Pages

Thursday, April 1, 2021

BRAC yatoa elimu ya fedha kwa wanafunzi kuadhimisha wiki ya fedha

Meneja Mafunzo kutoka Shirika  la BRAC Tanzania Naamala Samson akitoa mafunzo ya uhifadhi wa fedha na matumizi wanafunzi wa Darasa la sita na saba wa Shule ya Msingi Mapambano wakati wa maadhimisho ya Wiki ya fedha Duniani

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapambano wakichangia jambo baada ya kupata elimu ya uhifadhi wa fedha kutoka kwa Shirika la BRAC Tanzania katika wiki ya Fedha duniani.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapambano waakiwa katika picha ya pamoja

 Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv


Shirika la BRAC Tanzania limeshiriki  maadhimisho ya wiki ya fedha duniani kwa   kutoa elimu ya fedha kwa

wanafunzi wa Shule ya Msingi Mapambano iliyopo Sinza Jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwana yanajulikana kama Global Money  Week (GMW) yamejikita katika kutoa elimu Kwa vijana na watoto kupitia dhima ya '' Kujifunza, Kuweka akiba na Kuongeza kipato.

Akizungumza na wanafunzi hao wakati wa utoaji elimu hiyo, Meneja Mafunzo kutoka BRAC Naamala Samson amesema elimu wanayoitoa hapo ni kuhakikisha watoto na vijana wanajifunza kutumia pesa kwa busara, kuweka akiba kwa maisha yao ya baadae na pia kujenga uwezo wa kupata na kuongeza kipato kwa ajili yao na familia zao.

Vile vile Samson amesema, wiki  ya fedha kwa mwaka huu imeadhimishwa na na kauli mbiu ya 'Jitunze, jali pesa zako' ikiashiria umuhimu wa kujenga uimara wa kifedha na pia kujenga afya hasa katika muktadha wa sasa ambao ulimwengu mzima unapambana na changamoto ya ugonjwa wa virusi vya korona.

Amesema, BRAC Tanzania kama shirika linalojihusisha na masuala ya fedha likiwa na lengo la kupunguza umasikini nchini kupitia huduma za mikopo kwa wajasiriamali, hushiriki katika maadhimisho haya ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanakua wakiwa na elimu husika ya masuala ya pesa ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

"Sehemu ya dhamira ya BRAC ni kutoa elimu ya kifedha kwa wateja wake. Shirika linaamini kuwa kwa kushiriki katika harakati hii ya kuwafundisha watoto na vijana juu ya fedha, litakuwa linatengeneza kizazi ambacho kitakuwa na maarifa zaidi ya masuala ya kifedha ambacho kitawawezesha kufanya maamuzi bora ya pesa watakapokuja kuwa wajasiriamali," amesema.

Samson amesema kwa Mwaka huu, pamoja na kutembelea shule ya Msingi ya Mapambano na kutoa elimu ya fedha kwa wanafunzi wa darasa la sita na la saba, pia shirika limefanya kampeni ndogo ya elimu ya fedha kupitia mitandao yake ya kijamii na imetembelea klabu ya uwezeshaji kwa wasichana ya mradi wa ELA iliyopo Temeke na kutoa elimu ya fedha.

Global Money Week (GMW) ni kampeni ya kila mwaka ya kukuza uelewa juu ya umuhimu wa kuhakikisha kuwa vijana, tangu umri mdogo, wanaelewa masuala ya kifedha, na kuendelea kupata maarifa, ujuzi, mitazamo na tabia ambazo zitahitajika katika kufanya maamuzi mazuri ya kifedha na hapo baadaye kuweza kuwa na ujasiri wa kifedha.

No comments:

Post a Comment