Mmiliki
wa Blog ya 8020 Fashion, Shamimu Mwasha akitoka katika chumba cha
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mara baada
ya kuhukumiwa kifungo cha misha Jela leo Machi 31.
Mfanyabiashara
Abdul Nsembo (45) akiwa katika Mahabusu ya Mahakama Kuu Divisheni ya
Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama mahakama ya mafisadi leo
mara baada ya Kuhukumiwa Kifungo cha Maisha jela.
Gari
aina ya Land Rover Discover, T 817 DQN walilokutwa nalo washtakiwa na
Shamimu na Mumewe limeamuliwa litaifishwe na kuwa mali ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
MAHAKAMA
Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama
mahakama ya mafisadi, imemuhukumu Shamim Mwasha (41), na mume wake,
Abdul Nsembo (45), kutumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya
kupatikana na hatia ya kusafirisha na kujihusisha na biashara ya dawa za
kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 232.70.
Aidha,
Mahakama hiyo imeamuru kutaifishwa kwa gari aina ya Land Rover
Discover, T 817 DQN kuwa mali ya serikali na pia dawa za kulevya
walizokutwa nazo Mwasha na Nsembo kuteketezwa.
Hukumu
hiyo imesomwa leo Machi 31, 2021 na Jaji Elinaza Luvanda baada ya
kuridhika na ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashtaka walioweza
kuthibitisha pasipo kuacha shaka Shamimu na mume wake walitenda makosa
hayo.
Akisoma
hukumu hiyo Jaji Luvanda amesema, amepitia ushahidi wote wa upande wa
mashtaka na ule wa utetezi pamoja na hoja mbalimbali zilizowasilishwa na
imeonyesha kuwa, hakuna shaka kuwa vielelezo vyote vilikutwa nyumbani
kwa washtakiwa hivyo washtakiwa wote mmekutwa na hatia, mahakama
inawatia hatiani.
Hata
hivyo kabla ya kuwasomea adhabu, Jaji Luvanda aliuliza upande wa
mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema waliomba mahakama itoe adhabu
kali kulingana na sheria inavyoagiza kwa sababu kosa walilofanya
washtakiwa hao linaleta madhara makubwa kwa jamii ikiwemo utegemezi na
upungufu wa afya ya akili.
Katika
utetezi wao, washtakiwa kupitia mawakili wao, Juma Nassoro na Hajra
Mungula waliomba mahakama kuwapunguzia wateja wao adhabu kwani ni
wakosaji wa kwanza na pia ni wanandoa, ni wazazi wa watoto watatu
wanaohitaji malezi ya wazazi hivyo mahakama itoe hukumu kwa kuangalia
huruma hiyo.
Hata
hivyo Jaji Luvanda amesema anatoa hukumu kulingana na matakwa ya
sheria, na kwamba kifungu cha sheria cha 15 (1)a cha sheria ya kudhibiti
na kupambana na dawa za kulevya sura ya 95 walichoshtakiwa nacho
washtakiwa hakitoi mwanya wa kutoa adhabu mbadala zaidi ya kutoa kifungo
cha maisha tu.
"Ni
kweli washtakiwa ni wakosaji wa kwanza lakini sheria inatoa adhabu kwa
makosa haya na kwa kuwa sheria haijatoa mwanya kwa mahakama kutoa
huruma, ninawahukumu kifungo cha maisha gerezani na pia vielelezo
ikiwemo gari aina ya discover waliyokutwa nayo washtakiwa inataifishwa
na kuwa mali ya serikali." Amesema Jaji Luvanda.
Aidha
upande wa utetezi umeeleza nia yao ya kukata rufaa huku wakiomba
wapatiwe nakala ya hukumu haraka kwa ajili ya kuanza maombi ya rufaa
hiyo.
Katika
kesi hiyo Shamimu ambaye ni mmiliki wa blogu ya 8020 fashion na mumewe
mfanyabiashara Abdu Nsembo wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye
mashtaka mawili ya kusafirisha na kujihusisha na biashara ya dawa za
kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa gramu 232.70 kosa walilolitenda
Mei 1, 2020 katika eneo la Mbezi Beach Mkoani Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment