Wataalam wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Shifa ya nchini Misri wakimtibu mgonjwa mwenye matatizo ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo ambaye mapigo yake ya moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida (Tachyarrhythmia’s) wakati wa kambi maalum ya siku tatu ya matibabu hayo iliyofanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 10 walitibiwa katika kambi hiyo.
Wataalam wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya siku tatu ya matibabu hayo iliyofanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo.
Picha na JKCI
************************
Na Salome Majaliwa – JKCI
30/06/2021 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imechaguliwa kuwa kituo cha mafunzo cha
magonjwa ya moyo katika mfumo wa umeme wa moyo kwa wataalamu wa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la SaharaMafunzo hayo yatakuwa yakitolewa kwa njia ya mtandao na wataalamu wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa magonjwa ya moyo Dkt. Tatizo Waane alisema mafunzo hayo yatakuwa yakitolewa wakati wa kambi maalum za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo zitakazokuwa zinafanyika katika Taasisi hiyo.
Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo alisema katika kambi hizo maalum za matibabu licha ya kutibu, wataalamu wanabadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa wenye tatizo hilo la moyo unaokwenda kwa haraka.
“Katika kambi hizi huwa mafunzo yanafanyika kwa wataalamu waliopo katika Taasisi yetu pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) ambao wanapenda kujifunza matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo. Katika kambi zijazo mafunzo yatakuwa yanatolewa kwa njia ya mtandao ambapo wataalamu kutoka nchi mbalimbali watashiriki”, alisema Dkt. Waane.
Akizungumzia kuhusu kambi maalum ya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo iliyomalizika hivi karibuni Dkt. Waane alisema walifanya matibabu kwa wagonjwa 10 ambao wawili kati yao walitoka nchini Burundi wote wanaendelea vizuri na wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Dkt. Waane alifafanua, “Matibabu haya yamefanyika katika mtambo wa Carto 3 System 3D & mapping electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao ulizinduliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katikati ya mwezi wa sita mwaka huu ambapo hadi sasa jumla ya wagonjwa 194 wamepata matibabu”,.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo Prof. Mervat Aboulmaaty kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri alisema mtambo huo wa kisasa na wenye teknlologia ya hali ya juu licha ya kutumika katika kuokoa maisha ya watu wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo pia unasaidia kutoa elimu kwa wataalamu.
“Mimi pamoja na wataalamu wenzangu kutoka nchini Misri kazi yetu ni kutoa huduma ya kufanya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo na kuokoa maisha ya watu katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara”,alisema Prof.Mervat.
Aliongeza kuwa kupitia chuo kikuu cha Ain Shams cha nchini Misri wanatoa elimu kwa njia ya mtandao kuhusu matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo ambapo madaktari wengi wa Afrika wakiwemo wa Tanzania wamekuwa wakishiriki.
Naye Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo ambaye ndiye msimamizi wa kambi hiyo Yona Gandye alisema wameweza kutoa matibabu kwa mgonjwa ambaye alikuwa na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo ambapo moyo wake ulikuwa ukijaribu kufua umeme inashindikana katika hali ya kawaida na kuwa katika mtiririko wa hali ya juu (Atrial fibrillation), hali hii ikitokea mgonjwa anakuwa katika uhatarishi wa damu kuganda na kupelekea kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi.
“Matibabu haya yametolewa kwa mara ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki na nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ingawa mtambo kama huu umefungwa nchini Kenya lakini matibabu kama haya hayajawahi kutolewa”, alisema Dkt. Gandye ambaye pia ni mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo.
Alisema katika kambi ijayo ambayo itafanyika baada ya miezi miwili kutakuwa na mafunzo kwa njia ya mtandao ambayo yataunganishwa na hospitali ambazo hazijaanza kutoa huduma ya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo ili madaktari waweze kupenda kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa ambayo itawasaidia kutokusafiri nchi za mbali kwenda kutafuta matibabu ya aina hiyo.
No comments:
Post a Comment