembelea katika tovuti rasmi yam bio hizo www.crdbbankmarathon.co.tz ambapo
mtu binafsi anatakiwa kuchangia shilingi 30,000 na washiriki kupitia vikundi ni
shilingi 25,000. Malipo yanaweza kufanyika kupitia matawi ya Benki ya CRDB,
CRDB Wakala, SimBanking App, mitandao ya simu na kupitia kadi ambazo
zinawawezesha hadi watu wa nje ya nchi kufanya malipo.
No comments:
Post a Comment